BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

TUCTA YAIKABA KOO SERIKALI.

 YATAKA KIMA CHA SH 742,000 KWA MWEZI JK ASIKILIZA KILIO, AAHIDI KUONGEZA
 //www.mtanzania.co.tz
Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya.

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limeikaba Serikali likitaka kima cha chini kinachoweza kukidhi mahitaji ya msingi ya mfanyakazi nchini hivi sasa kuwa Sh 742,000 kwa mwezi.

Katibu Mkuu wa TUCTA, Nicholas Mgaya, alisema jana kuwa kiwango hicho kimepanda kutoka kiwango cha Sh 315,000 kwa mwezi mwaka 2006, wakati akihutubia kilele cha Sherehe za Wafanyakazi kitaifa, zilizofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine, mkoani Mbeya.

“Hii ni kutokana na kupanda maradufu kwa gharama za maisha kulikochangiwa zaidi na mfumuko wa bei, kushuka kwa thamani ya shilingi na ongezeko kubwa la bei ya vyakula,” alisema.

Alisema ingawa Serikali imekuwa ikitangaza nyongeza za mshahara kwa wafanyakazi kila mwaka, ongezeko hilo ni dogo mno na itachukua muda mrefu kufikia kima kinachoweza kukidhi mahitaji ya msingi ya mfanyakazi.

“Ndiyo maana TUCTA, tunapendekeza matokeo ya utafiti wote uliofanywa na serikali, TUCTA na mwingineo, utumike sasa kuandaa mpango mkakati wa taifa wa kuondok

ana na tatizo sugu la mishahara,” alisema katika risala hiyo ya wafanyakazi.

Alisema hivi sasa kodi ya mapato kwa wafanyakazi ni mzigo mkubwa, suala ambalo linatakiwa liangaliwe upya.

“TUCTA baada ya kupata ushauri wa kitaalamu tumebaini kuwa kodi hiyo kwa kuanzia inaweza kushuka hadi asilimia 11 bila kuathiri mapato ya seerikali,” alisema.

Akizungumzia misamaha ya kodi, alisema ingawa TUCTA imekwisha kushiriki kuishauri serikali kupunguza misamaha hiyo, jambo hilo halijazingatiwa.

“Kwa mfano takwimu za karibuni zinaonyesjha misamaha ya kidi imefikia Sh trilioni 1.8 mwaka huu, ikilinganishwa na Sh trilioni 1.05 mwaka 2011/12,” alisema.

Alisema haieleweki Serikali inaposema kuwa uchumi wa nchi unazidi kukua wakati hali ya wananchi kwa ujumla inaendelea kuwa duni.

“Umefika wakati sasa kwa serikali kutegua kitendawili hiki cha uchumi unakua wakati ukali wa maisha kwa wananchi unaongezeka.”

Naye Rais Jakaya Kikwete, amesema Serikali imedhamiria kukabili tatizo la ajira kwa vijana nchini.

Amesema Serikali, imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha ajira kwa vijana, ukiwamo mpango ambapo hadi sasa, vimekwisha kuundwa vikundi 512 vya vijana katika mikoa 17 nchini ambao watapewa mitaji ya kuanzisha miradi.

Rais, ambaye alikuwa akilihutubia taifa katika kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya jana, alisema vikundi hivyo vina zaidi ya vijana 5,000.

Aliwataka wakuu wa mikoa, wawahamasishe vijana wajiunge katika ushirika waweze kupata mitaji ya kuanzisha miradi.

Rais alisema wakuu hao wa mikoa watenge maeneo maalum kwa ajili ya miradi hiyo.

Aliipongeza Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA) kwa kuwezesha mradi wa matofali wa vijana wapatao 5,000 ambao wamekuwa wakiyauza matofali kwa Shirika la Nyumba la Taifa.

Akizungumzia suala la mishahara, ambalo limekuwa kilio kikubwa cha wafanyakazi kila mwaka, alisema katika mwaka ujao wa fedha, kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kitakuwa ‘kikubwa kidogo’.

Rais hakukitaja kiwango hicho, lakini alisema kitatajwa wakati wa hotuba ya bajeti ya waziri anayehusika.

Alisema hali hiyo, imewezekana kwa vile Serikali imeweza kuongeza kiwango cha mapato yake kwa mwezi kutoka Sh bilioni 541 hadi Sh bilioni 637 pamoja na kudhibiti ubadhirifu.

Alisema kiwango cha ukosefu wa ajira nchini ambacho hivi sasa ni asilimia 12, ni kikubwa mno, hivyo serikali inaendelea na mikakati ya kutengeneza nafasi za jira.

Nafasi za ajira zipatazo 600,000, zinatarajiwa kutengenezwa katika kipindi kijacho, alisema.

Alisema mifuko kwa ajili ya vijana na wanawake, inaendelea kuboreshwa na kuongezewa fedha, ukiwamo mfumo unaojulikana kama mabilioni ya Kikwete.

Hata hivyo, alisema upungufu ulijitokeza katika mfuko huo ambao ulikuwa ni kutolewa fedha, bila wahusika kupatiwa mafunzo na kutokuwapo ufuatiliaji.

Alisema zamu hii, hakuna atakayepewa fedha kutoka katika mfuko huo, bila kupatiwa mafunzo na kusimamiwa.

Rais aliwaeleza wafanyakazi kuwa hivi sasa unaangaliwa utaratibu ambao wafanyakazi wa umma, wataweza kupatiwa mikopo nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba.

Kwa mara nyingine, aliwaonya Watanzania waache chokochoko zinazoweza kusababisha vurugu na vita za dini nchini.

Alisema ameshangazwa kuona suala la nani achinje kuonekana kuwa tatizo nchini hivi sasa, wakati ni utaratibu ambao umekuwako katika jamii nchini tangu enzi za mababu zetu.

“Tusiwasikilize wanaotaka kutupeleka pabaya. Vita ya dini haina mshindi,” alisisitiza na kuwaasa viongozi wa dini na hasa wanasiasa kuwa mstari kuhakikisha amani haitoweki nchini.

Akizungumzia kiwanja cha ndege cha Songwe mkoani Mbeya, alitaka kiwe kichocheo cha kukuza uchumi katika mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe.

Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, akizungumza kwenye maadhimisho hayo, alisema kima cha chini cha mishahara katika sekta binafsi kinatarajiwa kutangazwa katikati ya mwezi huu.

“Fidia inatarajiwa kuongezeka hadi Sh milioni moja ikilinganishwa na Sh 108,000 za sasa,” alisema.

PINDA.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema Tanzania na dunia kwa ujumla inapitia changamoto nyingi za kisiasa, kijamii na kiutawala, ambayo yanahitaji usimamizi wa karibu wenye maadili mema katika jamii na kuhitaji moyo wa upendo, busara na hekima.

Akizungumza wakati wa kuwekwa wakfu Askofu Mteule, Titus Mdoe kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, alisema sherehe hizo zimefanyika wakati nchi inakabiliwa na changamoto ya vuguvugu la ukosefu wa amani na utulivu katika baadhi ya maeneo.

“Vuguvugu hii haiashirii mema nchi yetu, kuna umuhimu wa viongozi wote, wakiwamo wa dini kusisitiza umuhimu wa Watanzania wote kuishi pamoja kindugu, upendo, ushirikiano na kuvumiliana, vinginevyo nchi yetu itaacha kuwa kisima cha amani na kuingia katika orodha ya nchi zenye migogoro hata kuvunjika kwa amani nchini,” alisema Pinda.

Alisema Tanzania kwa sasa kuna mchakato wa maandalizi ya Katiba mpya na jukumu la kuifanya nchi kuwa katika hali ya amani na utulivu wakati tunaelekea katika chaguzi mbalimbali zinazoanza mwaka 2014.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es Salaam, Mhashamu Kardinali Polycarp Pengo, alisema hana budi kumshukuru Papa Benedict wa XVI kwa kuwa kabla ya kuachia madaraka, aliamua kulishughulikia ombi la kuwa na msaidizi mwingine.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: