BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

RAIS MAGUFULI AFANYA MABADILIKO MAKUBWA KWA KUWAPIGA CHINI WAKUU WA WILAYA 100 NA KUTEUA WAPYA.

 
Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli .

Dar es Salaam.
Miezi saba baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli ameendelea kupanga safu yake baada ya kuteua wakuu wa wilaya 139 huku akiwatema 100 wa zamani.

Kati ya wakuu hao wa wilaya wapya, 22 walikuwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri ambao wamepandishwa cheo kutokana na utendaji mzuri wa kazi.

Uamuzi huo wa kuwatosa huenda ukawa umetokana na vigezo alivyoviweka alipofanya uteuzi wa wakuu wa mikoa ambavyo vilikuwa ni suala la migogoro ya ardhi, tatizo la elimu hasa upungufu wa madawati, njaa na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu.

Rais alitangaza vigezo hivyo wakati akizungumza na wazee wa Jiji la Dar es Salaam Februari 15 na baadaye alizungumzia pia suala la wafanyakazi hewa ambao wamekuwa wakilipwa mishahara bila ya viongozi kuchukua hatua.

Katika mkutano huo, Rais alitoa mfano wa Wilaya ya Bariadi iliyopo Mkoa wa Simiyu, akisema imejenga kilomita 4.5 za barabara ya lami kwa Sh9.2 bilioni, fedha ambazo zingetosha kujenga kilomita 22 mpaka 23 za lami.

Katika kuonyesha kuwa alikuwa na vigezo vyake, Rais amemtosa aliyekuwa Mkuu wa wilaya hiyo, Ponsiano Nyami na kumteua Festo Kiswaga kuziba nafasi yake.

Vigezo vya uteuzi

Taarifa iliyotolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk John Kijazi imeeleza sifa za uteuzi wa wakuu wapya wa wilaya 100 kuwa ni vijana, elimu na uzoefu katika maeneo mbalimbali.

“Rais amewashukuru sana kwa utumishi wao mzuri na amesema pale ambapo itahitajika, Serikali itaendelea kuwatumia katika majukumu mengine,” alisema Dk Kijazi.

Alisema wakuu hao wa wilaya wanatakiwa kufika Ikulu, Dar es Salaam Jumatano kwa ajili ya kula kiapo cha maadili ya uongozi na kupewa maelekezo mengine kabla ya kurejea katika wilaya zao kusubiri kuapishwa na wakuu wa mikoa.

Ma DC wanahabari watoswa

Katika uteuzi huo, Rais amewatosa takribani wanahabari saba waliokuwa wakishikilia nyadhifa hizo huku akiwapa nafasi wanahabari wawili, Daniel Chongolo ambaye ni Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano CCM kuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido na Godwin Gondwe kuwa Mkuu wa Wilaya ya Handeni. Gongwe ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Tumaini na mtangazaji wa Kituo cha Televisheni cha ITV.

Wanahabari waliotoswa katika uteuzi huo na zilizokuwa wilaya zao katika mabano ni Betty Mkwasa (Mvomero), Jackline Liana (Nzega), Shaban Kissu (Kondoa), Novatus Makunga (Moshi), Muhingo Rweyemamu (Morogoro), Halima Kihemba (Kibaha), Baraka Konisaga (Nyamagana).

Mwandishi mwingine wa habari ni aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Iramba, mkoani Singida, Lucy Mayenga ambaye alimuomba Rais Magufuli asimjumuishe kwenye orodha ya wakuu hao wapya.

Katika orodha hiyo, mwanahabari aliyefanikiwa kubaki ni Seleman Mzee ambaye ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi.

Rais Magufuli pia amemteua Kippi Warioba, mtoto wa Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais mstaafu na Mwenyekiti wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi. Katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Kippi aligombea ubunge katika Jimbo la Kawe kwa tiketi ya CCM na kushindwa na Halima Mdee wa Chadema.

Miongoni mwa wakuu wa wilaya maarufu waliobaki ni pamoja na Gulamu Hussein Kifu (Kibiti) na Richard Kasesela (Iringa). Katika uteuzi huo Rais ameteua Humphey Polepole kuwa Mkuu wa Wilaya mpya ya Ubungo. 


Polepole ambaye alikuwa mjumbe wa Iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara uteuzi ambao ulifanyika Aprili 18. 

Pia yumo Asumpter Mshama ambaye alikuwa Mbunge wa Nkenge mkoani Kagera kuanzia mwaka 2010 hadi 2015. 

Mshama ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kibaha mkoani Pwani sambamba na Said Mtanda aliyeteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Nkasi. Mtanda alikuwa Mbunge wa Mchinga kati ya 2010-2015.MWANANCHI
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: