BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKATI JAJA NA TEGETE WAKIING'ARISHA YANGA SHINYANGA, SIMBA SC YAENDELEZA REKODI HUKU AZAM FC YANYUKWA LIGI KUU TANZANIA BARA.


Shinyanga. ‘Wametoa gundu’. Hicho ndicho unachoweza kusema kwa Jerryson Tegete na Genilson Santos ‘ Jaja’ walipofungia Yanga kwa mara ya kwanza, wakati Simba wameendeleza rekodi ya sare jijini Mbeya na Azam wakiambulia kipigo.


Baada ya kucheza kwa dakika 360, bila ya kuziona nyavu, Jaja aliifungia Yanga bao la kwanza kabla ya Tegete aliyetokea benchi kufunga mabao mawili katika ushindi mnono wa magoli 3-0 dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.


Wakati Yanga wakipata ushindi uliowaweka kileleni kwa saa 24.00 kabla ya Mtibwa kuivaa Mbeya City leo, watani zao, Simba walipata sare ya tano msimu huu baada ya kuiruhusu kirahisi Prisons kusawazisha bao kwenye Uwanja wa Sokoine na matokeo kuwa 1-0 .


Mabingwa watetezi, Azam walipokea kipigo cha kwanza cha 1-0 kutoka kwa JKT Ruvu kwenye uwanja wao, Azam Complex.


Shinyanga; Wenyeji Stand United walianza mchezo kwa kasi na kulishambulia kwa kasi lango la Yanga, lakini washambuliaji Mussa Said, Salum Kamana walikosa utulivu.


Dakika ya tano ya mchezo mashabiki wa Stand United waliingia uwanjani na trekta wakiwa juu ya kijiko na kushangiliwa kwa nguvu.


Kipa wa Stand, John Mwenda alinusurika kupata kadi nyekundu baada ya kumchezea vibaya Jaja kwenye eneo la penalti, lakini mwamuzi hakutoa adhabu yoyote.


Jaja aliwainua mashabiki wake kwa kufunga bao la kuongoza dakika 12, akimalizia mpira uliopigwa na Andrey Coutinho na kugonga mwamba na kumkuta akiwa nafasi nzuri na kuusukumia mpira wavuni na kumwacha kipa Mwenda asijue la kufanya.


Baada ya Yanga kupata bao waliamka na kushambulia huku Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite wakitawala vizuri eneo la katikati ya uwanja kabla ya Stand United kurudi mchezoni na kumiliki mpira kama walivyoanza na timu hizo kwenda mapumziko matokeo yakiwa 1-0.


Imani za kishirikina
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, baada ya filimbi ya mapumziko wachezaji wa Yanga waligoma kwenda kwenye vyumba vya kubadilishia nguo na kuamua kwenda kukaa jukwaa kuu.


Kitendo hicho kilisababisha vurugu, huku kocha Marcio Maximo akipigwa ngumi na mashabiki wengi waliokuwa wakirusha chupa. Polisi wachache waliokuwa uwanjani walishindwa kuzuia vurugu hizo, hata hivyo wachezaji wa Yanga wanakubali kushuka jukwaani na kwenda kukaa katikati ya uwanja.


Kipindi cha pili, kocha Maximo aliwapumzisha Coutinho, Jaja na Niyonzima na kuwaingiza Hussein Javu, Tegete na Nizar Khalfan mabadiliko yaliyozaa matunda kwa Yanga.


Yanga walitawala mchezo na kufanikiwa kupata bao pili lililofungwa na Tegete, dakika 77, akimalizia vizuri pasi ndefu ya Twite.


Tegete alifunga bao lake la pili dakika ya 90, akiunganisha krosi ndogo iliyopigwa na Mrisho Ngassa na kuwanyamazisha kabisa mashabiki wa Stand United.


Mbeya; Kibarua cha kocha Patrick Phiri kipo shakani baada ya Simba kulazimishwa sare 1-1 na Prisons.


Simba kama kawaida yao walipata bao la kuongoza dakika ya tatu, lililofungwa na Emmanuel Okwi kwa mpira wa adhabu iliyokwenda moja kwa moja wavuni.


Simba ilipata adhabu hiyo baada ya beki wa Prisons, Jumanne El-Fadhil kumchezea vibaya Ramadhani Singano nje kidogo ya eneo la 18. Prisons walisawazisha bao hilo dakika 86, kupitia kwa Hamis Maingo na kuzima ndoto ya Simba ya kupata ushindi wa kwanza msimu huu. Matokeo hayo yaliwafanya wachezaji wao, Manyika Peter na Okwi kuangua kilio baada ya filimbi ya mwisho ya mchezo.


Chamazi; Mabingwa watetezi, Azam wamepokea kipigo cha kwanza kutoka kwa JKT Ruvu.
Samwel Kamuntu aliiyeingia akitokea benchi alifungia JKT Ruvu bao pekee dakika 45, kwa shuti kali akiunganisha kwa shuti krosi ya Najim Magulu.


Kocha wa JKT Ruvu, Fred Minziro alilazimika kufanya mabadiliko dakika ya sita baada ya Idd Mbaga kubanwa na misuli ya paja na kulazimika kutolewa nje nafasi yake kuchuliwa na Kamuntu.


Katika mchezo mingine, Kagera Sugar ililazimishwa sare 1-1 nyumbani na Coastal Union. Wenyeji walipata bao kupitia kwa Paulo Maona, dakika ya27, kabla ya Coastal kusawazisha kupitia kwa Ramadhani Salim. Jahazi la Ndanda limezidi kuzama baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Mgambo JKT, shukrani kwa bao la Ally Nassoro katika dakika ya tatu.


Nao Ruvu Shooting wametumia vizuri uwanja wao wa nyumbani kwa kuichapa Polisi Morogoro 1-0, bao la Kassim Daby akiunganisha kona ya Hamis Nguya.


Wakati huohuo; Katika Ligi Daraja la Kwanza, pambano la Oljoro na Burkinafaso lilivunjika dakika 89, baada ya mwamuzi kukataa bao la pili la Oljoro lililofungwa na Cleaner Kabala na kuzuka kwa vurugu uwanjani hapo. Oljoro ilipata bao la kuongoza lililofungwa na Ramadhani Mwinyimbegu, dakika ya tano.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: