WAZIRI NDALICHAKO AWATAKA WATANZANIA KUWAENZI MARIA NA CONSOLATA UVUMILIVU NI SILAHA KATIKA MAISHA
Iringa. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Joyce Ndalichako aliwataka watanzania kuwaenzi pacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti kwa kujituma katika kazi.
Akizungumza katika ibada ya kuaga miili ya pacha hao waliofariki dunia katika hospitali ya mkoa wa Iringa, Juni 2, 2018, Profesa Ndalichako amesema pacha hao wameifundisha jamii kuwa uvumilivu ni silaha pekee katika maisha.
Amesema jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kuwapenda na kuwaenzi watu wenye ulemavu na kutowafichwa kwa kuwa hakuna anayeijua kesho.
"Maria na Consolata mmelala hapo mbele Mungu awape pumziko la milele, maisha yenu yamekuwa ushuhuda mkubwa kwetu," amesisitiza.
Profesa Ndalichako amesema hakuna haja ya kutengeneza mafarakano kuanzia ngazi ya familia, "Maisha yao duniani yamekuwa ya kujituma na ushuhuda mkubwa kwetu."
Kuhusu elimu yao, Profesa Ndalichako amesema Serikali iliwapatia ruzuku na sio mkopo kama ilivyo kwa wanafunzi wengine.
Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Walemavu, Ikupa Alex amesema mambo mawili ya kujifunza kutoka kwa pacha hao ni kutokata tamaa na kujiamini.
“Walemavu wengi hawajiamini kwa sababu tangu kwenye familia wameandaliwa mazingira ya kutojiamini, walemavu wenzangu tujiamini," amesema ambaye pia aligusia miundombinu ya baadhi ya majengo nchini kutokuwa rafiki kwa walemavu.Mwananchi
0 comments:
Post a Comment