BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

SIRI NA MBINU ALIZOTUMIA MHE AZIZ ABOOD KUREJEA KATIKA UBUNGE JIMBO LA MOROGORO MJINI ZAFICHUKA

Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini kupitia CCM, Abdullaziz Mohamed Abood akizungumza kwa wananchi katika mkutano wa hadhara wa chama chake juu ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi 2010-2015 katika uwanja wa Shujaa hivi karibuni.PICHA/JUMA MTANDA.

Juma Mtanda, Morogoro.
Mkoa wa Morogoro ni miongoni mwa mikoa iliyobeba historia ndefu katika nyanja mbalimbali ikiwemo siasa iliyoonekana chimbuko la kuibua viongozi mahiri na kuongoza serikali ya Tanzania.

Mmoja wa viongozi hao ni Rais wa kwanza wa Tanzania hayati, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mbunge wa kwanza katika mkoa wa Morogoro.

Nyerere ndiye mbunge wa kwanza wa jimbo la Mashariki katika Baraza Kuu la Kutunga Sheria (LEJICO) baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 1958, wakati huo jimbo la Mashariki Makao Makuu yake yalikuwa Morogoro.

Haikuwa kazi rahisi kwa Nyerere kushinda uchaguzi huo hasa ikizingatiwa kuwa vyama vyote vya upinzani vya wakati huo UTP na CONGRESS mizizi yake ilikuwa katika jimbo la Mashariki ambalo sasa ni Mkoa wa Morogoro.

Kutokana na historia hiyo Morogoro ilikuwa ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kukumbukwa kwani vyama vyote vilivyoipinga TANU vilikuwepo Mkoani Morogoro.

Vyama hivyo vilisaidiwa na kupata nguvu na mabepari na walowezi waliomiliki mashamba makubwa ya mkonge yaliyotapakaa kila kona ya mkoa huo.

Mbunge wa sasa wa jimbo la Morogoro mjini kupitia CCM ni, Abdullaziz Mohamed Abood ambaye alizaliwa Mei 27 mwaka 1959 huku akiwa mmoja wa viongozi katika Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika bunge la Tanzania bara.

Nafasi hiyo ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira ndani ya bunge hilo imetokana na kushinda ubunge katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015.

Lakini moja ya sifa ya Abood kushinda uchaguzi huo imetokana na kutekeleza vyema ilani ya CCM ya mwaka 2010-2015 kwa asiliamia 92 hali iliyopelekea wananchi kumchagua tena katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka 2015.

Uchaguzi huo umemfanya mbunge huyo kupata kura 99,748 na kuweka rekodi ya kuwa mbunge wa CCM aliyechaguliwa kwa kuvuna kura nyingi zaidi katika uchaguzi mkuu 2015/2020.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala haya, Abdullaziz Mohamed Abood (57) alieleza kuwa moja ya siri kubwa iliyomrejesha katika ubunge awali ya pili ni kutekeleza ahadi za ilani ya CCM ya 2010/2015 na kutatua kero ama changamoto kwa vitendo.

Abood alianza kusoma darasa la kwanza mwaka 1965 katika shule ya msingi Bungo Manispaa ya Morogoro na mwaka 1972 alihitimu darasa la saba na kujiunga na kidato cha kuanza shule ya secondari ya Forest Hill mwaka 1973 ambapo alimaliza kidato cha nne mwaka 1976.

Pia ni Mkurugenzi mtendaji wa Abood Group tangu mwaka 1984 hadi 2015.

Abood anaeleza kuwa baada ya kuapishwa bungeni mjini Dodoma yeye alianza kazi ya kusimamia vyema ilani ya CCM ya 2010/2015 huku akitatua kero za wananchi kwa haraka huku nyingine wakisaidiana na halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.

Jimbo la Morogoro Mjini lina eneo la ukubwa wa kilometa za mraba 531.39, kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya mwaka 2012 jimbo hilo lina jumla ya wakazi 515,866 kati yao wanawake 164,166 na wanaume 151,700 likikabiliwa na changamoto za kila aina.

“Jimbo la Morogoro mjini lina mitaa 274, kata 29 na tarafa pamoja lakini kuna changamoto nyingi na baadhi ya changamoto hizo nimeweka utaratibu nzuri wa kuzisikiliza kero na kupokea kutoka kwa wananchi kwa siku za jumanne na alhamisi na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na nyingi kuzitatua”.alieleza Abood.

Kero hizo au changamoto ni kutoka kwenye sekta ya afya, elimu, barabara, maji, michezo na nyingine.

Abood anaeleza ili kuweza kutambua changamoto ndani ya kata, mitaa amekuwa akifanya ziara na kuzungumza na wanachi na kujua kero zao lakini na kukagua miradi yote kwenye jimbo na kuitolea maelezo pale penye mapungufu ili kujenga uwajibikaji ndani ya Manispaa.

“Nimefanya ziara nyingi na kukumbana na changamoto za kuona miradi mingi kuchelewa katika kata kwa kutokamilika kwa wakati na wakati mwingine nimekuwa nikilazimika kuweka msimamo mkali wa kutaka ikamilike haraka ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo ya kweli kwa muda muafaka”.anaeleza Abood.

Kipindi cha 2010-2015 pekee niliweza kufuatilia fedha za miradi ya elimu ya msingi kiasi cha zaidi ya Sh172.3 milioni kutoka serikali kuu ambazo zilipatikana hadi kufika Manispaa na kutekeleza miradi mbalimbali.

Fedha hizo zilitumika kwenye matumizi ya ujenzi wa matundu ya vyoo, kujenga madarasa, ujenzi wa jengo ya utawala na kukamilisha ujenzi wa vyumba mbalimbali vya madarasa.

Upande wa shule za sekondari zaidi ya Sh840.1 milioni nazo ziliingia katika utelezaji wa miradi mbalimbali

huku zaidi ya watoto 500 wa shule za msingi na sekondari wakinufaka kwa kuchangiwa ada na michango cha sh40 milioni ambapo fedha hizo zilitokana na ofisi ya mbunge.

Tuna idadi ya jumla ya wanafunzi 150 wa vyuo vikuu vilivyopo katika jimbo hilo ambapo wazazi wao wana uwezo mdogo na tumeweza kuwasaidia na kuwachangia fedha za ada cha sh15.4 milioni.alieleza mbunge huyo.

SEKTA YA BARABARA.

Abood alifanikiwa kufuatilia kiasi cha fedha cha sh913 milioni na kuelekezwa katika miradi ya barabara za manispaa hiyo.

Fedha hizo ziliingia kwenye matengenezo maalumu kwa kiwango cha lami kwa barabara za Kichangani (Km 0.9) kwenda Mtawala, (Km.0.42) Mfungua kinywa (0.4 km) na Seng’ondo (Km0.7 alieleza Abood.

Barabara hizo zilijengwa na kampuni ya C.G.I. Contractors Ltd ya Morogoro kwa mkataba Na. LGA/079/2012/2013/W/02/0 wa ulionza kufanyiwa kazi Februari 12 mwaka 2013 kwa gharama ya shs594.6 milioni.

Alifafanua kwa kueleza kuwa pamoja na kuwa na barabara nyingi zinazopitika katika maeneo hayo, miundombinu yake hairidhishi nyakati za masika kwa barabara za kuingia Mazimbu, Mzinga, Chamwino, Lukobe, Soko Kuu, Mji mpya, Mafisa na Kichangani.

Ofisi ya Mbunge kipindi hicho ilitoa hundi ya Sh17 milioni na kutumika katika matengenezo ya barabara ya mitaa ya Walimu kata ya Kilakala,Tungi, Kihonda Kaskazini, Youth Mission, Kiegea, Nguvu Kazi na Mafisa ikiwa ni kuweka makaravati na kujenga vivuko vya Chalumbi, Nhugutu na Visore kata ya Boma.

Tumesaidia kukarabati miundombinu korofi kwa kutoa vifaa na vitendea kazi kama majembe 50, Koleo 150, sululu 30 na makaravati150 kwa barabara za kata ya Mlimani, Luhungo, Mlimani ikiwa na lengo la kuwapunguzia kero wananchi.

SEKTA YA MAJI.

Katika utekeleza wa sekta ya maji, Abood anaeleza kutokana na tatizo sugu la maji ndani ya Manispaa, jumla ya sh304 milioni zilipatikana baada ya ufuatiliaji kutoka serikal kuu hadi halmashauri na kuendeleza miradi ya maji ambayo ilitekelezwa.

Ofisi ya mbunge iliweza kugharimia uchimbaji wa visima 13 kwa kata za Mkundi, Kihonda,Tungi, Kilakala, Lukobe, Mindu na Kichangani na kiasi cha sh365 milioni zilitumika, lengo likiwa kupunguza kero ya maji maeneo hayo.

“Matarajio ya ofisi ya mbunge ni kuchimba visima 36 ya maji ndani ya Manispaa hasa kwa kata ambazo miundombinu ya mamlaka ya majisafi na salama (MORUWASA) bado haijafika.anaeleza Katibu wa mbunge huyo, Mourice Massala.

Massala anaeleza kuwa kwa upande wa miradi ya maji eneo la Bigwa, Kingolwira mtaa wa Bomba la Zambia, Lugala na Kasanga jumla ya sh42 milioni zilitumika.

SEKTA YA AFYA.

Katika sekta ya afya, mbunge huyo alifuatilia kwa karibu upatikanaji wa fedha kiasi cha sh1.43 bilioni ambazo ziingia halmashauri zikitoka serikali kuu kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa afya wa jimbo hilo.anaeleza Massala.

“Mbunge amefanya ukarabati wa chumba cha upasuaji hospitali ya mkoa na kutoa vifaa tiba na madawa, vitanda vya kubebea wagonjwa, mashuka, kuchimba kisima na tanki la maji na mambo mengine ambayo yalikuwa ni kero kubwa kwa wagonjwa wa hospitali ya mkoa.”alieleza Massala.

SEKTA YA MAENDELEO YA JAMII.
Massala akifafanua zaidi juhudi za mbunge huyo alieleza kuwa katika Kitengo cha kudhibiti Ukimwi Manispaa ya Morogoro kilipata sh92.9 milioni huku sh1.18 bilioni za usawa wa kijinsia, fedha ambazo zilitoka serikali kuu na kuingia katika idara hizo.

SEKTA YA MIFUKO.

Aliongeza kuwa, baadhi ya wananchi wa jimbo la Morogoro ni wafugaji wa ndani na ili mifugo iweze kupata tiba kwa magonjwa mbalimbali, ofisi ya mbunge ilifuatilia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawa na mambo mengine ya mifugo kiasi cha sh10.4 milioni.

SEKTA YA MICHEZO NDANI YA JIMBO.
Katika kuinua michezo, jimbo hilo lilitumia zaidi ya sh33. Milioni kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya michezo huku baadhi ya timu zilinunuliwa vifaa kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa soka.alieleza Massala.

“Mchezo wa soka unapendwa na vijana wengi na baadhi ya timu zimekuwa hazijiwezi kwa kununua vifaa hivyo lakini ofisi ya mbunge imekuwa ikinunua vifaa na kukabidhiwa timu ili vijana kuendeleza vipaji vyao vya soka”.alieleza Mourice.

UFAFANUZI JUU YA MFUKO WA JIMBO.

Massala alieleza kuwa mfuko wa jimbo hilo umechochea miradi mbalimbali ya wananchi katika sekta ya afya, elimu na nyingine kwa kutoa fedha zaidi ya sh157.3 milioni ambazo zilitumika ununuzi wa vifaa kwa ajili ya zahanati na kuchangia ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

Fedha za mfuko huo zimefanya maendeleo na katika miradi ya ujenzi wa soko la Kilakala ambalo lilipangiwa sh40 milioni na ujenzi wake tayari umekamilika.alieleza Massala.

SIRI YA USHINDI YAFICHULIWA.
Akizungumzia juu ya faida kubwa kwa vikundi vya ujasirimali, Massala anaeleza kuwa jamii hiyo ina mchango mkubwa katika kuinua uchumi kwa maendeleo ya kipato cha mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla wake.

“Mhe Abood amechaguliwa kwa kupigiwa kura katika nafasi ya ubunge lakini siri kubwa ya mafanikio yake ni kuwa karibu na wananchi na kuwasikiliza kero zao tuna amini ukiwezesha vikundi umewezesha familia mzima.”alieleza Massala.

Aboodi aliwasaidia kujikwamua na umasikini vikundi 350 vya ujasiliamali kwa kuwachangia jumla ya sh350 milioni.anaeleza Massala

Fedha hizo ziliweza kununua vyerehani 30, baiskeli 20, pikipiki 15 (BodaBoda), viti vya kukalia 5,000 kwa ajili ya kukodisha kwenye sherehe viligharimu kiasi cha sh7.5 milioni na maturubai 20 yenye thamani ya sh2 milioni na kupewa vikundi mbalimbali vya wajasiliamali kulingana ma mahitaji yao.

Massala alieleza kuwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro iliweza kuchangiwa Printer mpya ya kisasa yenye thamani ya sh500,000 inayotumika kutolea picha za Utra-Sound na kumwezesha daktari kusoma tatizo la ugonjwa kwa urahisi zaidi.”alieleza Massala.

Mkazi wa Mafisa kwa Mambi, Saida Ludege alieleza kuwa sifa za uchapakazi kwa wananchi ni yule mbunge anayeweza kutatua shida mbalimbali.

"Kama Abood angewauliza wakazi wa kata ya Mafisa kuna changamoto gani au kero gani basi waliowengi wangeeleza tatizo la mto Morogoro kujaa mchanga na maji kushindwa kupita mtoni na kupasua na kuingia kwenye kaya za watu hilo ni moja la tatizo"alisema Saida.

Saida alieleza kuwa ni kwenye Abood amekuwa akitekeleza ilani ya chama chake lakini anapaswa kuiangalia na kata hiyo hata miundombinu ya barabara haziko vizuri nyakati za masika na kusababisha kero.

SHAMIM KHAN
Shamim Khan aliyewahi kuwa mbunge jimbo la Morogoro na waziri wa fedha kipindi cha nyuma, anaeleza kuwa kazi ya mbunge kwa mujibu wa katiba ni kuwakilisha wananchi, kutunga sheria na kuisimamia serikali.

Shamim anaeleza ukiachilia kazi hizo, mbunge anapaswa kuwa karibu na wananchi wake kwa kushirikiana kwa ukaribu katika kazi za maendeleo bila kujali wananchi hao wanaishi eneo lipi na lina changamoto zipi.

“Abdullaziz Abood ni mbunge anayefuata nyayo zangu kwa kuwa karibu na wananchi na hii inasaidia kujua matatizo na changamoto wanazokumbana nazo wananchi na kutafuta njia za kuzitatua.”alisema Shamim.

Aliongeza kwa kueleza, ili kufahamu changamoto za wananchi ama matatizo yao ni lazima uwatembelee bila kujali kama wanaishi mazingira gani kwani hao ndio waliokuchagua na asante yao kwako ni kutatua changamoto za afya, barabara, maji na nyingine.

Wananchi wanajisikia faraja sana kumuona mbunge akishirikiana nao lakini naye awe tayari kusikiliza kero zao, mfano mimi nilitenga siku tatu kusikiliza shida zao na siku tatu kusikiliza za wanaCCM na nilipokea taarifa zao na kutekeleza ama kuzisukuma mbele.alieleza Shamim.

Abdullaziz Abood alianza harakati za kuwania ubunge katika jimbo hilo mwaka 2000 ambapo aliongoza kura za maoni lakini jina lake halikuweza kupitishwa na vikao vya halmashauri kuu ya CCM Dodoma ambapo lilipitishwa jina Mhandisi, Oscar Mroka aliyeshinda kiti hicho mwaka 2000-2005.

Mwaka 2005 alijitosa tena katika kinyang’anyiro hicho na kuongoza kura za maoni lakini hali hiyo ilijirudia tena na jina la Dk Omari Nibuka Mzeru ndilo lilichaguliwa kupeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu mwaka 2005 ambapo alishinda ubunge mwaka 2005-2010.

Abood hakuweza kukata tamaa ambapo mwaka 2010 alijitosa tena na kufanikiwa kuongoza tena kura za maoni na jina lake kufanikiwa kuteuliwa kugombea ubunge kupitia CCM safari hiyo akimbwaga mpinzani wake wa karibu, Profesa Romanus Ishengoma na Dk Mzeru alishika nafasi ya tatu kwenye kura hizo.

Abood ni mjumbe wa halmashauri kuu ya CCM (NEC) nafasi aliyoipata mwaka 2007 kwa kumbwaga, Dk Juma Ngasongwa aliyekuwa anashikilia nafasi hiyo kwa mkoa wa Morogoro huku akiendelea nayo hadi sasa kwa ngazi ya wilaya ya Morogoro mjini tangu mwaka 2012.

Wabunge waliowahi kuongoza jimbo la Morogoro mjini ni pamoja na Mwl Julius Nyerere 1961-1962, Oscar Kambona, Zuberi Mtemvu, Amir Jamal mwaka aliyemaliza ubunge wake mwaka 1985 na kuingia Shamim Khan 1985-1995, Luteni kanali mstaafu, Ahmed Mazora mwaka 1995-2000.

Wenginge ni Mhandisi Oscor Thomas Mloka mwaka 2000-2005, Dk Omari Nibuka Mzeru mwaka 2005-2010 huku Abdullaziz Mohamed Abood akipokea kijiti hicho kuanzia mwaka 2010 hadi sasa.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: