LICHA ya waasi wa M23 kutangaza kujiondoa kwenye mji wa Goma, Umoja wa
Mataifa unasema waasi hao hawajaonesha dalili ya kuondoka kabisa na
umetoa wito kwa mataifa ya kigeni kutojihusisha na mgogoro kwenye eneo
hilo.
Umoja wa Mataifa unatarajiwa kuwawekea vikwazo baadhi ya viongozi wa
kundi la waasi wa M23 na vile vile watu wanaowaunga mkono kutoka nje.
Kwenye azimio lililopitishwa kwa kauli moja na Baraza la Usalama, Umoja
huo umewataka waasi wa M23 kuweka silaha zao chini na kuacha mapigano
mara moja na pia kuwaachilia watoto wanaohudumu kwenye kundi lao kama
wapiganaji.
Likionesha wasiwasi wake kufuatia taarifa za mauaji, ubakaji na
kuajiriwa watoto kwenye kundi la M23, Baraza la Usalama limeelezea nia
ya ya kuwawekea vikwazo viongozi wa kundi hilo na watu wanaoaminika
kuliunga mkono.
Miongoni mwa vikwazo hivyo ni kupiga marufuku ya uuzwaji
wa silaha kwa makundi ya waasi wa Kongo.
Serikali ya Kongo ndiyo yenye jukumu la kulinda watu wake
Marais Yoweri Museveni wa Uganda (kushoto), Joseph Kabila wa DRC
(katikati) na Paul Kagame wa Rwanda katika mkutano wa viongozi wa Maziwa
Makuu juu ya mzozo wa Kivu ya Kaskazini, Novemba 2012.
Vile vile Umoja wa Mataifa umeitaka serikali ya Rais Joseph Kabila
kuendesha uchunguzi na kuwaadhibu waliohusika na uhalifu huo, kwani
"usalama na amani ya Kongo ni jukumu la kwanza la serikali hiyo."
Msimamo huo unafuatia lawama dhidi ya Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja
wa Mataifa nchini Kongo (MONUSCO) ambacho hakikuzuwia kutekwa kwa mji
wa Goma na waasi wa M23 wiki mbili iliopita.
Baraza hilo limeyatahadharisha makundi yote ya wapiganaji katika
mashambulizi yao dhidi ya walinda amani wa MONUSCO na raia wa kawaida.
Baadaye, Baraza la Usalama lilipitisha azimio linaloidhinisha ripoti ya
wataalamu kuhusu Kongo.
Mataifa ya kigeni yalaumiwa
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekanbi, Hillary Rodham Clinton.
Akizungumza na DW mjini New York, Naibu Balozi wa Rwanda kwenye
Umoja wa Mataifa, Olivier Nduhungirehe, alisema nchi yake inakubaliana
na hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa, lakini aliendelea kukanusha kuhusika
kwa nchi yake na mzozo wa Kongo.
"Rwanda siyo chanzo cha mzozo wa Kongo na haijihusishi hata kidogo.
Tumeshangazwa sana na msimamo wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
kuunga mkono ripoti ya kundi la wataalamu inayoelezea kwamba Rwanda
inawaunga mkono waasi wa M23, bila ya Baraza hili kuhoji mfumo wa
uchunguzi, ushahidi na tuhuma za wataalamu hao dhidi ya Rwanda." Alisema
Balozi Nduhungirehe.
Balozi wa Jamhuri ya Kodemokrasia ya Kongo nchini Ufaransa, Ileka Atoki,
alielezea msimamo wa nchi yake kwamba inataka viongozi wa Rwanda
waliotajwa kwenye ripoti hiyo wawekewe vikwazo.
"Ushahidi wa watu na vifaa umetambuliwa na Umoja wa Mataifa kuthibitisha
kuvamiwa kwa Kongo na nchi ya Rwanda.
Mbali na hayo, Rwanda inaendelea
kukiuka marufuku ya Umoja wa Mataifa ya kutowapa silaha wapiganaji na
kusababisha hali mbaya ya kiutu kwenye mkoa wa Kivu ya kaskazini.
Kutokana na mauwaji hayo, serikali ya Kongo na jumla ya raia wake wote
wanasubiri kuona hatua kali zikichukuliwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya
wahusika wa machafuko hayo."
Baada ya azimio hilo la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kiongozi
wa Kamati ya Vikwazo vya Umoja huo anatarajiwa kuwasilisha orodha ya
majina ya watu watakaowekewa vikwazo mwishoni mwa wiki hii.
Duru za kuaminika za Umoja wa Mataifa zimeimbia DW kwamba Umoja huo
utafuatilia kwa karibu kutekelezwa kwa matokeo ya Mkutano wa Marais wa
Nchi za Maziwa Makuu kuhusu usitishwaji mapigano na kuondoka kwa waasi
kwenye mji wa Goma.
Mataifa ya Magharibi yaendelea na diplomasia
Waasi wa M23 wakipiga doria kwenye mji wa Goma.
Hatua hii inakuja katika wakati ambapo Marekani, Uingereza na
Ufaransa zinaendesha juhudi maalumu za kidiplomasia katika mataifa ya
Kongo, Rwanda na Uganda ili papatikane suluhisho la mzozo wa hivi sasa
kwenye mkoa wa Kivu ya Kaskazini.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amewatolea wito
viongozi wote wa eneo la Maziwa Makuu kusitisha kuwasaidia waasi wa M23.
Akigusia ukweli kwamba kiasi cha watu 285,000 wameshayakimbia makaazi
yao tangu waasi hao waanze kuelekea mjini Goma mwezi Aprili, Clinton
amesema wengi wa watu hao wanahitaji msaada wa dharura na akawataka
waasi kuacha mashambulizi na kujiondoa moja kwa moja mjini Goma.
"Tunawatolea wito viongozi na serikali zao katika eneo zima kusita na
kuzuia msaada wowote kwa M23 kutoka ndani ya mipaka za nchi zao."
Alisema Clinton katika kile kinachotajwa kuwa ni kauli nzito zaidi
kuitoa tangu mzozo huu kulikumba eneo la Maziwa Makuu.
0 comments:
Post a Comment