
Aliyekuwa mgombea wa ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Jimbo la Itilima, mkoani Simiyu, Martine Makondo, amekihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Wananchi (Cuf) na kisha kutangaza kuwania nafasi hiyo kupitia chama chake hicho kipya.
Hata hivyo, Makondo alilazimika kuchukua, kujaza na kurejesha fomu yake ya ubunge kupitia Cuf chini ya ulinzi mkali wa polisi baada ya baadhi ya wanachama wa Chadema kukasirishwa na mgombea huyo kukihama chama hicho.
Mgombea huyo amehama Chadema siku chache baada ya jina lake kuenguliwa na vikao vya juu vya maamuzi vya Chadema licha ya kwamba aliongoza katika kura za maoni ya chama hicho kwa kupata kura 374 na kumshinda mpinzani wake Martine Mukuja aliyepata kura 120.
Licha ya matokeo katika kikao cha kamati tendaji ya chama hicho kuonyesha Makondo alipata kura tisa na Mukuja kura tatu, jina la Makondo liliondolewa na kurejeshwa jina la Mukuja kama mgombea ubunge wa Jimbo la Itilima na matokeo hayo kutangazwa Agosti 19, mwaka huu.
Kufuatia uamuzi huo, wanachama wa Chadema katika wilaya ya Itilima walilalamikia hatua hiyo na kuzua mtafaruku na kumshawishi Makondo kukihama chama hicho.
Hata hivyo, wakati Makondo akijiunga na CUF na kujaza fomu za kuwania ubunge kupitia chama hicho, baadhi ya wanachama wa Chadema na wananchi wa jimbo hilo walipoonyesha misimamo tofauti hali iliyosababisha kuwapo kwa vurugu na polisi kulazimika kutoa ulinzi kwa mgombea huyo hadi akirejesha fomu kwa Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo.
Akizungumza na NIPASHE, Makondo alisema amelazimika kukihama chama hicho baada ya kutoridhishwa na mwenendo mzima wa uteuzi ulivyofanyika.
Juhudi za Nipashe kuwapata viongozi wa Chadema Jimbo la Itilima kuzungumzia suala hilo zilishindikana baada ya kukosekana ofisini kwao lakini juhudi za kuwatafuta zinaendelea. Jimbo la Itilima linawaniwa na wagombea, Makondo (Cuf), John Cheyo (UDP), Njalu Silanga (CCM) na Martine Mukuja (Chadema).CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment