YANGA SC YATELEZA NA KUKALIA KUTI KAVU, KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA DHIDI YA ETOILE SPORTIVE DU SAHEL, SARE YA BAO 1-1 YAIWEKA NJIA PANDA.
Kipa wa Etoile Sportive du Sahel, Mathlouthi Aymen akimchezea rafu winga wa Yanga, Simon Msuva (aliyelala kifudifudi) na mwamuzi wa Msumbiji, Samwel Chirindza (kulia) akiashiria kuwa ni penalti ambayo ilipigwa na Nadir Haroub na kuipatia timu yao bao la kuongoza katika mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana. Timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1. (Picha na Rahel Pallangyo).
YANGA itakuwa na kibarua kigumu mjini Sousse nchini Tunisia baada ya jana kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Etoile Sportive du Sahel (ESS) katika mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sare hiyo inaifanya Yanga kuwa na mlima mkubwa wa kupanda kwenye mchezo wa marudiano utakaopigwa wiki mbili zijazo kwenye Uwanja wa Olympique de Sousse mjini Sousse.
Ushindi wa mabao yoyote au sare ya kuanzia mabao 2-2, utaifanya Yanga isonge mbele huku Etoile wakionekana kuwa na kazi nyepesi ya kupata sare ama ushindi ili kutinga hatua inayofuata.
Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliipeleka Yanga mapumziko ikiwa inaongoza kwa bao alilolifunga dakika ya kwanza kwa penalti baada ya kipa wa ESS, Mathlouthia Aymen kumuangusha Simon Msuva, ndani ya eneo la hatari wakati akijaribu kumpiga chenga, kutokana na pasi nzuri ya Haruna Niyonzima.
Etoile walikianza kwa kasi kipindi cha pili na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Ben Amor Med Amine, dakika ya 46 baada ya kupiga shuti kali la mbali lililomshinda kipa wa Yanga, Ally Mustapha ‘Barthez.’
Katika kipindi cha kwanza, Yanga ilionesha kwa kucheza kwa kuelewana katika dakika moja na kupata bao hilo lilitokana na kazi nzuri ya Niyonzima, lakini baada ya hapo wageni Etoile walikuja juu na kuutawala mchezo kwa sehemu kubwa ya kipindi hicho.
Mshambuliaji wao, Bouned Jah Baghdad ambaye kabla ya mchezo huo kuanza, alionekana kutokuwa fiti kutokana na kutapika uwanjani, alipoteza nafasi nyingi za mabao alizozipata kipindi cha kwanza ikiwemo ile ya dakika ya tisa ambapo mpira wa kichwa alioupiga ulidakwa na kipa Mustapha.
Mustapha alilazimika kufanya kazi kubwa katika dakika ya 29 baada ya kupangua shuti la Mouihbi Youssef, aliyekuwa ndani ya eneo la hatari na Kelvin Yondani kuondosha mpira huo kwenye hatari.
Kipindi cha pili, Yanga ilimtoa Haroub aliyekuwa ameumia kifundo cha mguu kipindi cha kwanza na nafasi yake ikachukuliwa na Said Juma ambaye aliipa uhai Yanga na kuanza kucheza kwa kasi na kutengeneza nafasi kadhaa, lakini Amissi Tambwe na Simon Msuva hawakuzitumia.
Dakika ya 61, Mrisho Ngassa alimtengenezea nafasi nzuri Msuva ambaye naye aliachia shuti kali lililopanguliwa na kipa Aymen na mabeki kuondosha mpira huo kwenye hatari.
Tambwe aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 84, baada ya kupokea pasi nzuri ya Ngassa, lakini mwamuzi Samwel Chirindza wa Msumbiji, alilikataa baada ya mshika kibendera namba moja, Arsenio Marenguka kudai mfungaji alikuwa ameotea, ingawa kwa wengi alionekana hakuwa ameotea.
Mshika kibendera huyo aliwakera mashabiki wa Yanga tangu kipindi cha kwanza na yeye na waamuzi wenzake wote kutoka Msumbiji walitoka chini ya ulinzi mkali kipindi hicho na pia mchezo ulipomalizika.
Aidha, Yanga ilipata pigo katika dakika ya 85, baada ya beki wa kulia, Juma Abdul kutolewa nje baada ya kuumia na nafasi yake kuchukuliwa na Rajab Zahir na hivyo Mbuyu Twite aliyeanza kama kiungo jana, alihamishwa tena kutoka beki wa kati na kwenda kucheza nafasi ya Abdul huku Zahir akicheza kati na Yondani.
Yanga: Mustapha, Abdul, Oscar Joshua, Harou/Makapu, Yondani, Mbuyu Twite, Hassan Dilunga/Kpah Sherman, Niyonzima, Tambwe, Ngassa na Msuva.
0 comments:
Post a Comment