WAZIRI WA FEDHA, Dk WILLIAN MGIMWA.
JUMUIYA ya Ulaya (EU), imeongeza masharti kwa Serikali ya Tanzania ili iweze kupatiwa msaada wa Bajeti kwa mwaka ujao wa fedha 2013/14.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo gazeti hili MWANANCHI imezipata, masharti mapya yaliyotolewa na jumuiya hiyo ni pamoja na kuitaka Serikali ya Tanzania kusimamia kikamilifu masuala ya haki za binadamu, utawala wa sheria, kuwapo mfumo madhubuti wa uwajibikaji katika usimamizi wa Bajeti na ushirikishwaji wa taasisi huru.
Balozi wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya nchini, Filiberto Ceriani Sebregondi alibainisha hayo jana katika mawasiliano na gazeti hili kwa njia ya mtandao kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba Wahisani Wakuu wa Bajeti ya Serikali (GBS), wamechelewa kuwasilisha fedha hizo katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha nchini.
Balozi Sebregondi alitaja maeneo mengine yaliyosisitizwa na EU kuwa ni pamoja usimamizi sahihi wa rasilimali za taifa na kuongeza uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali.
Balozi Sebregondi alitaja maeneo mengine yaliyosisitizwa na EU kuwa ni pamoja usimamizi sahihi wa rasilimali za taifa na kuongeza uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali.
Alisema kuwa kikao cha mwaka cha mapitio ya uchangiaji wa Bajeti ya Serikali kilichofanyika wiki iliyopita kilichowahusisha wachangiaji wakubwa wa GBS, ikiwamo EU na Serikali ya Tanzania kiliweka wazi juu ya kuwapo kwa uboreshaji wa mfumo wa utoaji msaada na kuridhiwa na pande zote.
Balozi huyo alisema, “EU kupitia chombo cha kutoa msaada wa kibajeti, mara kadhaa imekuwa ikifanya majadiliano na Serikali ya Tanzania juu ya kuongeza juhudi katika kuleta mabadiliko yakinifu kwenye maeneo ya uwajibikaji na vita dhidi ya rushwa.
“Wiki iliyopita wachangiaji wa GBS ikiwamo EU, walikutana na Serikali ya Tanzania kufanya tathmini ya mwaka wa fedha uliopita na kufikia makubaliano juu ya mabadiliko ya mfumo wa utoaji misaada kwa nchi zote zinazofadhiliwa.
Alipoulizwa kuhusiana na masharti hayo jana, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa alikiri kufanyika kwa mazungumzo baina ya Serikali na wahisani na kwamba waliyapokea na wapo tayari kuyatekeleza.
Waziri Mgimwa alisema, “Masharti hayo hayana athari yoyote kwa Bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha ujao wa 2013/14.”
Alisema kuwa hadi sasa Serikali inaendelea vyema na utekelezaji wa masharti hayo akiongeza kwamba walishawasilisha taarifa zote kuhusu maendeleo hayo.
Hivi karibuni Kamisheni ya Umoja wa Ulaya (EUC) na Kamati ya Kudumu ya Wawakilishi wa Umoja huo walikutana jijini Brussels, Ubelgiji kujadili Bajeti ya mwaka 2013 ya umoja huo, ambapo walitangaza masharti mapya ya utoaji misaada kwa nchi zinazoendelea.
Pamoja na mambo mengine, masharti hayo yanahitaji uboreshwaji wa haki za binadamu, utawala wa sheria, uwajibikaji katika matumizi na kudhibiti rushwa.
Akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013 bungeni mjini Dodoma Juni mwaka huu, Dk Mgimwa alisema kuwa katika mwaka huo wa fedha jumla ya Sh15 trilioni zinatarajiwa kutumika.
0 comments:
Post a Comment