WAZIRI CELINA KOMBANI KUZIKWA JUMATATU MKOANI MOROGORO, SIMANZI ZATAWALA WAKATI WA MAPOKEZI WA MWILI WAKE.
Dar es Salaam. Huzuni, simanzi na majonzi jana vilitawala Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakati mwili wa Celina Kombani, aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, ulipowasili.
Celina alifariki dunia Septemba 24, katika Hospitali ya Appolo nchini India alikokwenda kwa matibabu.
Mwili uliwasili kwa ndege ya Shirika la Emirates na kulakiwa na viongozi mbalimbali wa CCM na Serikali, ndugu, jamaa na marafiki.
Mara baada ya jeneza lililokuwa na mwili kutolewa ndani ya ndege hiyo, sauti za vilio ziliongezeka, baadhi ya watu waliofika uwanjani hapo wakilia kilio cha kwikwi huku machozi yakimininika.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah aliwaambia waandishi wa habari uwanjani hapo kwamba mwili huo utahifadhiwa Hospitali ya Lugalo kwa ajili ya utaratibu na ratiba nyingine zitakazofuata kabla ya maziko.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Kailima Kombwey alisema shughuli zote za kampeni kuhusu nafasi ya ubunge katika Jimbo la Ulanga Mashariki zitasitishwa kama Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka 2010 zinavyoeleza.
“Kwa hivyo uchaguzi wa ubunge ndani ya jimbo utafanyika baada ya uchaguzi mkuu,” alisema Kombwey. Katibu mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema chama hicho na Serikali vimepoteza kiongozi muhimu aliyekuwa mfuatiliaji, mtendaji na mwadilifu katika majukumu yake.
“Lakini familia inasikitika zaidi kwa kumpoteza mpendwa wao. Jimboni tuliamini ushindi wake,” alisema Kinana.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema aliwasiliana mara ya mwisho na waziri huyo kabla mauti hayajamfika na walizungumzia mipango ya kuimarisha huduma ya mawasiliano jimboni kwake.
Naye mtoto wa Kombani, Goodluck Millinga alisema mwili wa mama yake utaagwa keshokutwa kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Ulanga Mashariki mkoani Morogoro kwa ajili ya kuagwa.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment