BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

KOBE, KASA NA MIJUSI WOTE WAMO KATIKA MSAFARA WA MAMBA, TUMEJIULIZA KISA CHA DK SLAA KUACHANA NA UKATIBU UKUU AMA LOWASSA KUINGIA CHADEMA ?.


Na Hawra Shamte.

 
Leo nataka kukumbusha kidonda: Kadhia ya Dk Willibrod Slaa na kujiuzulu nafasi ya Katibu Mkuu, Chadema. 


Ni jambo ambalo wengi wanaliona kuwa lishapita, kweli limepita, lakini kutafakari mambo yapitayo kwa kina ni muhimu kwa sababu ndani yake huwa tunapata mafunzo.

Najiuliza hivi Josephine Mushumbusi (mchumba/mke) wa Dk Slaa alikuwa na fikra gani wakati ‘mume’ wake alipotingwa katika mkwamo wa kisiasa? Je, ni kwa kiasi gani alichangia uamuzi wa mumewe kujiuzulu?

Ingawa mwenyewe alikana kuwa hajamfungia mumewe wakati wa sakata zima la kawa, lakini hata kama alimzuia kutoka ndani ya nyumba au alimshauri ajiuzulu kwa sababu zozote zile, binafsi nampongeza kwa kuchukua hatua hiyo.

Nachukua nafasi hii kumpongeza Josephine kwa sababu kweli ni mwanamke wa shoka, mwenyewe alisema yeye ni ‘strong’ (ana nguvu) bila shaka hizo si nguvu za kupigana wala kuangushana mieleka bali ni nguvu za hoja, alikuwa anamaanisha kuwa yeye ni mwanamke mwenye kujiamini na anayeweza kushawishi apendapo kufanya hivyo.

Ikiwa alitumia nguvu zake za ushawishi kumzuia mumewe asiendelee na Ukawa, bila shaka alipima faida na hasara, inakuwaje wengine wanashindwa kufanya hivyo? Niliangalia Kamusi ya Kiswahili Sanifu, neno ‘liability’ wamelitafsiri kuwa ni ‘kuwiwa.’ Kuwiwa maana yake ni kutingwa au kukwazika.

Je, Josephine yeye alikwazika na nini? Dk Slaa kushindwa kugombea urais au Edward Lowassa kujiunga na Ukawa? Wapo waliosema kwamba alitamani kuwa ‘mke wa rais.’ Si vibaya kutamani na haina maana kwamba mtu akikosa anachokitamani achukie. 


Imani yangu ni kuwa Josephine hakuchukia, lakini kwa maelezo yake pia hakutilia maanani, kwa sababu halikuwa jambo lililomshughulisha.

Mwenyewe alisema Dk Slaa ana uamuzi wake na yeye (mke) ni mshauri tu. Anasema: “…siku moja alikuja nyumbani akaniambia uamuzi aliouchukua, nami sikuwa na la kusema, nilichukua shuka nikajifunika.”

Pengine kuwiwa kwa Josephine kumemsaidia Dk Slaa kutoa uamuzi wa busara kwa sababu aliuangalia upepo akaona unaelekea kusikoeleweka. 


Kama suala ni urais, Dk Slaa alisema kuwa ingelikuwa ndiyo jambo muhimu kwake, angejitangaza mapema kuwa ndiye mgombea wa Chadema, lakini alichukua muda kwanza wa kutafakari. Pengine kwa njia moja au nyingine, Josephine alimsaidia kufikiri.

Pengine aliyoyasema Dk Slaa siku alipotangaza rasmi kujiuzulu nafasi ya Katibu Mkuu wa Chadema, ni machache kuliko aliyoyahifadhi. 


Pengine alibakisha mengi kuliko tunavyofikiria, na ikiwa miongoni mwa mambo aliyoyabakisha ni hili la Josephine kujifunika shuka, binafsi nadhani Dk Slaa alifanya uamuzi wa busara, aliangalia mbali, yeye hakufikiria tu kuingia Ikulu, bali alifikiria faida na hasara au kwa maneno mengine, ‘aliwiwa.’

Ingelikuwa Dk Slaa ameendelea kushika nafasi yake na kuwa kiririni akimnadi yule aliyemsema kwa kinywa kipana mchana wa jua kali kadamnasini kuwa ni miongoni mwa watu aliowaita ‘wezi,’ ingelikuwa mbaya zaidi kwake kuliko ilivyo mbaya kwa Tundu Lissu, Freeman Mbowe na wengineo ambao hivi sasa mgombea wao wanamuona mweupe kama alfajiri, hana doa wala toa na wamesahau kama waliwahi kumsulubu.

Hivi sasa sentensi zinabadilika, badala ya kusema: “Hatutaki kiongozi anayetuhumiwa kuwa mla rushwa na fisadi,” sasa wanasema: “Usafi siyo kila kitu katika siasa, muhimu ni kuwa na mikakati ya ushindi.”

Alaa, kumbe sasa hivi wizi, ufisadi, kula rushwa ni ruksa? Hawa wanatukumbusha enzi za Mzee Ruksa aliposema kuwa ukitaka kula nyama ya ngombe, ruksa, ukitaka kula kuku, ruksa na ukitaka kula…. ruksa ili kuepusha shari iliyokuwa imetanda. Hivyo tunachokiona hivi sasa: kobe, kasa, mijusi wote wamo katika msafara wa mamba kwa sababu ruhusa imeshatolewa.

Hivi leo ndio tunajua kuwa “kutu ya kale, hainuki,” hivi sasa ndiyo tunatambua kuwa “yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.” Lakini inashangaza kasi ya mabadiliko kutoka baya kwenda jema, imekuaje?

Natamani Dk Slaa angelikuwapo akapanda tena kiririni na kututajia orodha ya mafisadi na asiishie hapo tu, bali aseme na walichokifisidi. 


Pamoja na yote hayo, nakubaliana na ile dhana ya kuwa hakuna mbaya wa kudumu wala mwema wa kudumu, pengine huyo ambaye wakati mmoja alionekana mbaya mbele ya macho ya watu, hivi sasa macho hayo hayo ya watu yanamuona mzuri. Ila sasa wanapaswa watuthibitishie uzuri wake bila kigugumizi na bila kuwa na mkwamo.

Walishindwa kumthibitishia Dk Slaa uzuri/usafi wa huyo mtu na wala hawakubainisha faida na hasara za yeye kuingia Ukawa mpaka akaamua kuondoka jahazini na kusepetukia pembeni. Kama kawaida maneno ya wasemaji ni mengi, amepewa hongo, amenunuliwa…, hivi jamani mtu hawezi kuwa na mawazo yake huru mpaka ahongwe, atumwe au anunuliwe?

Wanashangaa kubadilika ghafla kwa Dk Slaa, kutoka kuwa mkaribishaji mpaka kuwa mhamaji, lakini wanasahau kushangaa kubadilika kwa Edward Lowassa ndani ya kipindi kifupi tu, kutoka kukatwa CCM mpaka kujiunga na Chadema. 


Hawaulizi alifikiri kwa muda gani, hawaulizi mabadiliko ya kauli kutoka: “Wanaotaka niondoke CCM, wataondoka wao,” mpaka “CCM si mama yangu…,” imekuwaje? Ni kazi kuyadadavua mabadiliko ya kifikra, kimtazamo na kiitikadi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: