Kikosi cha Kilimanjaro Stars
kilichopambana na timu ay Somalia katika mchezo wa michuano ya Tusker Cecafa
Challenge Cup uliofanyika katika Uwanja wa Lugogo nchini Uganda leo na kushinda
kwa goli 7-0. Magoli ya Kilimanjarto Star yakipachikwa na Mrisho Ngasa (5) na
John Boko (2).
Mrisho Ngassa akishangilia moja ya goli kati ya
matano aliyofunga wakati wa mchezo na Somalia uliochezwa katika Uwanja wa
Lugogo nchini Uganda.
Boko akishangilia moja ya goli wakati wa
mchezo na Somailia
Mashabiki wa timu ya Kilimanjaro Stars waishio
nchini uganda wakiishangilia timu yao wakati mchezo dhidi ya timu ya
Somalia.
TIMU ya Soka ya TANZANIA Bara,
Kilimanjaro Stars imefuzu kuingia Robo Fainali ya michuano ya Tusker CECAFA Challenge, baada ya kuilaza Somalia
mabao 7-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Lugogo mjini hapa.
Matokeo hayo yanaifanya Bara
itimize pointi sita baada ya kucheza mechi tatu huku wakishinda mbili na
kufungwa moja tu.
Stars, inayodhaminiwa na
Kilimanjaro Premium Lager leo ilionyesha kandanda safi na kusisimua mashabiki
wa Tanzania waliokuja kuiunga mkono hapa, akiwemo Mbunge wa Kondoa Kaskazini,
Alhaj Juma Nkamia.
Iliwachukua sekunde 48 tu
Stars kupata bao la kwanza, kupitia kwa mshambuliaji wa Simba SC,
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premum Lager pia, Mrisho Khlfan Ngassa
aliyewazidi ujanja mabeki wa Somalia.
Kabla hawajakaa vizuri,
Somalia walipachikwa bao la pili, dakika ya 23 lililofungwa na Ngassa tena,
aliyeunganisha kona nzuri ya Issa Rashid.
John Bocco ‘Adebayor’ alifunga
bao la tatu katika mchezo wa leo na la tatu kwake katika mashindano haya dakika
ya 26 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Issa Rashid kutoka wingi ya kushoto.
Bocco tena aliwainua vitini
mashabiki wa Tanzania kwa kufunga bao la nne kwa kichwa, akiunganisha krosi ya
Ngassa dakika ya 41.
Ngassa alifunga bao la tatu
katika mchezo wa leo dakika ya 44 na la tano kwa Stars baada ya kuuwahi mpira
uliotemwa na kipa Hussein Abdallah kufuatia shuti kali la Salum Abubakar ‘Sure
Boy Jr.’
Somalia ilipata pigo dakika ya
30, baada ya kipa wake namba moja, Mohamed Abdullah kuumia baada ya kugongana
na Bocco na kutoka, nafasi yake ikichukuliwa na Hussein Abdallah.
Katika kipindi cha pili Ngassa
aliendeleza mvua yake ya mabao na kufunga mabao mawili zaidi moja dakika ya 73
na lingine dakika ya 74 hivi kumfanya awe amefunga mabao tano mpaka sasa.
Kocha wa Stars, Mdenmark Kim
Pouslen baada ya mchezo huo, alisema huu ni ushindi muhimu kwa kikosi chake
kwani sasa watacheza robo fainali.
“Vijana wamecheza vizuri
kabisa na kuzingatia kuwa mechi hii ilikuwa muhimu kwao na tumeibuka na ushindi
mnono wa mabao saba,” alisema.
Mbunge Nkamia alisema kwamba
amevutiwa na soka ya vijana leo na anaamini wana uwezo wa kurejea na Kombe
nyumbani. Nkamia aliwapongeza wadhamini wa Stars, Kilimanjaro Premium Lager kwa
kuchangia mafanikio ya timu hiyo tangu waanze kuidhamini na akaomba Watanzania
zaidi wajitokeze mjini hapa kuisapiti timu hiyo.
Meneja wa Bia ya Kilimanjaro
Premium Lager, George Kavishe ametuma salamu za pongezi kwa ushindi wa leo na
mafanikio ya kutinga Robo Fainali na kusema wao wana imani kuwa Stars itarejea
nyumbani na kombe hili.
“Tuna imani kubwa vijana
wataendelea kufanya vizuri, kikubwa tu tuwape sapoti kama watanzania ili
wasonge mbele zaidi,” alisema.
Katika mchezo wa leo, kikosi
cha Stars kilikuwa; Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Issa Rashid, Shomari Kapombe,
Kevin Yondan, Shaaban Nditi, Mrisho Ngassa, Salum Abubakar, John Bocco, Frank
Domayo na Amri Kiemba.
Somalia; Mohalim
Abdullahi/Hussein Abdallah dk30, Ali Mohamed, Said Mahamud, Ali Dadir, Sadaq
Abdikadir, Mohamed Salah, Abdikarim Abubakar, Abdallah Mohamed/Hamza Mukhtar,
Ahmed Abdikadir Dahir/Muhad Hajji na Ali Ahmed Ali.
0 comments:
Post a Comment