BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMA AZIDI KUNG'ANG'ANIWA NA JESHI LA POLISI TUHUMA ZA MADAWA YA KULEVYA

 
JESHI la Polisi bado linaendelea kumshikilia Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kwa ajili ya upelelezi zaidi baada ya mahojiano ya awali kuonyesha viashiria vya kutomuachia kwa sasa.

Gwajima, ambaye ni mmoja wa watuhumiwa 65 waliotajwa katika uchunguzi wa biashara ya dawa za kulevya na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliripoti Kituo Kikuu cha Kati cha Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam juzi.

Jana wananchi walifurika kituoni hapo huku wakiwashuhudia watu waliotajwa katika orodha ya Makonda wakiwasili na wengine wakisubiri kuitwa kwa ajili ya kuwadhamini.

Baadhi ya waliofika kituoni hapo ni aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni (CCM), Idd Azzan na mfanyabiashara Hussein Mkangala maarufu kwa jina la Hussein Pamba Kali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini, Kamshina wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alisema kati ya watu 65 waliotajwa na Mkuu wa Mkoa, wawili walifika kituoni hapo juzi akiwamo Askofu Gwajima.

Alisema watuhumiwa hao walilala maabusu na uchunguzi bado unaendelea, hivyo wengine waliotajwa wanaombwa kufika kama walivyotakiwa.

Kamishna Sirro alisema timu ya upelelezi iko tayari ikiwasubiria wahusika wahojiwe na watakaobainika kuhusika wataendelea kuhojiwa zaidi na watakaoona hawahusiki wataachiwa.

Alisema wale ambao wanaendelea kuwashikilia wameonyesha kuwa na vitu vinavyoashiria waendelee kuvipeleleza.
“Anayefika hapa si lazima tumweke ndani.

Tukikuhoji tukafuatilia baadhi ya mambo yanayotakiwa ya msingi. Tunaita ni mahojiano ya awali na upelelezi mwingine wa awali ukifanyika tunaweza kujua tuna mtu wa aina gani na hapo ndipo tunajua unabaki au unatoka," alisema Sirro.

“Kama kuna vitu ambavyo vitatuonyesha kuna dalili fulani, tutabaki na wewe kwa ajili ya kuthibitisha ukweli wa yale ambayo tunafikiria ambayo upelelezi umeonyesha, hivyo si kila mtu anayekuja lazima abaki kituoni.

"Walikuja wale wamiliki wa hoteli tuliwahoji tukaona kimsingi hakuna kitu chenye uzito tukawaachia... tukakubaliana nao vitu vya kufanya.”

Aliwataka watu wasiwe na woga maana wamekuwa na dhana kwamba mtu ukishafika kituoni hapo na kuonana na Kamshina Sirro "utawekwa ndani jambo ambalo si la kweli".

“Huna sababu ya kuwa na uwoga wowote maana kuna watu wanapiga simu sana. Tumefanya nini? Wengine wanatuma ndugu zao, hakuna sababu ya kutuma ndugu kwa ajili ya kumwona Kamshina Sirro.

"Suala la msingi umetajwa na wewe unajua uko safi njoo uripoti kwenye ile timu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa, watakuhoji na wakikuona huhusiki watakuachia.”

Kamshina Sirro alisema kwa wale ambao wametakiwa kufika halafu wakakaidi amri hiyo, watawafuata maana hiyo ndio dawa.

“Kama umeitwa halafu hautaki kuja, tutakufuata. Hiyo ndiyo dawa tu lakini kwa yule mwenye busara kamili anaitwa polisi, tena anahojiwa na Kamishna Sirro, nafikiri ni heri angekuja kama ameshindwa kufika jana akawa na sababu zake za msingi akaja kesho (leo) hakuna ubaya.”

Alisema kuna baadhi ya watu walioitwa wametuma taarifa kupitia mawakili wao kuwa watafika baada ya muda fulani.

“Unaweza ukasema waje leo na mwingine labda ni mgonjwa wa kitandani, sasa hapo utafanyaje? Tukipatiwa taarifa, hakuna tatizo.

"Lengo la upelelezi huu sio kukomoa watu, ni kutaka kupata ukweli kuhusu hao watu wanaotuhumiwa.” 


Jumatano Makonda alitaja orodha ya watu 65 na kuwataka kujisalimisha polisi jana kwa ajili ya kuhojiwa na kwamba miongoni mwao wamo wanaojihusisha na uuzaji, wanaotumia na wenye taarifa za kuwezesha jeshi la polisi kuupata mtandao mzima wa dawa za kulevya.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: