MAREKANI imekosoa uamuzi wa Israel kujenga nyumba 3,000 za walowezi
mashariki mwa Jerusalem na katika ukingo wa magharibi, ambapo waziri
Hillary Clinton amesema hatua hiyo kuwa inarudidha nyuma jitihada za
amani.
Mapema, Ikulu ya Marekani iliita hatua hiyo ambayo imekuja siku moja
baada ya Umoja wa Mataifa kupiga kura ya kihistoria na kuipandisha
Palestina hadhi ya nchi muangalizi siku ya Alhamisi kwa kuzingatia
mipaka ya mwaka 1967, kama isiyo na manufaa yoyote.
"Kwa kuzingatia
tangazo lililotoka jana naomba nirejee kwamba utawala huu, kama
tawala zilizotangulia, umeweka bayana kwa Israel kuwa shughuli hizo
zinarudisha nyuma jitihada za majadiliano ya amani," alisema Clinton.
Clinton akishuhudia rais Mahmoud Abbas na Waziri Mkuu Netanyahau wakipeana mikono.
Clinton aliyasema hayo wakati akizungumza katika jukwaa lilioandaliwa na
kituo cha sera za mashriki ya kati cha Saba mjini Washington, mbele ya
hadhira iliyowajumuisha mawaziri wa mambo ya kigeni wa Israel Avigdor
Lieberman na wa Ulinzi Ehud Barak.
Clinton alisema kuwa suluhisho la
kudumu la mgogoro wa Gaza lingekuwa mpango mpana wa amani kati ya Israel
na Wapalestina wote, wakiongozwa na wawakilishi wao halali, mamlaka ya
Palestina.
Aelezea sababu za kuipinga Palestina Umoja wa Mataifa
Utawala wa rais Barack Obama ulijaribu kuzuia shinikizo la Palestina la
kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, ukisema kuwa hatua hiyo ingekuwa
kizingiti katika njia ya amani na kwamba taifa la Palestina lingetokana
tu na mazungumzo na Israel.
"Wote tunapaswa kuweka kituo baada ya kura
ya wiki hii. Pande zote zinapaswa kutafakari kwa kina njia iliyoko mbele
yetu,"
Clinton alisema. Aliongeza kuwa pande zote zinapaswa kufanya
kazi kwa pamoja ili kutafuta njia ya kusonga mbele katika mazungumzo
ambayo ndiyo yataleta suluhisho la mataifa mawili, ambayo inabaki kuwa
shabaha yao.
Makaazi ya walowezi wa kiyahudi katika eneo linalokaliwa na Israel la Hebron.
Alisema pande mbili zitakapokuwa tayari kushiriki tena mazungumzo, rais
Obama atakuwa tayari kushirikiana nao kikamilifu.
Mapema, msemaji wa
bazara la taifa la usalama, Tommy Vietor alisema kuwa Marekani inarejea
upinzani wake wa muda mrefu dhidi ya makaazi ya walowezi, ujenzi
mashariki mwa Jerusalem na matangazo ya Israel.
"Tunaamini vitendo hivi
havileti manufaa yoyote zaidi ya kuhujumu jitihada za kurudi kwenye meza
ya mazungumzo;" alisema Vietor.
PLO yalaani tangazo la Israel
Taarifa za vyombo vya habari zimesema baadhi ya ujenzi wa Israel
utafanyika katika eneo linalogombaniwa katika ukingo wa magharibi
maarufu kama E1, ambalo linapita kati ya upande wa mwisho wa mashariki
ya eneo lililotekwa la Jerusalem mashariki, na makaazi ya Maaleh Adumim.
Chama cha Ukombozi wa Palestina, PLO, kimelaani hatua hiyo na kusema ni
uvamizi dhidi ya taifa hilo.
Wapalestina wanapinga kwa nguvu zote,
mradi wa E1 kwa sababu unaligawanya eneo la ukingo wa magharibi katika
vipande viwili - kaskazini na kusini, hatua ambayo inafanya uundwaji wa
taifa la Palestina kuwa mgumu.
Picha inayoonyesha kizuizi kinachotofautisha mji wa Palestina wa Qalqilya na makaazi ya walowezi.
Wapalestina wanaitaka Jerusalem kuwa mji mkuu wa taifa lao na wanapinga
mipango ya upanuzi wa Maaleh Adumim, eneo lililoko kilomita 5 kutoka
ukingo wa mashariki wa mji wa Jerusalem.
Kitendo cha Marekani kulaani
ujenzi wa makaazi ya walowezi na Israel huko nyuma kimekuwa
kikisababisha malumbano kati ya Obama na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.
Viongozi hao wawili wana uhusiano wa mashaka hivi sasa, licha ya hoja
za utawala wa rais Obama kuwa serikali hiyo imefanya kazi ya ziada
kuhakikisha inalinda usalama wa Israel kuliko utawala uliyopita.
0 comments:
Post a Comment