Dkt.
Sengondo Mvungi, akiwa kwenye gari la kubeba wagonjwa, baada ya
kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akihamishiwa hapo kiutoka
Hospitali ya Tumbi, Kibaha Jumapili Novemba 3, 2013.
KAMISHNA
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania (CRC), Dkt. Sengondo Mvungi,
amejeruhiwa vibaya sehemu za kichwani na usoni, baada ya kukatwa mapanga,
nyumbani kwake, Kibamba Msakuzi, nje kidogo ya jiji, majira ya saa sita usiku
Jumamosi Novemba 2, 2013.
Kwa
mujibu wa taarifa za ndugu na polisi, Dkt. Mvungi ambaye pia ni Mhadhiri
Mwandamizi wa Sheria, Chuo Kikuu cha Bagamoyo, mkoani Pwani, alicharangwa
mapanga, baada ya kutaka kujua nini kilichokuwa kikiendelea kufuatia mabishano
baina ya mkewe na watu hao ambao walitishia kumuua endapo asingewapa fedha.
Taarifa
zinasema, watu hao sita wengine wakiwa nje ya nyumba kwa nia ya kujihami endapo
wangevamiwa na majirani, walivamia nyumba hiyo yenye ghorofa moja, na kumkuta
mkewe Dkt. Mvungi wakati huo Dkt. Mvungi akiwa kwenye chumba tofauti katika
nyumba hiyo.
Kwa
mujibu wa taarifa hizo, wavamizi walipoona mke wa Dkt. Mvungi anachelewa
kutekeleza maagizo yao,
walifyatua baruti na hapo Dkt. Mvungi akajaribu kuelekea kulikotokea mlio huo
na ndipo alipokutana na mapanga ya kichwani na usoni.
Uchunguzi
wa awali wa polisi umeonyesha kuwa tukio hilo ni la kihalifu, kwani watu hao
ambao kwa sasa wanatajwa kama majambazi, waliiba fedha, simu na laptop, hali
inayoonyesha wazi kuwa nia yao ilikuwa ni kutekeleza wizi.
Dk.
Mvungi aliwahi kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2005 kwa tiketi ya
Chama cha NCCR-Mageuzi.
Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania (CRC), Dkt. Sengondo Mvungi.
0 comments:
Post a Comment