KLABU YA POLISI MORO SC YAKABIDHIWA KWA RAIA
Juma Mtanda, Morogoro.
Klabu ya Polisi Morogoro SC iliyopo ligi daraja la kwanza Tanzania bara imekabidhiwa kwa Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo baada ya jeshi hilo kabiliwa na majukumu ya ulinzi na usalama mkoani hapa.
Akizungumza na MTANDA BLOG mjini hapa katika mahojiano maalumu, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Odilo Tweve alidokeza kuwa timu ya Polisi Moro SC kwa sasa ipo mikononi mwake baada ya uongozi wa jeshi hilo kumkabidhi timu tangu 15 Juni mwaka huu.
Tweve alieleza kuwa uongozi wa jeshi la polisi mkoa wa Morogoro ili jeshi hilo liweze kutekeleza vyema majukumu ya ulinzi na usalama kutokana na hivi sasa kutoweza kuendesha shughuli za mpira hasa timu ya Polisi Morogoro ambayo inashiriki ligi daraja la kwanza.
“Nimeandikiwa barua ya kunikabidhi timu kama Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Polisi Morogoro tangu Juni 15 mwaka huu baada ya uongozi wa polisi mkoa wetu kuwa na majukumu ya ulinzi na usalama waliyonayo na hawataweza kuendesha timu.”alieleza Tweve akinuu baadhi ya maneno kwenye barua hiyo.
Tweve alieleza kuwa katika barua hiyo, uongozi wa polisi mkoa umeomba kumkabidhi timu hiyo kwa uongozi wa timu ili iweze kuona namna gani inaweza kuiendesha na kuwakilisha mkoa huo ili wao polisi wabakiwe na kazi yao kuu ya ulinzi na usalama wa raia na mali zao.
Barua hiyo iliyosainiwa na Kaimu Kamanda wa polisi Morogoro (ACP), Maisha Maganga yenye kumbukumbu MRG/A.23/2/VOL.V208 imetanguliza shukurani zao za dhati kwa kutekeleza na nakala kwenda kwa mkuu wa mkoa, Meya wa Manispaa ya Morogoro na kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro.
Akizungumzia hatua ya kukabidhiwa timu hiyo, Tweve alieleza kuwa kazi iliyopo mbele yake kwa sasa ni kuitisha kikao na wadau wa soka ili kuinusuru isivutwe ama kushuka daraja.
“Jukumu lililopo mbele yangu ni kuitisha kikao na wadau wa soka ili kuangalia namna ya kusajili wachezaji lakini isiangukie katika janga la kushuka daraja ama kuvutwa na TFF.”alieleza Tweve.
Tweve aliwataja baadhi ya wadau wakuu wanaoisaidia timu hiyo kufanya usajili na mambo mengine kuwa ni mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdullaziz Abood, Ahmed Islam, Mbaraka Al Saed (Mbala), Herry Kihongozi na chama cha soko mkoa Morogoro (MRFA) wengine.
“Kuna wadau wengi wamekuwa wakitoa sapoti kubwa katika hii timu kwa kutoa msaada na timu tayari imeanza mazoezi asubuhi na mchana.”aliongeza Tweve.
0 comments:
Post a Comment