MGOMBEA
urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema yeye ndiye anayetosha
kupambana na umaskini wa wananchi huku Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick
Sumaye, akiitaka CCM ianze kuondoa hirizi Ikulu kama zipo kwa vile
Ukawa wanaingia madarakani.
Waliyasema hayo kwenye mikutano ya kampeni iliyofanyika wilayani Temeke Dar es Salaam jana.
Akizungumza katika mkutano uliofanyika Uwanja wa Tungi Kigamboni, Lowassa alisisitiza lengo lake ni kupambana na umaskini.
“Nitaanza
na elimu kutoka shule ya watoto wadogo hadi elimu ya juu ambayo
itakuwa ni bure… elimu ni muhimu kuanzia kwa mtoto mdogo hadi elimu ya
juu.
“Baada ya elimu kinachofuata ni kilimo cha kisasa cha
umwagiliaji, kufungua akaunti maalumu kwa ajili ya mama lishe,
wamachinga na bodaboda , kufungua viwanda kwa ajili ya ajira kwa vijana.
“Mkinichagua baada ya kuapishwa nitaanza na kivuko cha feri
ambako wananchi mtavuka bure bila malipo yoyote,” alisema Lowassa.
Akiwa
kwenye mkutano uliofanyika katika viwanja vya Chanika Magengeni
wilayani Temeke, alisema anawashangaa baadhi ya watu wanaofuatilia
safari zake zikiwamo ziara zake sokoni na kwingineko wakati
wanaosafirisha wanyama hai nje ya nchi wakiwamo twiga, hawahojiwi.
Alisema
hata alipopanda daladala baadhi ya watu walihoji kitendo hicho lakini
bado wamekuwa hawahoji waliopeleka twiga nje ya nchi.
Lowassa alisema kwa sasa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wamechoka
kula mlo mmoja na kwamba wanahitaji maisha mazuri ambayo watayapata kwa
kufanya mabadiliko.
“Wananchi wanahitaji mabadiliko na maisha
mazuri, nina imani fedha za kufanya haya yote zipo …tutatoa elimu bure
kuanzia shule za watoto wadogo hadi Chuo Kikuu kwa kuwa uwezo huo upo,
kama fedha hamna mbona mashangingi kila siku yanaongezwa?” alisema
Lowassa.
Sumaye
Naye Sumaye alisema ni vema
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kijiandae kuachia Ikulu na kama kuna kirizi
kilizoweka kizitoe kwa sababu Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
wanaingia madarakani.
“Kama kuna hirizi ama kitu kingine ambacho
wamekisahau, sasa muda umefika watoe kila kilicho chao kwa sababu Ukawa
wanaingia madarakani,” alisema Sumaye.
Alisema mgombea urais
wa CCM, Dk. John Magufuli ni sawa na mtu aliye kwenye kitanda ambacho
kina wadudu ikizingatiwa chama chake kilivyo hivyo kumchagua ni
kuendelea kupoteza mwelekeo wa maendeleo.
“Kitanda chenye wadudu
kinachomwa moto, hivyo Magufuli anafananishwa na kitanda hicho …kama
vipi aje Ukawa akishindwa tutamtupa porini na kitanda chake,”alisema
Sumaye.
Sumaye alisema nchi ipo katika kipindi ambacho wananchi
wenyewe wana hiari ya kuamua kujikomboa au kubaki katika shida huku wana
CCM wakiendelee kushiba.
Alisema ana imani wananchi wanahitaji mabadiliko lakini kwa kuichagua CCM hakuna matumaini mbele yao.
“CCM
lazima iondoke madarakani, haiwezi kuangalia afya ya wananchi … ni aibu
mno eti Dar es Salaam tunaugua kipindupindu ni aibu sana,”alisema
Sumaye.
Alisema anamshangaa Magufuli kudai eti nchi ni yake wakati hajapata ushindi na kuhoji endapo atapata ushindi wao wataishi wapi.
“Namshangaa Magufuli kusema nchi yake, je akishinda sisi wengine tutajificha wapi?” alihoji Sumaye.
Alisema
pia kwamba CCM inatoa maneno ya vitisho kwa wananchi lakini wao Ukawa
hawasumbuki bali watafanya siasa ya amani na demoktasia.
Alisema watakaosababisha machafuko ni CCM kwa kukataa demokrnasia ya wanachi kwa sababu Ukawa wanahitaji amani.
Mgombea
ubunge wa Kigamboni, Lucy Mageleli alisema Lowassa ni kama Musa
aliyekuja kuwakomboa watu wa Kigamboni kutoka utumwa wa CCM.
Alisema
Serikali ya Lowassa ikiingia madarakani itahakikisha umaskini kwa watu
wa Kigamboni unaisha na Mungu atawapa nchi yenye asali na maziwa.
“Wananchi
kivuko siyo starehe ni sehemu yetu na ni haki yetu hatutakiwi
kukilipia, pia hayo magari ya Ridhiwani yanayoegeshwa hapo kusubiri
wamanchi tutakapoingia madarakani yataondoka na tutabakia na daladala
zetu za Buguruni, Mbagala na Gongo la mboto.
Duni
Naye
mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma haji Duni, alisema taifa linahitaji
mabadiliko ya fikra kwa kupata elimu bora, nafasi mpya ya kufikiri
akisema CCM imeshindwa kutekeleza ahadi zake.
Alisema mwaka
2005 Rais Jakaya Kikwete alipokuwa anataka urais aliahidi kuleta maisha
bora kwa kila Mtanzania lakini hali hivi sasa imekuwa mbaya zaidi ya
awali.
“Hata huyo Magufuli kwanza hatufai kwa kuwa yeye kila
kitu anashangaa tu kama ilivyo kwa mwenzake ambaye alikuwa anacheka
twiga wanaondoka, yeye anacheka… kila kitu yeye anacheka tu.
“Tunahitaji
mabadiliko tena ya fikra … inatupasa kupata elimu hivyo ni lazima kila
mtu apate haki hiyo na Lowassa si mtu wa kuchekacheka,” alisema.
Mbowe
Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wananchi wamekubaliana kuwa mwaka
2015 wamechoka maumivu na wanachohitaji ni mabadiliko tu.
“Wananchi wamechoka, wanahitaji mabadiliko na ndiyo maana hata sisi tumesimamisha mgombea mmoja tu wa Ukawa,”alisema Mbowe.
Akifafanua
kuhusu mkanganyiko wa mgawanyo kwa wagombea katika kuwania udiwani na
ubunge katika Ukawa, alisema kauli ya wengi ni ya Mungu, kwa pamoja
walikaa na kuamua kumsimamisha mgombea mmoja kutoka chama chochote
anayekubalika katika kila kata na jimbo.
Mbowe alisema ili waende na kasi ya mabadiliko ni lazima wapate mgombea makini na anayekubalika kwa umakini wake.
“Natoa
saa 48 kwa viongozi mbalimbali kufanya uamuzi wa kuwapitia wagombea
ambao wana sifa… awe wa chama chochote ili mradi wa ushirika wetu na
atakayekiuka haya tutamfukuza, hatuna haja ya kubembelezana,”alisema
Mbowe.
Hata hivyo, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuona
umuhimu wa kushughulikia kauli iliyotolewa na kiongozi mmoja wa CCM
aliyedai CCM kitaachia majimbo yote na kata lakini si Ikulu.
MABANGO
Wananchi hao muda wote walikuwa wakishangilia huku waionyesha mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali.
Baadhi
yaliandikwa, ‘Toroka uje Ukawa ndiyo mpango mzima’, ‘Malofa katika
ubora wetu’, ‘Vijana Chanika tulitumika na CCM sasa zamu ya Ukawa’,
‘Tumeikataa CCM jumla tunataka mabadiliko’, ‘Wazee wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki tusaidiwe’.
Mengine yalisomeka, ‘Magufuli huwezi
kuitengeneza injini ya gari ukiwa ndani ya gari bovu shuka uichungulie
injini hiyo…hamia ukawa’.
Mengine yalisema, ‘Tunamchagua Lowassa
kutoka UKAWA maendeleo yatakuja’, ‘mchawi mpe mwana akulelee’, ‘heri
Kipindupindu kuliko CCM’, ‘miaka 50 ya kudanganywa inatosha’, ‘M4C bado
tuna imani na Lowassa hatuyajali maneno mnayoyasema wembe ni ule ule’ na
wengine walikuwa na msalaba uliokuwa umeandikwa ‘John Pombe Magufuli
kuzaliwa mwaka 1961 kifo 25, Oktoba 2015’.MTANZANIA
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / siasa /
slider
/ LOWASSA AJIGAMBA KUWA YEYE NDIYE ANAYEFITI KUPAMBANA NA UMASIKINI TANZANIA NA SIYO MGOMBEA MWINGINE NGAZI YA URAIS.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment