MTOTO WA MZEE YUSUPH MAKAMBA BADO ANG'ANG'ANIA KUWANIA URAIS 2015 NDANI KUPITIA CCM.
NAIBU Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba amesema hakuna mwanasiasa yeyote anayemhofia kuwa kikwazo katika harakati zake za kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kutangaza nia hiyo Aprili mwaka huu. Januari alitangaza nia hiyo alipokuwa akihojiwa katika kituo cha Dira ya Dunia kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).
Katika mahojiano maalumu aliyofanya jana na wawakilishi wa vyombo mbalimbali vya habari wa mjini Iringa waliotaka ufafanuzi kuhusu nia yake hiyo Makamba alisema;
“Huu ni msukumo wangu unaotokana na dhamira yangu ya dhati ya kuleta aina mpya ya uongozi utakaosaidia kuipeleka nchi mbele zaidi na nimejipanga kushinda.”
Alikutana na wanahabari hao ikiwa ni siku moja baada ya kushiriki mahafali ya 13 ya shule ya sekondari Mtera inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Iringa.
Kutumiwa na Lowassa January alitumia fursa hiyo pia kukanusha uvumi wa baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa wanaodai kwamba anatumiwa kisiasa na Waziri Mkuu wa zamani ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa anayetajwa pia kuwania nafasi hiyo.
“Mimi ni mtu mzima, nina utashi wangu, nina familia yangu, nina mke na watoto, nina jimbo, nina nyadhifa serikalini na kwenye chama, kuniambia mimi nafanya jambo fulani kwa sababu ya mtu fulani ni matusi makubwa sana,” alisema.
Alisema watu wanaosema hayo wanakosea sana na kwa bahati mbaya watu hao hawamjui alivyo na kwamba wanapaswa kumuomba radhi. January ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM alisema;
“huo unaweza kuwa mkakati na mbinu chafu za kumpunguzia mtu mwingine nguvu za kisiasa ili watu wanaokuamini wakate tamaa, hata hivyo huko mbele mambo haya yatajulikana.”
Pamoja na kukanusha kuwa nyuma ya mtu yeyote katika harakati zake hizo, alisema wapo wengine wanaozihusisha harakati zake za sasa na uchaguzi wa miaka mingine ijayo jambo ambalo pia alisema si la kweli.
“Ukiingia kugombea nafasi za uongozi halafu hufanyi kwa dhamira ya dhati ya sasa wewe hufai kabisa kuwa kiongozi; hayo mawili nayasikia na naomba Watanzania wajue kwamba si ya kweli,” alisema.
Uzoefu wa kisiasa Akizungumzia hoja iliyotolewa na baadhi ya wanasiasa wanaodai kwamba ili uwe rais lazima uwe na uzoefu wa miaka mingi wa kisasa, alisema zaidi ya marais waliomaliza muda wao na rais aliyeko madarakani, hakuna Mtanzania mwingine anayeweza kujitapa kuwa na uzoefu wa kushika nafasi hiyo nyeti ya nchi.
“Uzoefu wa kisiasa wa miaka mingi? Hiyo sio hoja kwa sababu unaweza kuwa na uzoefu lakini ukashindwa kuyafahamu na kuyafanyia kazi matatizo ya wananchi,” alisema.
Alisema zaidi ya Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Pili, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa na Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, hakuna mwingine anayeweza kujisifu kwamba ana uzoefu huo.
Akitoa mifano alisema kama uzoefu wa kisiasa kingekuwa kigezo muhimu cha kumpata Rais wa nchi, Mwalimu Julius Nyerere asingeingia kwenye historia hiyo kwani alichaguliwa kushika nafasi hiyo ya uongozi akiwa kijana asiye na uzoefu unaozungumzwa.
“Ipo na mifano mingine ya nje ya nchi. Barack Obama amechaguliwa kuwa Rais wa taifa kubwa kabisa duniani kiuchumi akiwa na uzoefu wa kisiasa wa miaka mitano tu,” alisema.
Alisema ametangaza nia ya kuwania urais wa nchi hii baada ya kujiuliza maswali muhimu matatu, mojawapo likiwa ni kama kazi hiyo ataiweza kwa maana ya kuwa na uwezo wa uongozi, kuwa meneja wa kazi hiyo na kuhamasisha wananchi kuleta maendeleo. Swali lake la pili, Makamba alisema ni kama anaweza kuwaunganisha Watanzania wote bila kujali dini, itikadi wala rangi zao na la tatu kama ana mawazo mapya yanayoweza kusaidia kuleta mabadiliko ya kimaendeleo katika nchi.
“Majibu ya maswali hayo yote ni ndio. Nataka kuona nchi yetu inasonga mbele kwa kasi zaidi. Nina dhamira ya dhati kabisa ya kuleta aina mpya ya uongozi nchini; swali la nne ninalojiuliza ni kama nitaweza kushinda, na swali hilo tunaendelea kulifanyia kazi kwa sababu ni lazima ushiriki kwenye mchezo wenyewe.
Mchakato wa Katiba Aliwataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kuipigia kura ya kuikubali Katiba Inayopendekezwa kwa sababu ina mambo mengi mapya yatakayowasaidia Watanzania kwa ujumla wao tofauti na Katiba ya sasa.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment