RAIS OBAMA AKITOA HOTUBA.
RAIS Barack Obama amemwonya rais wa Syria Bashar al-Assad kwamba atawajibishwa endapo majeshi yake yatatumia silaha za kemikali dhidi ya upinzani nchini Syria.
Obama alitamka hayo katika kikao hapa Washington kusisitiza msimamo wa Marekani dhidi ya ulimbikizaji wa silaha za nuklia na kemikali wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya mkataba wa ushirikiano wa kupunguza vitisho vya silaha za kemikali kati ya Marekani na Russia.
Lakini kilichogonga vichwa vya habari ni onyo lake kwa rais wa Syria, siku moja baada ya Washington kuionya Damascus dhidi ya matumizi ya silaha za kemikali.
Obama alisema Marekani itaendelea kuunga mkono azma halali ya raia wa Syria, na kutoa misaada ya kibinadamu kwa upinzani na katika makabidhiano huru ya madaraka pasipo utawala wa Assad.
Alimwonya rais Assad kuwa dunia inatizama kinachoendelea nchini Syria na kwamba matumizi ya silaha za kemikali kamwe hayatakubalika.
RAIS WA SYRIA ASSAD.
Na ikiwa atafanya kosa la kutumia silaha hizo kutatokea madhara na Assad atawajibika.
Obama alisisitiza kuwa dunia haiwezi kuruhusu karne ya 21 kutumbukizwa katika kiza cha karne ya 20 ya matumizi ya silaha kama hizo.
Alisema jukumu la kuzuia ugaidi wa kutumia silaha za nuklia ni mojawapo ya maswala yaliyopewa kipaumbele kwa usalama wa kitaifa, na kwamba dunia inasogea mbele kuhakikisha hakuna silaha za nuklia katika siku za usoni.
0 comments:
Post a Comment