PUMZI YA MWISHO KWA EDWARD LOWASSA NA BERNAD MEMBE KUELEWEKA LEO ?.
Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete akipiga makofi wakati alipowasili katika mkutano wa chama hicho Mjini Dodoma hivi karibuni. Picha ya Maktaba,
Dar es Salaam. Wakati makada wa CCM wakivuta pumzi ya mwisho kwa matarajio ya kuondolewa kifungo cha miezi 12 ili wajitose rasmi kuwania urais, Kamati Kuu ya chama hicho inakutana leo kukiwa na habari kuwa itatumia muda mwingi kujadili mwelekeo wa mchakato wa Kura ya Maoni na badala wa wanachama hao sita.
Adhabu ya makada sita wa CCM ya kufungiwa miezi 12 ilishaisha tangu kastikati ya mwezi huu na sasa wanasubiri kwa hamu tangazo la Kamati Kuu la kumalizika kwa adhabu yao ili wawe huru kutangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho na kuendelea na shughuli nyingine za kujiandalia mazingira ya kupitishwa na Halmashauri Kuu.
Makada hao ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Edward Lowassa na Fredrick Sumaye, ambao waliwahi kuwa mawaziri wakuu, William Ngeleja, Steven Wasira, ambaye ni Waziri wa Kilimo na Chakula, na January Makamba, ambaye ni Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia.
Hadi sasa makada hao, ambao walituhumiwa kuanza harakati za kampeni kabla ya muda, hawajatangaza rasmi nia ya kuwania urais na habari zinasema kuwa wamekuwa kwenye maandalizi ya kufanya hafla kubwa ya kutangaza mpango huo.
Lakini habari ambazo Mwananchi imezipata zinasema kuwa kuna uwezekano mdogo wa Kamati Kuu kuzungumzia suala hilo kwa kuwa kikao hicho kitajikita zaidi kuzungumzia mwenendo wa mchakato wa Kura ya Maoni ambao unaonekana kuyumba.
“Watu wameandika sana kuhusu Kamati kufanya uamuzi wa wagombea urais waliofungiwa, lakini nakuhakikishia suala hilo halitazungumzwa labda iweje sijui,” alisema mpashaji habari wetu aliye ndani ya chama hicho.
“Suala linalosumbua kwa sasa ni Kura ya Maoni na hilo ndilo litachukua muda mwingi.”
Alisema kamati Kuu itatoa mwelekeo wa Kura ya Maoni, ambayo mchakato wake unapingwa vikali na vyama vya upinzani ambavyo vinasema uchache wa vifaa, muda mdogo wa maandalizi, watendaji na matumizi ya teknolojia ya uchukuaji wa taarifa za wapigakura kuwa vinaweza kfanya kazi ya uandikishaji kuchukua muda mrefu na hivyo Kura ya Maoni isipigwe Aprili 30 kama ilivyotangazwa na Rais Jakaya Kikwete.
Kada mwingine wa chama hicho pia aliidokeza Mwananchi kuwa wagombea hao waliofungiwa watabidi kuvuta pumzi zaidi kabla ya kuachiwa huru rasmi.
Mmoja wa wasaidizi wa kada aliyefungiwa alipoulizwa kuhusu mipango ya bosi wake kutangaza rasmi kugombea, alisema: “Sisi tunaisubiri Kamati Kuu tu. Ikitangaza kumalizika kwa adhabu tu, hata wiki ijayo tutatangaza rasmi.”
Alipoulizwa kuhusu kikao hicho cha leo, katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuzungumzia ajenda.
Hivi karibuni, Nape alithibitisha kuwa muda wa adhabu hiyo ulikuwa ukingoni na kuwa viongozi hao sita wangefanyiwa tathmini na kamati ndogo ya maadili ili kubaini iwapo adhabu hiyo ilitekelezwa ipasavyo.
Kikao hicho kinafanyika wakati upepo wa kisiasa ndani ya chama hicho ukiwa haujatulia na ikionekana wazi kuwa makada waliofungiwa wameanza kupoteza uvumilivu na sasa wafuasi na mashabiki wao wanajitokeza waziwazi kutangaza misimamo yao kwa mtu wanayeona anafaa kuteuliwa na chama hicho kugombea urais.
Hivi karibuni, Dk Raphael Chegeni aliiambia Mwananchi kuwa ametumwa na wanachama wa CCM kutoka Kanda ya Ziwa kwenda kumshawishi Lowassa ajitokeze kuwania urais, ikiwa ni kuitikia wito wa Rais Kikwete ambaye aliwataka wana-CCM kuwashawishi watu wanaowaona wanafaa kugombea nafasi hiyo kubwa nchini.
Habari hiyo pia iliambatana na taarifa kuwa baadhi ya wafuasi wa mbunge huyo wa Monduli walienda kuangalia uwezo wa kutumia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha kwa ajili ya hafla ya kutangaza nia.
Hata hivyo, zikiwa zimesalia siku chache kabla ya harakati za kugombea urais na ubunge kuanza na ukweli kwamba wanachama wengine wanaendelea kujinadi, Kamati Kuu inaweza kutoa msimamo kuhusu adhabu za makada hao.
Kikao hicho kitakachoongozwa na mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ni cha pili kufanyika mwaka huu. Katika kikao cha kwanza kilichofanyika Kisiwandui, Zanzibar Januari 13, kiliagiza adhabu kali zichukuliwe dhidi ya vigogo watakaobainika kukiuka masharti ya adhabu ya mwaka mmoja waliyopewa ambayo ilimalizika Februari 18.
Kikao hicho pia kiliahirisha kutoa ratiba ya mchakato wa uchaguzi kwa chama hicho, ambayo hueleza tarehe ya kuanza kuchukua fomu na kurudisha, muda wa kampeni, tarehe za vikao vya kupitisha wagombea kwenye ngazi ya ubunge na urais na tarehe ya vikao vya mwisho vya kitaifa kwa ajili ya kupitisha wagombea wa ngazi zote.
Kamati ndogo ya Maadili inayoongozwa na makamu mwenyekiti wa CCM-Bara, Philip Mangula ndiyo iliyopewa jukumu la kufanya tathmini ya vigogo hao sita kuona kama walitekeleza ipasavyo adhabu waliyopewa, kisha kupeleka mapendekezo yake katika kikao cha Kamati Kuu.
Mbali na vigogo hao, kamati hipo pia imeshamuhoji aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge kutokana na kuhusika katika sakata la uchotwaji fedha kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow.
Katika mgawo huo wa Escrow, Profesa Tibaijuka alipokea Sh1.6 bilioni, sawa na Chenge wakati Ngeleja alipokea Sh40.4 milioni. Profesa Tibaijuka na Chenge wamefikishwa mbele ya Sekretarieti ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma kuhusu tuma hizo.
Chenge na Ngeleja wote ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (Nec), ambapo kwa mujibu wa mazimio ya Kamati Kuu iliyokaa Zanzibar, makada hao pamoja na Tibaijuka ikiwa watakutwa na hatia, suala hilo litafikishwa mbele ya Kikao cha leo na kupewa adhabu, ikiwamo kuvuliwa nyadhifa zao ndani ya chama.
Hatma ya vigogo hao imebaki mikononi wa kamati ya Mangula ikitegemea zaidi kile ambacho makamu mwenyekiti huyo atakiwasilisha katika kikao hicho cha Kamati Kuu.
Kamati Kuu inaundwa na mwenyekiti wa CCM, makamu wake na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, ambaye ni Rais wa Zanzibar. Wengine ni wajumbe 14 waliochaguliwa na Mkutano Mkuu, ambao ni Stephen Wasira, Pindi Chana, Professa Tibaijuka, Jerry Slaa, Adam Kimbisa, Dk Emmanuel Nchimbi na William Lukuvi kutoka Bara.
Wengine ni Shamsi VuaiNahodha, Dk Hussein Mwinyi, Profesa Makame Mbalawa, Dk Salim Ahmed Salim, Dk Maua Daftari, Hadija .H. Abuu na Samia Suluhu Hassan kutoka Zanzibar.
Wakati huohuo, katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana kesho anaanza ziara ya siku tisahuku akitarajia kukutana na kero ya ardhi wilayani Kondo.
Taarifa iliyotolewa jana na katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Albert Mgumba, Kinana atapelekwa maeneo ya Bahi, Mnemia na Itaswi ambayo yana migogoro ya wakulima na wafugaji.
Ziara ya hiyo inaanzia Wilaya ya Mpwapwa kesho asubuhi na itaanzia jimbo la Mpwapwa kabla ya kwenda Kibakwe.
“Kila kitu kimekamilika na sina shaka. Katibu atafanya ziara kama alivyotarajia kwenye maeneo hayo,” alisema Mgumba.
Alitaja lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi na kuhimiza utekelezaji wa Ilani.MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment