BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

FEDHA ZA ESCROW HATA KAMA NI ZA MTU, DENI LIMELIPWA NA WATANZANIA, FEDHA HIZI ZINA MASHAKA MAKUBWA !!!.



 

Kwa ufupi.
Mwanasiasa akitoa takrima anategemea umpigie kura, mtu akiwa anampa mwanafunzi wa kike fedha ya chips na kumpa lifti kwenye gari, maana yake anamhitaji binti huyo mwanafunzi.





Sakata la akaunti ya escrow, ambalo watu wamejichotea fedha kama vile watu wanavyozoa mafuta yaliyomwagika kwenye gari la mafuta lililopata ajali bado lipo midomoni mwa watu.



Wengine tunajiuliza kama kweli mambo haya yametokea katika nchi hii ya walala hoi wengi au ni katika nchi moja tajiri, ambapo kuna utajiri mwingi?


Unajua inashangaza sana kwamba katika nchi tunayoambiwa kwamba ni maskinisana, eti kuna mtu amepewa shilingi milioni moja zidisha mara elfu moja mia sita.


Jamani hii si kufuru? Mwingine anafanyishwa kazi kutoka asubuhi mpaka usiku, hata amesahau masaa halisi ya kumaliza kazi, lakini anapata kipato ambacho hata tarehe ya kumi ya mwezi haifiki.


Mimi najiuliza, hata huyo mtoaji naye ana nini cha ajabu ambacho Mungu amemjalia yeye tu kiasi kwamba fedha zote hizo ziende kwake mpaka awe na za ziada za kugawa wakati wengine wanalala na njaa ?.


Yaani wengine wanashindwa kupata mshahara kwa sababu taasisi zao hazina fedha, lakini yeye fedha inamwendea tu. Iweje fedha hizi?


Jambo hili linaumiza na maumivu haya yanaongezwa na ukweli kwamba mwisho wa siku atakayeathirika na sakata hili ni huyo huyo ambaye saa hizi analala na njaa.


Huu ndiyo ukweli kwa sababu hakuna mtu anayetoa fedha kama hizo bila kutegemea malipo na nikiangalia nyadhifa za watu waliopewa, hasa wale viongozi wa Serikali, nalazimika kuzungumza kwa nguvu kabisa kwamba malipo hayo yalitarajiwa yalipwe na sisi wananchi wa kawaida bila kujali kwamba fedha hizo ni za umma au za mtu binafsi. 


Yupo waziri aliyesema kwamba yeye fedha hizo kapewa kwa ajili ya maendeleo ya shule yake. Pengine ni kweli zilitoka kwa sababu hiyo, lakini je, nini baada ya hapo? Hivi kweli anataka tuamini kwamba fedha alizopewa hazina masharti yoyote? Kama huyo mtu huruma yake iko kwa elimu ya Watanzania kwa nini asizipeleke kwenye shule za kata?


Hakuna mtu anayetoa kitu bila kutegemea malipo yoyote; iwe ni malipo kutoka kwa huyo aliyempa au hata thawabu kutoka kwa Mungu. Lakini thawabu kutoka kwa Mungu inatolewa kama mtu umejitoa kwa moyo kwa kumlishia, kumvishia na kumhifadhia maskini wake. Nasisitiza kutoa kwa moyo kusikokuwa na dhamira nyingine yoyote zaidi ya kuwasaidia hao wasio na nacho.


Hakuna mahali popote katika kitabu kitakatifu ninachokiamini mimi palipoandikwa kwamba mtu atapewa thawabu kwa kumlisha yule ambaye tayari anacho.


Hivyo, bila wasiwasi wowote tunasema mtu huyo aliyetoa zaidi ya bilioni kama mchango wa shule ya mtu binafsi alitegemea kupata kitu kutoka kwa huyo aliyempa.


Tunaweza tukathibitishiwa kwamba fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow ni za mtu binafsi lakini tusikubali kugeuzwa kuwa watoto wadogo kwa kudanganywa kuwa mtoaji wa fedha hizo alitarajia kupata malipo moja kwa moja kutoka kwa mtu aliyempa hizo fedha.


Jamani, mtu anayetoa fedha nyingi hivyo anatarajia kupata kitu kikubwa sana; kikubwa ambacho siamini kama mtu binafsi anacho na angekuwa nacho asingekubali kuchukua fedha ambazo anajua baadaye zitamtokea puani.


Bila shaka mtu huyu alitarajia kutoa kitu ambacho siyo chake bali ni cha watu wengine. Kwa kiwango cha fedha kilichotolewa na kwa nyadhifa walizonazo viongozi hao katika Serikali yetu bila shaka walipokea fedha hizo kwa malipo ya rasilimali za umma, ambazo waliamini wanaweza kuzitoa kwa kutumia mamlaka walizonazo. Jamani hata katika vitu vya kawaida tu mtu anaelewa kwamba akipata takrima yoyote basi kuna malipo ndani yake.


Mwanasiasa akitoa takrima anategemea umpigie kura, mtu akiwa anampa mwanafunzi wa kike fedha ya chips na kumpa lifti kwenye gari, maana yake anamhitaji binti huyo mwanafunzi.


Mbona asitoe lifti kwa watu wanaokwenda kuona wagonjwa wao hospitali naye anawapita asubuhi wanapopeleka chai kwa wagonjwa hao? Jamani tukubali misaada ya namna hiyo ni rushwa na kwa hawa mawaziri wetu tukubali kwamba wamepokea rushwa kubwa hata kama fedha hizo ni za mtu binafsi.


Watanzania tufumbue macho, tuone rushwa hiyo kwa Waziri wa Ardhi inavyoweza kutuathiri. Hivi unajua kwamba nchi hii tuna vichaa. Huyo mwenye mabilioni ndani ya Akaunti ya Escrow anaweza akawa anamezea mate eneo kubwa la Manzese; sasa atalipataje? Mtu mwenye kichaa kama hicho akitoa mabilioni yake atatarajia kupewa eneo hilo la Manzese bila kikwazo cha wakaaji wa huko. 


Sasa wakaaji wa Manzese siyo waziri bali ni Watanzania wa kawaida tu na mwenye mabilioni yake anajua akimchapa nayo usoni waziri, basi waziri atapata upofu, atakosa huruma, kisha atatoa amri ya kuwahamisha wakazi hao kwa kisingizio cha kupisha mradi wa maendeleo kwa jamii wakati anajua kwamba utamwendeleza yeye waziri na huyo mwekezaji.


Wakazi wa Manzese wataishia kupewa fidia ya kulipia pango la nyumba kwa miezi 6. Ndizo hizo mtu anatarajiwa atumie kwa kupanga nyumba wakati anahangaika kupata kiwanja kingine, akanunulie kiwanja na akajenge. Akijitahidi atawajengea nyumba za muda za maboksi au mbao huko kwenye misitu. Yote haya yataendelea wakati waziri mhusika akiwa anaendelea kunufaika na hiyo shule yake.


Inawezekana kabisa malipo yasiwe kupewa eneo la Manzese, lakini kwa malipo yoyote yale Watanzania ndiyo tutakaoathirika kwani malipo yenyewe ni makubwa mno, ambayo mtu mmoja hata kama ni waziri hawezi kuyalipa. Hivyo sote tupaze sauti zetu kwa mitindo tofauti tofauti ili jambo la kwanza kabisa vyombo vilivyowateua viwaondoe madarakani haraka iwezekanavyo.


Ni muhimu sana watu hawa kuondoshwa kwanza madarakani kwa sababu sote tunajua jinsi viongozi wa namna hii wasivyo na aibu, wanaweza kuendeleza azma yao ya kutumia rasilimali zetu kwa njia yoyote ili walipie fedha walizozichukua kama bado hawajafanya hivyo.


Mengine ya mahakamani, kuwafunga ama kuwachukulia hatua nyingine yoyote ile yafanywe baadaye.
Jumapili njema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: