MWANAMKE ALIYEKUFA WAKATI AKIOMBEWA UGONJWA ILI APONE NA NABII RAJABU AZIKWA ARUSHA
MWANAMKE aliyedaiwa kufa wakati akiombewa na mchungaji aliyejulikana kama ‘Nabii Rajabu’, Lightness Kivuyo mkazi wa Unga-Limited, amezikwa jana kwenye makaburi ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Sokoni-One, kusini mwa jiji la Arusha.
Taarifa kutoka kwenye familia ya marehemu zinaeleza kuwa hawakuona sababu ya kuendelea kuchelewesha maziko ya mwanamke huyo, ambaye kifo chake kilikuwa mikononi mwa nabii huyo wa Kwa-Mrombo, sasa kimekuwa gumzo jijini hapa.
“Tumeshapata gari na sasa tunaelekea kwenye hospitali ya Mount Meru kuuchukua mwili wa marehemu kwenda kuuzika kule Sokoni One,” alisema baba mkubwa wa marehemu, Ally Kivuyo. Lightness ameripotiwa kufa wakati akifanyiwa maombi nyumbani kwa mchungaji mmoja aliyejulikana kama ‘Nabii Rajabu’ eneo la Kwa-Mrombo jijini hapa juzi.
Kwa mujibu wa dada wa marehemu, Juliana Daudi, ameacha mgane na watoto wawili. Habari zaidi zinasema kwamba Polisi sasa inawashikilia watu watatu kuhusu tukio hilo. Watu hao ni mume wa marehemu, Shafii Mohammed ambaye ndiye amemsindikiza mkewe nyumbani kwa nabii huyo, nyakati za usiku, mchungaji huyo, Nabii Rajabu pamoja na mkewe ambaye jina lake halikupatikana mara moja.
Katika ibada hiyo ya maombi Lightness alifariki huku akiwa amenyolewa nywele zote na nyusi. Wakisimulia mkasa huo Juliana alisema kuwa shemeji yake (mume wa Lightness) alifika nyumbani akiwa anahema, huku akidai kuwa dada yake alikuwa kwenye hali mbaya kwenye maombi.
Alisema aliondoka mbio na kwenda kwa Mrombo, nyumbani kwa Nabii Rajabu na kumkuta dada yake amelazwa kwenye kochi, akiwa bila nguo isipokuwa tu khanga alizofunikwa nazo. Polisi jijini hapa wamesema kwamba wanachunguza kifo hicho kwenye ‘maombi tatanishi’.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo watuhumiwa watafikishwa mahakamni mara tu upelelezi utakapokamilika.
Daktari Mfawidhi katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru, Jackline Uriwo alikiri juzi kupokea mwili wa marehemu huku akisema kuwa mume wa marehemu na watu wengine walipofika hospitalini usiku, Kwanza walijaribu kuwadanganya kuwa mama huyo alikuwa hai na kwamba aliletwa kwa ajili ya matibabu, lakini wakagundua kuwa walichopokea ni mwili mfu, hivyo wakaupeleka kwenye chumba cha kuhifadhi maiti.
Mkurugenzi wa huduma ya mazishi katika hospitali hiyo ya mkoa, Daktari Francis Coster alisema kuwa mwili ulipelekwa pale na mume wa marehemu ambaye alisisitiza kuwa mkewe hajafa bali kazimia tu, na kwamba mara nyingi huzimia kwa saa nyingi.
Dk Coster aliongeza kuwa ilibidi na wao wasiweke mwili kwenye jokofu na kuulaza kwenye machela kwa saa sita na ndipo wakaamua kuuweka kwenye droo za maiti kwani ilikuwa wazi sasa kwamba asingeamka tena asilani.
Waganga hospitalini hapo wamekiri kuwa marehemu alifika hapo akiwa amenyolewa upara huku mwili wake ukiwa na mikwaruzo pamoja na uvimbe, hususan maeneo ya mikono na kifua.
Baba mkubwa wa marehemu, Ally Kivuyo ambaye ndiye mlezi wa Lightness alisema kuwa mume wa marehemu Shafii, alikwenda kwake kumtaarifu kuwa mkewe alikuwa amefariki wakati akipata matibabu hospitalini.
“Lakini baadaye ndio nikaletewa taarifa zingine kuwa, Lightness kumbe alikufa wakati akifanyiwa maombi au vitu vingine, nyumbani kwa mtu anayeitwa ‘Nabii Rajabu,’ hapo basi ikabidi niwataarifu polisi ambao walikuja kumkamata mumewe pamoja na huyo anayejiita nabii au mtabiri,” alisema Kivuyo.
0 comments:
Post a Comment