Kikosi cha kwanza cha Yanga kilichoumana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa na kushinda mabao 4-1
Kikosi cha kwanza cha JKT Ruvu kilichoumana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa na kushinda mabao 4-1.
MABINGWA wa soka Afrika Mashariki na Kati, Yanga, leo
wamevuna ushindi wa kwanza tangu kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
baada ya kuwafunga Maafande wa JKT Ruvu ya Pwani, mabao 4-1 katika mechi
iliyochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar
es Salaam.
Wakati ushindi huo ukipeleka faraja kwa mashabiki wa Yanga,
kwa upande wa JKT Ruvu ni mwendelezo wa maumivu kwani ni kipigo cha pili
mfululizo, ambapo katika mechi iliyopita, walifungwa mabao 2-0 na Simba
uwanjani hapo.
Katika mechi hiyo ambayo Yanga ilishuka dimbani bila Kocha
Mkuu wake Tom Saintfiet, aliyetimuliwa tangu juzi, wakali hao wa Jangwani
walionesha uhai tangu kuanza kwa mechi hiyo.
Yanga wakionesha kiu ya kuondoka na ushindi, ndani ya dakika
tatu za kwanza, walifika mara mbili langoni mwa JKT Ruvu kabla ya beki wake,
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kuifungia bao la uongozi dakika ya tano, akiunga pasi
ndefu ya Athumani Idd Chuji aliyepokea mpira mfupi ya adhabu ndogo ya Harouna
Niyonzima.
Baada ya bao hilo,
Yanga ikazidi kutawala mchezo na kushambulia mara kwa mara, na kupoteza nafasi
kadhaa kupitia wakali wake Simon Msuva na Didier Kavumbagu, waliokuwa mwiba kwa
walinzi wa JKT, lakini pia ikikosa kupitia Nizar Khalfan na Hamis Kiiza.
Dakika ya 31, Kavumbagu akaipatia Yanga bao la pili, akiitendea
haki pasi ya Oscar Joshua.
Mwamuzi wa mchezo huo Hashimu Abdallah, akamlima kadi ya
njano kiungo Ally Khan wa JKT, ambaye alikuwa akijaribu kupunguza kasi ya idara
ya kiungo ya Yanga kwa kucheza rafu za mara kwa mara kwa Haruna Niyonzima.
Kavumbagu aliyeonesha uhatari zaidi mbele ya lango
kulinganisha na mechi zilizotangulia, aliwachambua mabeki wa JKT Ruvu na kutoa
pasi nyoofu kwa Nizar, ambaye alikosa bao kunako dakika ya 35.
Licha ya Yanga kutawala mchezo huo, JKT Ruvu haikuwa nyanya
kivile, kwani nayo mara kadhaa ilishambulia na kupoteza nafasi zake, ikiwamo ya
Haruna Adolf aliyefumua shuti kali dakika ya 39 na kumbabatiza Kevin Yondani na
kuwa koa tasa.
JKT wakarudi tena langoni mwa Yanga dakika ya 43, ambapo
shambulizi lao kali likamalizwa na rafu ya Athumani Idd Chuji kwa Adolf na
Stanley Mkomolwa aalipiga adhabu ndogo na kukosa. Hadi mapumziko Yanga ikawa
mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi Yanga ikacharuka zaidi na kufunga mara mbili kupitia
kwa Simon Msuva dakika ya 53 na baadaye Kavumbagu tena kunako dakika ya 65.
JKT ikaendelea kupambana, ambapo mtokea benchi Credo
Mwaipopo aliyeingia kuchukua nafasi ya Said
Otega, aliifungia bao pekee la kufutia machozi katika dakika ya 65.
Hadi filimbi ya mwisho Yanga ikaibuka na ushindi huo wa
mabao 4-1 na kuzika rasmi jinamizi la kufanya vibaya, lililozinduliwa kwa sare
ya 0-0 dhidi ya Tanzania Prisons, kisha kichapo cha mbwa mwizi juzi cha mabao
3-0, ilipowafuata Wakata Miwa wa Manungu, kwenye Uwanja wa Jamhuri, mjini
Morogoro.
Huko Chamazi Complex nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam,
wenyeji wa uwanja huo, Azam FC, waliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi
ya Mtibwa Sugar, lililowekwa nyavuni mapema kipindi cha kwanza na nyota wa
kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche, huku Wakata Miwa hao wakimaliza
pungufu.
KWA HISANI YA BLOG:francisdande.blogspot.com

0 comments:
Post a Comment