GARI LA MBUNGE LAUA MWENDESHA PIKIPIKI
Magu. Mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, Moses Mjuni amefariki dunia baada ya kugongwa na gari la Mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko katika Kijiji cha Kishamba wilayani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Khadija Nyembo alisema jana kwamba ajali hiyo ilitokea juzi saa mbili usiku, “Gari la mbunge lilimgonga mtumishi wetu wa Hospitali ya Magu ambaye alikuwa anaendesha pikipiki na dereva wa gari hilo amekamatwa yupo polisi,” alisema Nyembo.
Akizungumza kwa simu jana, Matiko alisema ajali hiyo ilitokea takribani kilomita 10 kutoka Daraja la Mto Simiyu wakati akitoka Mwanza ambako walikutana na mwendesha pikipiki na dereva wake, Kelvin Matango alikuwa akimkwepa baada ya kuingia upande wake.
“Nilitoka Mwanza saa 12:00 jioni kwenda jimboni kwangu (Tarime), tulipopita mbele kidogo karibu kilomita10 kutoka daraja la Mto Simiyu, ghafla alijitokeza mwendesha pikipiki akawa anaendesha kwa kuyumbayumba na dereva alishindwa jinsi ya kumkwepa akamgonga, mimi nilikuja kuona yule mtu ameshafariki dunia,” alisema Matiko.
Matiko alisema licha ya kwamba hakupata majeraha, baada ya kutokea ajali hiyo alipelekwa katika Hospitali ya CF ya jijini Mwanza ambako alipewa dawa na kuruhusiwa.
Hata hivyo, Matiko alisema alikuwa akisikia maumivu makali ya mgongo na mbavu hivyo kutakiwa kwenda kufanyiwa vipimo kuona kama atakuwa amepata madhara.
“Nasikia maumivu makali ya mgongo na mbavu za kulia, nahisi mkanda wa gari ulinibana zaidi, nilitakiwa kwenda hospitali ya CF kufanyiwa uchunguzi lakini nimeshindwa kwa sababu hapa tunapozungumza naenda Magu kumaliza masuala ya polisi kwani dereva na gari vipo polisi,” alisema Matiko.
Alisema baada ya kumaliza kushughulikia masuala hayo ndipo atarudi tena hospitali kufanya uchunguzi wa afya yake.
Mwanajeshi afa, 10 wajeruhiwa Arusha
Katika ajali nyingine iliyotokea mkoani Arusha, askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), George Ngwegeta alifariki katika Kijiji cha Oldonyosambu wilayani Arumeru. Watu wengine 10 wamejeruhiwa katika tukio hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema jana kuwa mwanajeshi huyo pamoja na majeruhi hao, walikuwa wamepanda gari dogo la abiria aina ya Nissan Caravan wakitoka Namanga kuelekea Arusha.
Alisema gari hilo lilipinduka mara tatu baada ya kupasuka tairi la mbele likiwa katika mwendo wa kasi na dereva gari hilo linalofanya safari zake kati ya Arusha na Namanga, Pailoti Pamphili alishindwa kulidhibiti. Kamanda Mkumbo alisema dereva huyo anashikiliwa.
Kuhusu majeruhi, Kamanda Mkumbo alisema hadi jana jioni, walikuwa wamelazwa katika Hospitali za Selian na Mount Meru na watano kati yao hali zao hazikuwa nzuri.
0 comments:
Post a Comment