MSHINDI wa shindano la ‘Miss East Afrika 2012’, Joselyn Maro amepiga hodi Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) akilalamikia kutokabidhiwa nakala muhimu za zawadi yake ya gari.
Mrembo huyo alisema jijini Dar es Salaam, juzi kuwa tangu ashinde na kupewa gari aina ya Mazda, hadi sasa hawezi kuliendesha kutokana na kutopewa kadi ya gari hilo.
Alisema, hicho kimekuwa kikwazo cha kulitumia akilazimika kuliegesha nyumbani akisubilia kupata nyaraka hizo muhimu.
Alisema, amekuwa akilazimika kuwasiliana na mratibu wa shindano hilo kampuni ya Lena Events bila ya mafanikio yoyote.
“Mimi nimekuwa nikimwomba kunisaidia suala hili la gari lakini ushirikiano umekuwa hakuna, niliamua kwenda Basata tangu Februari, ninasubiri majibu” alisema mrembo huyo.
Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Sanaa wa Basata, Vivia Sharua alikiri kupokea malalamiko ya Miss huyo na kusema ofisi yake imekuwa ikifanya jitihada za kumpata mwandaaji huyo bila ya mafanikio.
“Sisi tumekuwa mara kwa mara tukimwandikia barua ya kumuita kwenye kikao lakini inaonekana kuwa amekuwa akituchenga” alisema Shalua.
Aliongeza kuwa, Basata wamepata pia malalamiko kutoka kwa mtoaji wa gari hiyo yenye thamani ya dola 18,000 za Marekani, akisema hajamaliziwa fedha zake.
Shalua alisema kutokana na kutolipwa kwa fedha zake mmiliki alietoa gari hilo, amezuia kadi ya gari ili lisiruhusiwe kutumika hadi amaliziwe fedha zake.TANZANIA DAIMA

0 comments:
Post a Comment