DK BASHIRU ARITHI MIKOBA YA KINANA CCM
Kamati kuu ya Chama Cha Mapinduzi CCM nchini Tanzania imemteua Dkt. Bashiru Ali Kakurwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho.
Aidha Raymond Mangwala ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) ndani ya chama hicho tawala katika mkutano wa siku mbili uliomalizika jijini Dar es Salaam.
Siku ya Jumatatu CCM kilipokea barua ya kustaafu ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho tawala Abdulrahman Kinana.
Akizungumza katika kikao hicho, mwenyekiti wa chama cha CCM rais wa Tanzania John Magufuli amepongeza kazi iliyotokana na tume iliyokuwa chini ya uongozi wa Dkt Bashiru iliyoshughulika na uhakiki wa mali za chama na kusema kwamba anatumai kuwa katibu mkuu huyo mpya atatumia aliyoyaona katika kukiendeleza chama katika wadhifa huo mpya.
'Tumekupa jukumu hili tukiwa na matumaini makubwa kwamba yote uliyoyaona kwa miezi mitano sasa ukayafanyie kazi katika Chama chote na jumuia zake kwa nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM', amesema Rais Magufuli. Wajumbe wa CCM katika mkutano wa siku mbili uliomalizika jijini Dar es Salaam.
Kuondoka kwa Kinana ndani ya Chama kulizua maswali kuhusiana na nani ataweza kuvaa viatu vyake, na hasa baada ya kurejea kazi alizozifanya za kisiasa kwani Kinana aliongoza kampeni za rais wa awamu ya tatu Benjamini Mkapa, na kusimamia kazi mbali mbali za utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Falsafa yake ya kijamaa, imejenga wasifu wa nje wa Kinana unaoakisi kusimamia kile alichokiamini ndani ya chama chake,huku akitajwa kubobea katika uenezi na ambaye amepata mafunzo katika nchi mbali mbali za kikomunisti jambo ambalo linazidisha kuendelea kuhitajika kwake hata alipoamua kustaafu.
Hata hivyo katika shughuli za ujenzi wa chama akiwa katibu mkuu wa chama , Kinana alizunguka nchi nzima kufanya shughuli mbali mbali za chama akishirikiana na watu katika kazi za mikono na kula nao chakula jambo ambalo linatajwa na baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa kwamba lilikiimarisha zaidi chama hicho na kuongeza mshikamano.
Ni mtu ambaye amekuwa akiiamini na kuitekeleza falsafa ya kijamaa,haiba yake ikionyesha uwezo wa kujenga umoja na kuunganisha watu ndani ya chama chake,kuondoka kwake kuna acha swali kwamba je ni nani baada yake atakayevaa viatu vyake,hilo ni jambo la kusubiria moshi mweupe kutoka ndani ya kikao cha halmashauri kuu ya chama taifa ambacho kimeendelea kwa siku ya pili leo. Abdulrahaman Kinana
Abdulrahman Kinana ni nani?
Abdulrahman Kinana alizaliwa miaka 66 iliyopita Arusha, Kaskazini mwa Tanzania
Kinana ni mwanasiasa nguli aliyeshika nyadhifa mbalimbali serikalini.
Alihitimu shahada yake katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani akibobea kwenye masuala ya mikakati.
Alikuwa Waziri wa ulinzi na Jeshi la kujenga taifa naibu Waziri wa mambo ya nje na uhusiano wa kimatafa na Waziri wa ulinzi.
Kinana aliwahi kufanya kazi na Jeshi la wananchi la Tanzania kwa miaka 20 kabla ya kusaafu akiwa na cheo cha ukanali mwaka 1972.
Abdulrahman Kinana pia aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika mashariki mwaka 2001 mpaka mwaka 2006.
Ni mwanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alikuwa mstari wa mbele katika kampeni za urais kuanzia mwaka 1995 wakati Rais Benjamini Mkapa alipokuwa katika harakati za kuwania urais halikadhalika katika kipindi cha Rais mstaafu Jakaya Kikwete.
Kinana aliwahi kuwa mwakilishi wa diplomasia wa rais wa Tanzania katika eneo la maziwa makuu na kabla ya hapo alikuwa mwenyekiti wa mawaziri wa ulinzi wa nchi za kusini mwa Afrika, SADC wakati huo akiwa Waziri wa ulinzi katika serikali ya Rais wa pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi.
0 comments:
Post a Comment