WAANDISHI ENDELENI KAZI ZA MPOKI BUKUKU, KUZIKWA LEO DODOMA.
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ametoa pole kwa familia, ndugu na waandishi wa habari nchini kwa msiba wa Mpoki Bukuku (44).
Amesema ameondoka bado yapo mambo mengi makubwa, ambayo waandishi nchini wanaweza kujifunza na kuyaendeleza kutokana na kazi zake.
“Mpoki alikuwa mtu muhimu na nguzo muhimu katika tasnia ya habari. Kuna kazi nyingi amefanya na pia kuna watu wengi wamepitia katika mikono yake. Tujifunze na tuendeleze kazi hizo. Kwa niaba ya wizara na kwa niaba ya serikali natoa pole kwa mke, watoto, familia, ndugu na waandishi wote wa habari kwa msiba huu mkubwa,” amesema Waziri Nnauye.
Alisema hayo alipotoa salamu za rambirambi Dar es Salaam jana, alipowaongoza mamia ya waandishi kumuaga Bukuku katika Shule ya Sekondari Tabata iliyopo Kimanga. Bukuku alikuwa mpigapicha mwandamizi wa Kampuni ya The Guardian Limited.
Alifariki dunia wiki iliyopita. Waziri Nnauye alisema yeye binafsi amemfahamu Mpoki siku nyingi kama rafiki, kaka na ndugu wa karibu; na kwamba kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia, ndugu na tasnia ya habari kwa jumla.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alisema anatoa pole kwa familia, ndugu na waandishi wa habari kwa msiba huo mkubwa.
Mbowe alisema Mpoki ameondoka baada ya kukamilisha wajibu wake kwa familia yake na Taifa; na katika maisha yake alijitahidi mno kujenga jamii na urafiki kwa watu wengi.
Alisema waandishi wana wajibu mkubwa kwa Taifa kwa kusema ukweli, kukosoa pale panapostahili na kuwa jasiri, mambo ambayo Mpoki aliyafanya. Aliomba familia na waandishi wa habari nchini kuwa jasiri na kuwa na moyo wa subira katika kukabili pengo aliloacha mpigapicha huyo maarufu.
“Waandishi wa habari tuyatafakari maisha yake na kukumbuka kazi zake alizofanya kwa weledi na umakini,” alisema Mbowe, ambaye ni mbunge wa Hai. Mpoki ni mtoto wa tano katika familia yao, ambayo kwa sasa inaishi Msalato, nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Alisoma shule za msingi Forodhani jijini Dar es Salaam, Mlimwa mjini Dodoma na Kisarawe.
Elimu ya sekondari aliipata katika Shule ya Mtaala wa Kiingereza ya Stockley (sasa Canon Andrea Mwaka) iliyopo mjini Dodoma na kisha Makumira mkoani Arusha.
Alipata masomo yake ya uandishi wa habari katika Chuo cha Uandishi wa Habari cha TSJ, Dar es Salaam na kisha kuajiriwa na gazeti la Majira.
Alipoacha Majira aliajiriwa na Kampuni ya Mwananchi alikofanya kazi kwa miaka kadhaa.
Mwaka jana alijiunga kampuni ya The Guardian Limited, alikofanya kazi hadi mauti yalipomkuta, Ameacha mke na watoto watatu.
0 comments:
Post a Comment