BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

MPASUKO WA CHADEMA SASA MBINU ZA KUSULUHISHA KAMBI ZINAZOKWARUZANA CHINI YA MWAVULI WA USALITI ZIMENZA.

 
JUHUDI za chini kwa chini kusuluhisha kambi zinazokwaruzana katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), chini ya mwavuli wa usaliti zimeanza kuchukua nafasi yake, Raia Mwema, limebaini.
  


Kambi zinazosuguana kwa sasa chini ya kivuli hicho cha usaliti ni ile inayodaiwa kuwa ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe, inayouwanganisha wabunge Tundu Lissu, Peter Msigwa, Godbless Lema, John Mnyika na Katibu Mkuu Dk. Wilbroad Slaa, ambayo inajitambulisha kwa ‘kete’ ya kudhibiti usaliti dhidi ya chama hicho.  

Kambi nyingine ni ile ya Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, yenye wasomi wengi inayotajwa kumuandaa Zitto kuwania nafasi ya uenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani ili kumng’oa mwenyekiti wa sasa Mbowe, kama naye atajitosa kugombea tena wadhifa huo.  


Miongoni mwa wasomi wanaotajwa kuwamo katka kambi hiyo ni pamoja na mwanasiasa  mkongwe wa mageuzi nchini, Profesa Mwesiga Baregu na msomi mwingine aliyekwishajeruhiwa kisiasa ndani ya chama hicho, Dk. Kitila Mkumbo.  


Hata hivyo, pamoja na juhudi hizo za usuluhishi wa kambi hizo mbili zinazoendelea chini kwa chini, kuna uwezekano mkubwa viongozi wa juu wa chama hicho, wakiongozwa na Mbowe, kususia usuluhishi huo na kama itakuwa hivyo, basi katika kipindi cha siku chache zijazo, hatari ya chama hicho kuzidi kupasuka ni kubwa.  


Viongozi wakongwe katika masuala ya mageuzi nchini waliozungumza na gazeti hili wiki hii, wamefananisha kinachoendelea sasa ndani ya chama hicho na kilichokitokea chama cha NCCR-Mageuzi mwishoni mwa miaka ya 1990.  


Wakati huo, NCCR kilikuwa ndiyo chama kikuu cha upinzani hapa nchini, chini ya uenyekiti wa Augustine Mrema, lakini mgogoro mkubwa uliokikumba ulimlazimu akihame chama hicho na kujiunga chama cha TLP na kuhama kwake kukawa mwisho wake wa kisiasa na mwisho wa nguvu kubwa za chama hicho cha mageuzi.  


Mmoja wa wanasiasa wa mashuhuri wa kambi ya upinzani nchini ambaye amejitolea kusuluhisha mgogoro kati ya kambi inayotajwa kuwa ya Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na ile inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema haoni uwezekano wa CHADEMA kutopasuka endapo hali ya sasa itaendelea.  Kila anachofanya Mbowe kwa sasa kinafanana kabisa na kile alichokuwa akifanya Mrema. 


Wakati ule, Mrema alikataa kuwasikiliza wanasiasa waliokuwa na mrengo wa kisomi kama vile akina Dk. Sengondo Mvungi (sasa marehemu) na Mabere Marando na akawa anawasikiliza ‘makomandoo’ wa kisiasa.  Kwake, aliona wasomi wananyatia tu nafasi yake. 


Matokeo yake akawafanya kuwa maadui zake lakini wenzake walimshauri kwa nia njema tu. Taarifa zilizopo zinabainisha kwamba, kwa kadri inavyooneka, Mbowe naye anafanya makosa yale yale.  “Nasikia hawasikilizi kabisa akina Zitto, Profesa Mwesiga Baregu, Marando na Dk. Kitila Mkumbo. 


Yeye anawasikiliza akina Joseph Mbilinyi, Godbless Lema, Tundu Lissu na Peter Msigwa.  “Lakini huwezi kufananisha hawa watu. Akina Baregu wamekuwa kwenye mageuzi kwa miaka zaidi ya 20. Wanaheshimika ndani na nje ya nchi na upeo wao hauna mfano kwenye upinzani.  


“Sasa unaachaje kumsikiliza huyu na ukamsikiliza zaidi mtu ambaye hana sifa za kimageuzi katika ngazi ya kitaifa? Wanaozua tuhuma dhidi ya wenzao hawana hata miaka mitano ndani ya chama?  “Labda nikupe mfano mzuri. 


Hivi unategemea leo, CCM kwa mfano, eti akina Richard Tambwe Hizza, waanzishe mkakati wa kumng’oa kwenye chama mtu kama Kingunge Ngombale Mwiru kwa madai ni msaliti? 


Haya mambo yako CHADEMA tu,” alisema mwanasiasa huyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake kwa maelezo kwamba amefuatwa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA ili awasuluhishe kwenye mgogoro huu wa sasa na kujulikana msimamo wake kunaweza kupunguza kuaminiwa kwake na pande hasimu kwenye mgogoro wa sasa.

Mgogoro wa sasa wa CHADEMA unatokana na hatua ya kikao kilichopita cha Kamati Kuu ya CHADEMA kuamua kuwavua nyadhifa zao zote ndani ya chama Zitto, Dk. Kitila na aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Arusha, Samson Mwigamba.


Raia Mwema linafahamu kwamba mgawanyiko ndani ya chama hicho ulionekana wazi ndani ya Kamati Kuu ya chama kutokana na hoja zilizotolewa na baadhi ya wajumbe kukinzana; wengine wakimtetea Zitto na wengine wakitaka afukuzwe kwenye chama.


Gazeti hili limearifiwa kwamba kambi ya mashambulizi dhidi ya Zitto iliongozwa na Lissu lakini kwenye mitandao ya kijamii, Msigwa –ambaye ni Mbunge wa Iringa Mjini, amekuwa akiendesha mashambulizi dhidi ya Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali.  


Profesa Baregu na Marando ni miongoni mwa waliomtetea Zitto na hoja yao kubwa ilikuwa kwamba kwa vile walikiri makosa yao, kukubali kujiuzulu kwao kulitosha kulimaliza suala hilo badala ya kuliendeleza kwa kuwataka wajieleze kwa maandishi kuhusu makosa yao.  


Dalili za mpasuko  Kuanzia wiki iliyopita, yamekuwepo matamko mbalimbali kutoka mikoani na taasisi mbalimbali kuhusiana na hatua ya akina Zitto kuvuliwa nyadhifa zao.  


Matukio hayo yanaonyesha kwamba uamuzi huo haujakubaliwa na wanachama wote na ndiyo maana wiki iliyopita, makao makuu ya CHADEMA yalianza kutuma baadhi ya makada wake kwenda mikoani kwa ajili ya kueleza maamuzi hayo ya Kamati Kuu kwa wanachama wake.  


Katibu Mkuu wa CHADEMA, alikuwa amepanga kufanya ziara katika mikoa ya Tabora na Kigoma – inayotajwa kuwa ngome kuu ya kisiasa ya Zitto, kuanzia kesho lakini tayari baadhi ya viongozi wa mikoani wameonyesha kutokuwa tayari kuandaa mikutano hiyo.  


Katika taarifa yake iliyotolewa kwa vyombo vya habari juzi,  Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Kigoma, Jafari Kasisiko, alisema ingawa ziara ya Slaa ina lengo la kujenga chama, mazingira yaliyopo sasa hayatoi fursa ya kufanya hivyo.  


Hata hivyo, wana CHADEMA kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wametoa taarifa inayoeleza kuunga mkono maamuzi hayo ya Kamati Kuu na taarifa yao ilitolewa na kiongozi wa matawi ya chama hicho, Frank Sumbe.  


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umebaini kwamba maamuzi hayo yanaungwa mkono zaidi katika mikoa ya Kaskazini na Nyanda za Juu lakini kuna upinzani kwenye mikoa ya Kanda ya Kusini na Ziwa Magharibi anakotoka Kabwe.  


Jana Mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Singida, Wilfred Kitundu, naye alitangaza kujiuzulu wadhifa wake huo akipinga maamuzi hayo ya Kamati Kuu. Pamoja na mambo mengine, Kitundu ndiye mwanachama wa kwanza kujiunga na chama hicho kutokea mkoani Singida.  


Hata hivyo, Raia Mwema limeambiwa kwamba baadhi ya wanachama waandamizi wa CHADEMA wameanza kujipanga kutafuta suluhu ya mgogoro wa sasa kwa kutafuta watu wanaoheshimika nje ya chama hicho kwa ajili ya kazi hiyo.  


“Wenyewe kwa wenyewe hatuwezi kusuluhishana kwa sasa kwa vile tunajuana. La msingi hapa ni kutafuta watu kutoka nje ya chama ambao wanaheshimika na kila upande. Kukubali CHADEMA ife ni kuwaondolea Watanzania tumaini,”alisema mmoja wa wabunge wa CHADEMA ambaye hakutaka kutajwa jina.  


Wakati hali hiyo ya kutokuelewana ndani ya CHADEMA ikiendelea, gazeti hili limeambiwa kwamba wanachama hao watatu waliotakiwa kujieleza, tayari wamekabidhiwa mashitaka yao 11 wanayotakiwa kuyajibu katika kipindi cha siku 14 tangu wakabidhiwe barua zao.  http://www.raiamwema.co.tz
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: