BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WATANZANIA KUPUNGUZIWA KIDUCHU GHARAMA ZA MATUMIZI YA UMEME NA TENESCO

SHIRIKA la Umeme (Tanesco) limetoa mapendekezo ya kutaka kushusha umeme kwa asilimia 1.1 kwa mwaka huu, huku Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na Ewura (Ewura CCC), likieleza kuwa lilitarajia bei hiyo ishuke zaidi.

Akitoa maoni ya Baraza la Ushauri la Serikali (GCC) jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa baraza hilo, Amani Mafuru alisema Tanesco kukubali kushusha bei ya umeme, kutaleta ahueni kwa wateja wake kwani wanaweza kupata huduma kwa gharama nafuu.

Hata hivyo, alisema Baraza hilo linaitaka Ewura kufanya upembuzi yakinifu, ili kupungua kwa bei ya umeme isije ikawa sababu ya shirika hilo kushindwa kujiendesha au kujiendesha kwa hasara.

“Baraza linaishauri Ewura kufanya uchambuzi makini, ili baadae kupungua kwa bei kusije kukaifanya Tanesco kushindwa kujiendesha na hivyo kuomba ruzuku ya Serikali,” alisema.

Alisema kwa mujibu wa hesabu za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2013, Tanesco ilipata hasara ya zaidi ya Sh bilioni 467, hivyo baraza lina wasiwasi kama Tanesco itaweza kujiendesha.

Alibainisha kuwa ni muda muafaka kwa shirika hilo kuwa na mipango endelevu, ili kuachana na utumiaji wa mitambo ya mafuta na badala yake ianze kuweka mipango ya kubadili mitambo hiyo ili itumie gesi asilia.

Mafuru alisema kutokana na hatua hiyo, Tanesco isije ikaingia katika matatizo makubwa ya kifedha na kujikuta ikilazimika kuomba ruzuku serikalini ili iweze kujiendesha. 


“Ewura ijue kuwa Tanesco ni shirika kubwa hivyo halipaswi kuwa tegemezi kwa Serikali kwa shughuli zao za kujiendesha,” alisema.

Akitoa maoni yake, Kaimu Mwenyekiti wa Ewura CCC, Thomas Mnunguli, alisema punguzo hilo la bei ya umeme kwa asilimia 1.1 kwa mwaka huu na 7.9 kwa mwaka ujao ni dogo na halitarajiwi kuleta unafuu wowote kwa mtumiaji.

Alisema baraza hilo lilitarajia kuwa punguzo hilo lingekuwa kubwa zaidi hasa ikizingatiwa kuwa mazingira ya sasa yanaruhusu bei hizo kushuka zaidi, ikilinganishwa na mwaka 2013 wakati wa bei za sasa zilipopangwa na Ewura.

“Mazingira mazuri kwa sasa ni kama kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme wa maji baada ya mabwawa makuu ya umeme wa maji kupata maji, kuongezeka kwa uzalishaji umeme wa gesi ambao ni rahisi kuliko ule wa mafuta ya petroli,” alisema Mnunguli.

Alisema kama ombi hilo litakubaliwa, tafsiri yake ni kuwa bei hizo zitaendelea kuwa juu kwa asilimia 38.1 kulingana na bei ya umeme ya mwaka 2013 kabla Ewura haijapandisha bei.HABARILEO
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: