BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WANANCHI WAOMBWA KUMSAIDIA RAIS MAGUFULI KUKAMUA MAJIPU MADOGO


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi

Dar/mikoani.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewataka viongozi wa dini kuihamasisha jamii kumsaidia Rais John Magufuli kukamua majipu madogomadogo ambayo yapo kila mahali nchini na kumuachia mkuu huyo wa nchi yake makubwa.

Akihutubia mamia ya wananchi waliohudhuria mkesha wa mwaka mpya wa kuombea Taifa amani, uliofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam juzi, Lukuvi alisema kuna ubadhilifu katika ngazi za chini kama vile halmashauri na kwamba wananchi wanatakiwa kuchukua hatua bila kumsubiri Rais.

“Majipu ya Rais Magufuli yako mengi kila mahali, tumuachie aendelee kukamua majipu makubwa lakini vijipu vidogovidogo hataviweza, tunatakiwa kumsaidia kuvitumbua,” alisema. 


Alisema kuna watumishi wanaoendelea kupokea rushwa ili watoe huduma na pia wako wanaopoteza mapato ya Serikali kwa wizi. “Ni lazima watu wa aina hii tuwafichue na kuwachukulia hatua ili wengine wenye nia kama hiyo waogope kutenda uovu huo,” alisema.

Aliwaomba viongozi wa dini kumuombea Rais Magufuli ili aweze kuwashughulikia kikamilifu wala rushwa, wabadhirifu na wezi wa mali za umma.

Akizungumzia katika mkesha huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema:

“Tulikuwa na Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 wengi walidhani nchi ingetumbukia katika vurugu lakini kupitia maombi, Mungu ametuvusha salama.”

Alisema mbali na kuvuka salama, pia Tanzania imepata Rais bora ambaye amekuwa gumzo katika nchi mbalimbali duniani. “...Kila nchi inataka awe rais wao Mungu ampe ujasiri ili aendelee kuwatumikia Watanzania, viongozi wa dini mtuombee nasi tunaomsaidia tuwe wajasiri kama yeye, ” alisema.

Awali, akiwakaribisha viongozi hao, Mwenyekiti wa mkesha wa kuombea Taifa amani, Askofu Godfrey Malassy alisema sadaka zilizopatikana katika mjumuiko huo, zitatumika kununulia vifaa vya umeme wa jua vitakavyofungwa katika vituo vya afya mkoani Tabora.

“Tumelenga kuwasaidia wanawake wanaojifungua kwenye vituo vya afya ambavyo havina umeme kwa kuwafungia vifaa vya umeme jua vijijini,” alisema.

Alisema viongozi wa dini hawatachoka kumuombea Dk Magufuli ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa kuwa ameonyesha ujasiri kufichua ubadhirifu.

“Tuko na Magufuli katika maombi yetu na tunafanya hivyo kwa kuwa dalili zinaonyesha Tanzania itapiga hatua za kimaendeleo kama akiendelea na spidi anayoionyesha,” alisema.

KKKT wamuombea Magufuli
Jana asubuhi, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa aliongoza ibada ya kumuombea Rais Magufuli na baraza lake ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu. 


Ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Azania Front iliambatana na ile ya shukrani ya kuanza mwaka mpya.

Dk Malasusa alisema ni jukumu la kanisa hilo na Watanzania kuendelea kuwaombea viongozi wa nchi ili amani iliyokuwapo miaka ya nyuma iendelee kutawala mwaka huu.

Juzi usiku, Mchungaji Charles Mzinga wa kanisa hilo aliwataka waumini kuwa wanyenyekevu kwa Mungu na kupendana ili kutimiza kusudi la uhai waliojaliwa bila malipo yoyote.

Mwaka wa kujirekebisha
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Titus Mdoe amewataka Watanzania kutumia mwaka huu kujirekebisha tabia kwa kuacha ubinafsi, rushwa na ufisadi na kuongeza uzalendo, uaminifu, uungwana na kufanya kazi kwa bidii.

Akihubiri katika ibada ya mkesha wa shukrani kwa Mungu kwa kumaliza salama mwaka 2015 juzi usiku, Mdoe alisema matendo mengi ya kurudisha nyuma Taifa yanafanyika kwa sababu watu hawana hofu na Mungu.

Alisema kuna watu wamekabidhiwa ofisi kubwa zinazolibeba Taifa wakidhani wamepatiwa kutokana na shahada zao, utendaji au uhusiano na watawala bila kuhusisha kuwa bosi wao ni Mungu.

“Kuna watu vyeo vingine wamepewa kwa ushkaji kama wanavyosema vijana wa sasa. Lakini hata kama umepewa kiushkaji fanya kazi kwa bidii na umshukuru Mungu. Ukweli ni kwamba hata kama una madigrii ukienda pale bila ya Mungu utaitumia nafasi hiyo kuharibu ulimwengu,” alisema.

Kuishi tunu za Nyerere
Katika mahubiri yake, Padri Joseph Mosha wa Kanisa la Mtakatifu Petro aliwataka waumini kuzienzi tunu za Mwalimu Julius Nyerere ambazo ni utu, amani, upendo, uzalendo, kuheshimiana na kutokuwa na ubaguzi wa dini, rangi wala kabila.

“Tuziishi zile tunu za Baba wa Taifa, akiwa bado hai alihimiza Watanzania kuwa na upendo kwa watu wote, kuwa na utu, vitu hivi ndivyo vimeendelea na kuifikisha Tanzania ilipo, basi ili tuendelee kuwa hivi tulivyo tuziishi,” alisema.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: