BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

HUYU NDIYE RAIS MSTAAFU WA SIERRA LEONE AMBAYE MAISHA YAMEMPIGA NGWALA



Na Geofrey Chambua
DUNIANI tunajifunza na kuona vitu vingi tofauti vya kushangaza, kuogofya na kufurahisha. Wengi hawamjui Valentine Strasser ambaye aliwahi kuwa rais wa nchi ya Sierra Leone kati ya Aprili 29, 1992 hadi Januari 16, 1996

Wakati akiingia madarakani aliweka rekodi ya kuwa kiongozi mwenye umri mdogo kuwahi kutokea. Hata sasa, hakuna taifa ambalo limewahi kupata Mkuu wa Nchi mwenye umri chini ya miaka 25 ili avunje rekodi ya Strasser (KUMBUKA Joseph Kabila aliingia madarakani akiwa na miaka 27 ILIHALI Yahya Jammeh alikuwa na umri wa mika 29 alipompindua Sir Dawda Jawara mwaka 1994)
 
Aprili 29, 1992, Strasser akiwa kijana mwanajeshi mwenye umri wa miaka 25, aliwaongoza wanajeshi wenzake kuvamia Ikulu ya Sierra Leone, wakamteka aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Joseph Saidu Momoh, wakamlazimisha kukimbia, naye akatorokea Conakry, Guinea.

Alipata madaraka siyo kwa mapinduzi ya kupanga. Wakati huo Sierra Leone wanajeshi wa vyeo vya chini walikuwa na hali mbaya kiuchumi hadi walikuwa wanakosa sare. 

Hivyo wakaandama kwenda ikulu kupeleka malalamiko yao kwa rais. Baada ya rais kuona kundi la wanajeshi linaingia ikulu....walimkuta rais amejificha ndani ya kabati lililopo kwenye chumba cha kuogea, kisha wakamteka Rais Joseph Saidu Momoh na wakamlazimisha kukimbia, naye akatorokea Conakry, Guinea.
Image may contain: 1 person 
Valentine Strasser 
 
Hivyo dogo aliyekuwa kinara wa maandamano akaokota dodo kwenye mnazi. Ila kwa sasa anagonga mnazi kama teja vile.

Baada ya Momoh kutorokea Conakry, Strasser alijitangaza kuwa Rais wa Sierra Leone. Maisha yakabadilika, alishakuwa Mkuu wa Nchi, kwa hiyo hakutaka kuishi kwenye nyoyo za Wasierra Leone.


Hakulipa malimbikizo ya mishahara ya wanajeshi na watumishi wengine wa umma. Alifuja almasi ya Sierra Leone, kwa vile jina lake ni Valentine, basi sikukuu ya Valentine’s Day akaifanya kuwa sherehe ya kitaifa yenye mapumziko.


Strasser alikuwa na mbwembwe nyingi, mwaka 1993 katika mkutano wa Wakuu wa Serikali katika nchi za Jumuiya ya Madola, uliofanyika Limassol, Cyprus, alitinga kwa mbwembwe akiwa amevaa suruali ya jeans na fulana yenye maandishi Sunny Days in Cyprus (Siku za Jua Kali Cyprus).

Alikuwa mtu wa starehe, vurugu nyingi kwa wanawake, aliua watu wasio na hatia. Strasser alisahau kuwa ipo siku uongozi hautakuwa kwenye mikono yake, na ambacho kinaweza kumfaa ni kuishi ndani ya mioyo ya watu ili wamtetee na kumpigania baadaye.


Januari 16, 1996, Strasser alipinduliwa na msaidizi wake, Brigedia Jenerali Julius Maada Bio. Strasser akakimbilia Uingereza, akajiunga na Chuo Kikuu cha Warwick, kilichopo mjini Coventry, akaanza masomo ya sheria, akasema anataka awe wakili ili awatetee Waafrika.

Mwaka mmoja wa masomo, Strasser aliishiwa fedha, akaacha chuo. Maisha Uingereza yakawa magumu, akakimbilia Gambia nako kukawa pagumu, mwisho akarudi Sierra Leone, mjini Grafton, Mashariki ya Mji Mkuu wa nchi hiyo, Freetown.


Kazi ya kwanza ambayo Strasser aliifanya ikawa kuanzisha kichuo kidogo cha kufundisha kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Maisha ya chuo yakamshinda.

Baada ya kila kitu kwenda kombo, Strasser alirudi nyumbani kwa mama yake mzazi na kuishi kwenye banda la uani. Hata sasa, akiwa na umri wa miaka 49, anakunywa pombe za kienyeji mtaani. Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu.


Strasser anaishi kama mtu tu mtaani. Mlevi na hakuna anayemjali. Hana mtu wa kumtetea wala kumpigania kwa sababu hakuishi kwenye nyoyo za watu. Strasser ndiye Mkuu wa Nchi wa zamani, anayeishi kimaskini kuliko wote duniani.

Picha Valentine Strasser alivyo sasa. Hana hadhi yoyote kama kiongozi mkuu wa nchi mstaafu. Strasser anaishi kama mtu wa kawaida tu mtaani. Mlevi na hakuna anayemjali.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: