MBARALI UNITED FC YATEMA POINTI TATU MBELE YA SABASABA UNITED FC LIGI DARAJA LA PILI MOROGORO
Nahodha wa timu ya Mbarali United FC, Jonathan Mwaibindi akimzuia mshambuliaji wa Sabasaba United FC, Gamba Matiko wakati wa ligi daraja la pili uliofanyika uwanja wa jamhuri Morogoro na Mbarali United kukung'utwa bao 3-2.
Juma Mtanda, Morogoro.
Timu ya soka ya Mbarali United FC ya mkoani Mbeya imekiona cha mtema kuni baada ya kushindwa kuhimili kasi na kujikuta wakipelekwa puta na mchakamchaka na timu ya Sabasaba United FC ya Morogoro katika ligi daraja la pili 2016/2017 kwa kuambulia kipigo cha bao 3-2 katika mchezo uliofanyika uwanja wa jamhuri mkoani hapa.
Sabasaba United FC inayonolewa na kocha mkuu, Amri Ibrahim ilitandaza soka lenye kasi na kuelewana zaidi pamoja na maarifa na kupelekea Mbarali United FC ichanganyikiwe na kuwapa mwanya wenyeji kutengeneza mashambulizi mengi langoni mwao.
Ndoto za Mbarali United FC kupata matokeo mazuri katika mchezo huo yaliyeyuka na kujikuta wakiinamisha vichwa chini baada ya kutandikwa bao la ushindi dakika za lala salama.
Hesabu za Mbarali United kuibuka na ushindi zilizimwa na mshambuliaji wa Sabasaba United, Shaibu Mguhi dakika ya 90+2 aliyepokea pasi ya, Stanley Mkachage na kufumua shuti kali akiwa nje ya 18 na mpira kujaa wavuni na kumwacha kipa, Fevick Joshua asijue la kufanya na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa Sabasaba United kufuatia ushindi huo.
MTANDA BLOG ilishuhudia katika mchezo huo Mbarali United FC ikianza kupata bao la mapema lililofungwa na, Kelvin Jackson aliyenasa pasi ndefu na kumchanganya kipa wa Sabasaba United FC, Kelvin Igendeneze baada ya mshambuliaji huyo kuwatoka walinzi na kukwamisha mpira kimiani.
Wenyeji walisawazisha bao hilo dakika ya 19 kwa njia ya mkwaju wa penalti kupitia kwa, Daud Pascal kufuatia mchezaji wa Mbarali United United FC kuunawa mpira ndani ya 18 na mwamuzi wa mchezo huo, Nassibu Hamza kutoka Kilimanjaro kutoa adhabu hiyo.
Bao la pili kwa Mbarali United FC lilikwamisha wavuni na, Maiko Aloyce baada ya kazi nzuri ya, Mlidy Jangai wakati Sabasaba walisawazisha kwa bao lililofungwa na Shabaan Maneno na kufanya mchezo huo umalizike kwa Mbarali United FC kutandikwa bao 3-2.
Timu ya Mbarali United FC baada ya kufunga bao la pili ilikuwa ikiamini kuibuka na ushindi ndani ya dakika 90 lakini Sabasaba United FC ilitulia na kuanza mchezo wa kasi na kufanikiwa kusawazisha bao la pili na kuongeza lingine dakika za nyongeza 90+2.
0 comments:
Post a Comment