BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WIKI YA KUUMBUKA MAFISADI BUNGENI IMEIVA DODOMA


CAG, Prof. Mussa Assad.
 
NI wiki ya mafisadi kuumbuka! Ndivyo unavyoweza kuziita siku saba za juma hili kwa kuwa zitakuwa mahsusi kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuanika bungeni watumishi wanaotafuna fedha za umma.

Hatua hiyo inakuja baada ya Rais John Magufuli kukabidhiwa Ripoti ya CAG ya mwaka 2015/16, na juma hili itakabidhiwa bungeni mjini hapa ili serikali itoe majibu ya hoja mbalimbali za ukaguzi wa Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi ambayo CAG ni mkuu wake.

Machi 27, Rais Magufuli alipokea Ripoti ya CAG, Prof. Mussa Assad, Ikulu jijini Dar es Salaam, ikigusa maeneo mengi ukiwamo ukusanyaji wa kodi kutoka vyanzo mbalimbali na misamaha ya kodi, uandaaji na utekelezaji wa bajeti ya serikali, hali ya Deni la Taifa, usimamizi wa rasilimali watu, usimamizi wa mali na madeni ya serikali, na usimamizi na uendeshaji wa taasisi za umma zikiwamo taasisi muhimu za kifedha na Shirika la Umeme (Tanesco).

Alipotafutwa na Nipashe kwa simu jana asubuhi, Prof. Assad aliweka wazi kuwa ripoti yake kwa mwaka wa fedha 2015/16 ataiwasilisha bungeni wiki hii.

Nipashe ilitaka kujua ni lini CAG na wataalamu wake wataingia bungeni kuwasilisha ripoti yao ya ukaguzi kwa mwaka wa fedha 2015/16 baada ya kubaini kuwa ratiba ya vikao vya Bunge la Bajeti iliyotolewa na Ofisi ya Katibu wa Bunge haijaeleza chochote kuhusu uwasilishwaji wa ripoti hiyo nyeti.

Taratibu na sheria iliyoanzisha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi inamtaka CAG kuwasilisha ripoti yake ya ukaguzi ndani ya siku saba za mwanzo za Bunge la Bajeti (pasi na kuzihusisha siku za mwishoni mwa wiki na sikukuu).

Katika majibu yake, CAG Prof. Assad alisema: "Nitakwenda bungeni Alhamisi. Tarehe 13 Aprili (Alhamisi) ndiyo tumeipanga kuwa siku yetu ya 'ku-table' (kuwasilisha) ripoti."

"Bado hatujachelewa maana bado tumo ndani ya muda wa siku saba kisheria maana unatakiwa uondoe siku za Jumamosi na Jumapili na siku za sikukuu. Alhamisi tutakuwa bungeni mjini Dodoma."

Bunge la Bajeti lililoanza Jumanne leo linaingia katika kikao (siku) chake cha nne. Ijumaa hapakuwa na kikao kutokana na sikukuu ya Kumbukumbu ya Kifo cha Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume.

Baada ya kuiwasilisha, CAG atakabidhi ripoti yake kwa kamati mbili za Bunge zenye mamlaka ya kuifanyia uchambuzi ambazo ni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

KAZI NA SERIKALI
Akiwa safarini jana kuja mjini hapa akitokea jimboni kwake Sumbawanga Mjini, Makamu Mwenyekiti wa PAC, Aeshi Hilaly, aliiambia Nipashe kuwa kamati yake inaisubiri ripoti ya CAG kuona kama mapendekezo ambayo iliyatoa mwaka jana yamefanyiwa kazi na serikali.

"Tutaipitia ripoti yote. Pale patakapoonekana pana upungufu, tutaufanyia kazi. Yapo mambo ambayo tuliagiza yafanyiwe kazi baada ya kuona kuna upungufu, tunatarajia kwamba ripoti inayokuja hautakuwapo," Aeshi alisema.

"Kama yatakuwapo, basi tutahoji kwanini yamejirudia tena kwa sababu tuliyaipitia katika ripoti ya mwaka jana, tukaona upungufu na tukaelekeza cha kufanya na mengine tukapata majibu."

Mwenyekiti wa LAAC, Vedasto Ngombale, alisema ripoti ya CAG itawapa mwongozo kujua utekelezaji wa miradi ya maendeleo huku akiweka wazi kwamba CAG amekuwa na wakati mgumu kutekeleza majukumu yake mwaka huu kutokana na ufinyu wa bajeti.

"Utendaji wa CAG 'this time' (wakati huu) unaonekana uko chini kwa sabahu bajeti yake ilifyekwa. Hata mimi ambaye nafanyia ukaguzi serikali za mitaa, nimefanya kwa kuangalia taarifa za maandishi zaidi badala ya kwenda kuangalia miradi," alisema.

"Safari hii tumekwenda kuona hali halisi katika miradi chini ya 20 na yote ilikuwa na dosari ambazo zinaonekana CAG mwenyewe hakupata nafasi ya kwenda kukagua miradi.

"CAG amecheleweshewa kupatiwa fedha, hali inayoathiri utendaji wake. Kama kweli serikali inataka kudhibiti matumizi mabaya ya fedha, basi inapaswa kumtumia sana CAG maana yeye ndiye jicho la serikali. Sasa kama yeye anakosa mawanda ya kufanya kazi, kazi inakuwa ngumu sana.

"Hata sisi kamati mara hii tumepata shida maana huko mwanzoni CAG alikuwa anatuwezesha kwa fedha za semina za namna ya kukagua vizuri miradi ya maendeleo, lakini kwa sababu ya ufinyu wa bajeti yake, hatujapata semina hata moja mwaka huu," alisema Ngombale na kuongeza kuwa miradi waliyoikagua ni pamoja na ya maji na ujenzi wa barabara, madarasa na maabara.

MCHWA WA BAJETI
Miongoni mwa hoja zinazotarajiwa kuwa gumzo katika ripoti ya CAG ni madai ya uwapo wa ufisadi katika miradi inayosimamiwa na taasisi na mashirika ya umma na 'mchwa' wa fedha za maendeleo katika halmashauri mbalimbali hasa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Dodoma, Singida, Kilimanjaro na Pwani.

Hoja nyingine ni kukua kwa kasi kwa Deni la Taifa, uwapo wa watumishi hewa na mradi wa mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam ambao Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inapaswa kueleza faida zake na sababu za kujenga kituo cha mabasi hayo eneo la Jangwani jijini ambalo ni njia kuu ya maji na pia ni mkondo wa upumuaji wa bahari.

DENI LA TAIFA
Wakati akiwasilisha bungeni hotuba yake kuhusu bajeti ya serikali, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, Deni la Taifa lilifikia Dola za Marekani bilioni 20.7 (Sh. trilioni 46.66) likijumuisha deni la ndani na la nje pamoja na mifuko ya hifadhi ya jamii kutokana na riba na adhabu mbalimbali zinazosababishwa na kuchelewa kulipa.

Ripoti ya CAG inatarajiwa kuanika jinsi deni hilo linavyopaa na ushauri wake kwa serikali. Katika Bunge la Bajeti mwaka jana, upinzani uliiomba Ofisi ya CAG kufanya ukaguzi maalumu wa Deni la Taifa baada ya kuwa umebaini kuwa deni hilo limekua maradufu kutoka 2010 hadi 2015.

Kwa mujibu wa David Silinde, Naibu Waziri Kivuli wa Fedha na Mipango, mwishoni mwa Juni 2010, jumla ya Deni la Taifa lilikuwa Dola 9.9 (Sh. trilioni 13.6 kulingana na thamani ya kipindi hicho), lakini miaka mitano baadaye, yaani 2015, lilifikia Sh. trilioni 41.5.

MAGUFULI KUAMUA
Hivi karibuni kuliibuka madai ya kuwapo kwa ufisadi katika taasisi na mashirika ya umma kiasi cha Rais Magufuli kuamua kuzichukua fedha zake na kuzihifadhi Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Macho na masikio ya wengi yanatarajiwa kuelekezwa kwenye Ripoti ya CAG Alhamisi kujua jinsi 'vigogo' wa mashirika na taasisi hizo walivyofuja fedha za umma.

Tuhuma za kukosekana kwa uadilifu katika matumizi ya fedha za maendeleo zimezikumba halmashauri nyingi huku baadhi ya watendaji wake wakitumbuliwa.

Mchwa wa fedha za maendeleo wamekuwa wakibainika katika ripoti zilizopita za CAG, hivyo macho na masikio ya wengi yanatarajiwa kuelekezwa kwenye changamoto hiyo katika Ripoti ya CAG.

Baadhi ya miradi inayohusisha mashirika na taasisi hizo ni mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi katika halmashauri za Singida, Arusha na Kilimanjaro ambazo PAC ilibaini zimejengwa chini ya kiwango, baadhi ya barabara zimejengwa chini ya kiwango na Wakala wa Barabara (Tanroads) na uchunguzi wa CAG kuhusu fedha zilizowekwa na Mamlaka ya Bandari (TPA) katika benki mbalimbali kwa utaratibu wa akaunti maalum (fixed account) kutokana na kiasi kidogo cha riba kilicholipwa.

Miradi mingine ni pamoja na wa maji Chalinze mkoani Pwani uliobainika kuwa na ongezeko la bilioni 30 kwenye gharama zake, ukarabati wa ofisi ya Makamu wa Rais jijini Dar es Salaam uliobainika kuwa chini ya kiwango, mradi wa Dege Eco na maagizo ya LAAC kwamba CAG afanye ukaguzi maalum kwenye miradi ya maji inayotekelezwa na Manispaa ya Dodoma mwaka 2012/13 na 2014/15.

WATUMISHI HEWA
Machi 12, mwaka jana, serikali ilianza msako wa watumishi hewa na uhakiki wa vyeti vya watumishi wote wa umma, uhakiki ambao ulikamilika rasmi Machi 31, mwaka huu.


Rais Magufuli ameshaagiza watumishi hewa wanaolipwa mabilioni ya shilingi wasakwe. Ripoti ya CAG ya mwaka 2014/15 ilibainisha kuwapo kwa kadhia hiyo na wiki hii Prof. Assag anatarajiwa kuanika kiasi cha fedha ambacho Tanzania imepoteza kutokana na watumishi hewa katika mwaka wa fedha 2015/16.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: