KINGUNGE NGOMBALE-MWIRE ATOA USIA KWA WABUNGE, WAFIKIRIE TANZANIA NA HATIMA YAKE
MJADALA wa wazi wa Bunge Maalumu la Katiba kuhusu Rasimu ya Katiba inayopendekezwa, umehitimishwa jana kwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge, Samia Suluhu, kuruhusu wajumbe wazee watoe neno la maridhiano.
Akizungumza baada ya kupewa nafasi, mjumbe mzee kuliko wote, Kingunge Ngombale-Mwiru, alitaka wajumbe wasiangalie mambo binafsi ambayo hayakuwekwa katika Katiba Inayopendekezwa, bali waangalie matakwa ya nchi.
“Wananchi wanataka Katiba, tusije tukazuia Katiba bora kwa sababu tunataka kila kitu kingie katika Katiba. Nataka tufikirie nchi yetu na hatima yake.
“Ili Katiba hii ipite, lazima ipate theluthi mbili Tanzania Bara na theluthi mbili Zanzibar na hapa maana yake ni kura…kitendo cha kusema Mh, tunaweza kukwama na mkwamo huo hauna tija kwa wafanyakazi, wafugaji, wavuvi, wachimbaji wadogo na wanawake,” alisema.
Alisisitiza yaliyowekwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, yanatosha kufanya Tanzania ipige hatua mpya katika miaka hamsini ijayo.
Akielezea ubora wa Katiba inayotakiwa na wananchi, Kingunge alisema wajumbe wote kwanza watambue kuteuliwa kwao na makundi yao kwa upande mmoja na Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, kwa upande mwingine, hatimaye wametumwa na wananchi, ambao wanataka Katiba mpya.
Katiba hiyo ili iwe bora kwa mujibu wa Kingunge, inatakiwa iimarishe mafanikio ya miaka 50 ya Tanzania, na hili kufanikisha hilo, ndio maana Bunge hilo lilikataa muundo ambao ulikuwa ukielekea kusambaratisha nchi.
Kigezo cha pili cha Katiba bora, Kingunge alisema ni uwezo wake wa kuondoa kero za wananchi.
Alitoa mfano wa uamuzi wa Bunge Maalumu la Katiba, kurudisha nafasi ya Rais wa Zanzibar, kuwa Makamu wa Pili wa Rais.
“Uamuzi wetu wa nyuma (kumwondoa Rais wa Zanzibar katika nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania), ulikuwa na upungufu…tuliangalia zaidi ujio wa vyama vingi na kusahau walioungana walikuwa pande mbili za Zanzibar na Tanganyika,” alisema na kusisitiza kwa mabadiliko hayo, Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ni bora.
Eneo lingine la Katiba bora kwa mujibu wa Kingunge, ni Katiba husika kuingiza mambo mapya ambapo kwa sasa Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, imeimarisha nafasi ya wananchi katika nchi.
“Ndio maana tunazungumzia haki kwa mara ya kwanza ya wakulima, wafugaji, wachimbaji wadogo, wanawake, vijana, walemavu na makundi mengine,” alisema.
Alisema baada ya mkutano huo wa Bunge Maalumu la Katiba, Tanzania haitakuwa kama ilivyokuwa nyuma, kwa kuwa makundi yote ya jamii, yamekutana na kufanya uamuzi.
Wasioridhika Hata hivyo, Kingunge alizungumzia uwezekano wa kuwepo makundi ya watu ambao hawataridhika na uamuzi huo, kwamba bado watakuwa na nafasi ya kuendeleza mjadala nchi nzima.
Alisema pamoja na hayo na kwa sababu ya mambo mapya yaliyowekwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa, mambo hayo yatoshe kusababisha wajumbe hao wapige hatua mpya.
Zanzibar Mjumbe John Cheyo, alisema mambo yaliyowekwa katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa ya manufaa kwa wakulima, wafugaji na makundi mengine ya jamii, yanamshawishi apige kura ya Ndiyo.
Hata hivyo alisema Zanzibar katika Katiba hiyo ndio yenye kura ya turufu na wameomba mambo mengi katika Rasimu ya Katiba Inayopendekezwa na kupatiwa, lakini wakikataa kutoa theluthi mbili, watakuwa wamewanyima haki Watanzania Bara.
“Mmeomba kukopa tukasema sawa, mkaomba kudhaminiwa tumesema sawa. Tumetoa… tumetoa… tumetoa, haiwezekani upokee kila kitu, lazima mjifunze kutoa.
“Nyie Zanzibar mpo milioni moja, huku Tanzania Bara tupo zaidi ya milioni 40, mkitunyima Katiba mtakuwa mmetuonea na tusipoipata, watu wengi wataendelea kudai Tanganyika.
“Hili la Tanganyika tumelizima hapa…kuna mambo mengi ya vijana, wazee, wanawake, wakulima…sasa nyinyi mkitunyima, tutaona mmetuonea,” alisema Cheyo.
Baada ya kusema hayo, Mjumbe Ramadhan Abdalah Shaaban kutoka Zanzibar, alimtaka Cheyo asiwe na wasiwasi na kura za Zanzibar, kwa kuwa Katiba Inayopendekezwa, itakuwa Katiba.
“Tunashangaa walio ndani (ya Bunge Maalumu) ni asilimia 75, waliotoka nje (kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi, Ukawa) ni kama asilimia 20 eti ndio wanaowakilisha wananchi, kichekesho. “Sisi Zanzibar tuna hakika zaidi ya asilimia 50 tutaipata…sisi majemedari tupo, tumepitia mengi na Mungu akipenda tutafanikisha Katiba,” alisema.
0 comments:
Post a Comment