BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WATANZANIA 2,994 WAPOTEZA MAISHA MWAKA 2016 KWA AJALI ZA BARABARA 9,151.


NI miezi 12 ya vilio. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Watanzania zaidi ya 2,000 kufariki dunia, huku wengine wakipata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali za barabarani 9,151 nchini.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, hadi kufikia Novemba 30, mwaka huu Watanzania 2,994 walifariki kwa ajali zilizohusisha mabasi, malori, magari madogo, bajaji na bodaboda.

Akizungumza na MTANZANIA jana katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi Mohamed Mpinga, alisema mwaka huu imekuwa tofati na mwaka jana ambako zilitokea ajali 8, 337 ikiwa ni pungufu ya ajali 814.

Kutokana na hali hiyo, alisema ipo haja kwa Watanzania kuendelea kuchukua hatua za kudhibiti ajali kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ikiwa ni pamoja na kudhibiti madereva wakorofi ambao wamekuwa wakivunja sheria za usalama barabarani.

“Ukiangalia takwimu hizi za ajali hadi kufikia Novemba mwaka huu, ajali zilizotokea ni 9,151 ambazo zimehusisha mabasi, bodaboda na magari binafsi.

“Kwa upande wa vifo 2,994, vifo vya bodaboda ni 820 na majeruhi ni 1,998 huku kwa upande wa mabasi na magari binafsi vifo ni 2,174 na majeruhi 6,362.

“Kwa kweli bado tunatakiwa kushirikiana, nasi kama jeshi tunataka kuona Watanzania wakiendelea kusafiri na kufika salama mahala wanapokwenda kwa kutumia magari yao,” alisema.

Kamanda Mpinga alisema kwa kipindi cha mwaka jana zilitokea ajali 8,337 huku majeruhi wakiwa 9,383 na vifo 3,468.

“Kwa kipindi cha mwaka jana ajali za pikipiki au bodaboda zilikuwa 2,626 na kusababisha vifo 934. Hapa utaona kuna pungufu la vifo vya watu 114, kwahiyo ukiangalia hapa bado tunaendelea kupambana ili kuondoa hali hii.

“Kama Jeshi la Polisi tumekuwa tukichukua hatua mbalimbali ikiwamo kutoa elimu kwa madereva wa bodaboda pamoja na wananchi wanaotumia usafiri huo, ili kuweza kujikinga na ajali ambazo zinaweza kusababisha ulemevu wa kudumu au hata vifo,” alisema.

Alisema katika kuhakikisha kikosi hicho kinadhibiti makosa yanayoweza kusababisha madhara, wanaendelea kusambaza askari wanaovaa kiraia wakitumia tochi ili kudhibiti madereva wanaokwenda mwendo kasi na wasiotii sheria za usalama barabarani.

“Mafanikio haya pia yametokana na mkakati wa usimamizi wa sheria na udhibiti wa mwendo kasi, ulevi, kuhakikisha abiria wanavaa mikanda na uvaaji wa kofia ngumu kwa waendesha na wapanda pikipiki,” alisema.

MIKAKATI YA MWISHO WA MWAKA
Akizungumzia kuelekea kipindi cha mwisho wa mwaka huu na mwanzoni mwa mwaka mpya wa 2017, Kamanda Mpinga aliwataka madereva na watumiaji wengine wa vyombo vya moto kuwa makini ili kuepuka ajali zinazoweza kuzuilika

Alisema katika kipindi hiki watu wengi hupenda kusafiri kwenda maeneo mbalimbali na hivyo kuongeza matumizi ya vyombo vya moto barabarani, na huambatana na starehe nyingi ikiwa ni pamoja na ulevi kwa madereva.

“Kutokana na starehe na ulevi, madereva hupoteza umakini na kushindwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na hatimaye kusababisha ajali ambazo hugharimu maisha ya watu wengi na kuacha majeruhi,” alisema.

Alisema kwa kutambua hilo, kikosi cha usalama barabarani kimejipanga kuwatia mbaroni madereva wote watakaokiuka sheria na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.

“Wakati mwingine tutalazimika kuwaweka mahabusu badala ya kulipa faini kama ilivyozoeleka, kitendo ambacho kimekuwa kikiwafanya madereva kuvunja sheria kwa makusudi wakijua kwamba endapo watakamatwa watalipa faini na kuachiwa,” alisema.

MADEREVA WAKOROFI
Kamanda Mpinga alisema kwa sasa wanaendelea na operesheni katika barabara zote kuu nchini kwa kutumia tochi kuwakamata madereva wanaoendesha magari kwa mwendo kasi.

Alisema katika operesheni hiyo wamefanikiwa kuwakamata madereva wa mabasi mbalimbali ya abiria ambao walikuwa wakiendesha kwa kasi ya zaidi ya kilomita 90 kwa saa.

277 WABURUZWA KORTINI
Kamanda Mpinga alisema hadi sasa jumla ya madereva 277 wamefikishwa mahakamani wakitokea mahabusu na kulipa faini kati ya Sh 300,000 hadi 600,000 na wengine kupata kifungo gerezani.

Alisema madereva hao walikamatwa katika mikoa ya Geita, Kagera, Mara, Tabora, Lindi, Iringa, Shinyanga, Arusha Kilimanjaro, Rukwa na Njombe.

“Hatua nyingine ambayo tumekuwa tukiichukua kuwanyima dhamana kwa wale wanaopelekwa mahabusu na leo (jana) hii nimepokea taarifa kutoka Kagera wako madereva wamefungwa kwa siku saba na mkoa huu wamekuwa wakifuatilia sana,” alisema Mpinga.

USALAMA WA WATOTO
“Niwaombe wazazi na wananchi kwa ujumla kuangalia usalama wa watoto wao wanapovuka barabara, katika kumbi za disko na fukwe za bahari. Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani litaongeza nguvu ya kutosha katika kipindi hiki,” alisema.

MATUKIO YA AJALI
Machi 26, mwaka huu watu sita walipoteza maisha na wengine 38 kujeruhiwa vibaya, baada ya basi la Kampuni ya Lupondije Express walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Iringa kupinduka katika eneo la Ipogolo baada ya dereva kushindwa kulimudu.

Julai 4, mwaka huu watu 29 walifariki dunia papo hapo katika ajali iliyohusisha mabasi mawili ya kampuni moja, City Boy, yaliyogongana uso kwa uso saa 9 alasiri, eneo la Kijiji cha Maweni wilayani Manyoni mkoani Singida.

Mabasi hayo, T 531 DCE ambalo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Kahama mkoani Shiyanga na jingine T 247 DCD lililokuwa likitoka Kahama kwenda Dar es Salaam yaligongana yalipokuwa yakipishana.

Desemba 13, mwaka huu, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yussuf Masauni, alilitaka Jeshi la Polisi lidhibiti matukio ya ajali kwa asilimia 10, ikiwamo kufanya ukaguzi wa mabari ya abiria mara kwa mara ili kupambana na madereva wazembe.

Alisema baadhi ya ajali zinazotokea nchini ambazo husababisha hasara na kupoteza maisha ya wananchi wengi, zinachangiwa kwa kiasi kikubwa na uzembe wa watendaji kushindwa kusimamia kazi yao kikamilifu ikiwamo kufanya ukaguzi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: