Na Juma Mtanda, Morogoro.
Polisi mkoani Morogoro, wamesema kikundi chochote cha watu kitakachojaribu kuvuruga uchaguzi wa leo wa Serikali za Mita, kitashughulikiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria, washiriki wake.
Akizungumza na waandishi wa habari jana saa 12:30 asububi, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Leonard Paulo alisema polisi wamepokea taarifa za kuwepo kwa kundi la watu waliopanga kuvuruga uchaguzi huo unaofanyika nchini kote leo.
Alisema watu hao wanapaswa kuacha mara moja kujihusisha na vitendo hivyo na kwamba vinginevyo, watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
“Jeshi la Polisi linawatahadharisha na kuwaonya wale wote wenye nia na malengo mabaya ya kuvuruga uchaguzi huu kuwa watashughulikiwa kikamilifu na kwa mujibu wa sheria," alinena Kamanda Paulo..
"Tumeimarisha ulinzi katika vituo vyote vya kupigia kura na tunawahimiza wananchi waliojiandikisha kuwa waende vituoni bila hofu ili wakapige kura zao bila hofu," alisisitiza.
Alisema ulinzi katika siku ya leo, unafanywa kwa ushirikiano wa polisi, vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wadau wa amani.
Kamanda huyo aliwataka wananchi waliojiandikisha kupiga kura katika uchaguzi huo, kujitokeza kwa wingi na bila hofu ili kutekeleza haki yao hiyo ya msingi.
Pia aliwataka wananchi kutoa taarifa kwa polisi kuhusu kikundi chochote kitakachobainika kuwa na mpango wa kutaka kuvuruga uchaguzi.
0 comments:
Post a Comment