SITOSAHAU VITISHO NILIVYOKUWA NAPEWA
MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) ambaye atastaafu rasmi Juni 30, mwaka huu, amesema katika kazi zake amewahi kupokea vitisho kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali.
Dk. Bisimba ameitumikia nafasi hiyo ya uongozi kwa miaka 22 na tayari Mei 28, mwaka huu, bodi ya LHRC ilimteua Anna Henga kuwa mkurugenzi mpya wa kituo hicho na ataanza rasmi majukumu yake ifikapo Julai Mosi.
Mwanaharakati huyo ambaye anaacha kumbukumbu nzito katika taasisi hiyo inayojishughulisha na masuala ya haki za binadamu, aliiambia MTANZANIA kuwa amepitia changamoto nyingi zikiwamo za kutishwa.
“Changamoto kubwa ni pale uongozi wa nchi na baadhi ya watu kutotaka kuelewa kazi yetu na kulazimisha kutwambia kuwa tunatumika au sisi ni vyama vya siasa.
“Tulianza kwa kuitwa watu wa Mtikila (Marehemu Christopher Mtikila), baadaye NCCR-Mageuzi mara Chadema na kisha Ukawa.
“Nimewahi kutishwa na baadhi ya viongozi wa Serikali, mfano kuna kiongozi mmoja aliwahi kuniambia nimetangaza vita, kwahiyo na yeye amejiandaa kupambana na mimi,” alisema bila kufafanua.
Alipoulizwa alijisikiaje alipokuwa akishutumiwa katika mitandao ya kijamii kuwa anaitumikia Chadema, alisema: “Ukweli nilikuwa nawaonea huruma hao watu waliokuwa na mawazo finyu na hasi.
“Baadhi yao walipopatwa na shida walifika katika kituo chetu kuomba msaada na kukiri kuwa walikuwa hawaelewi kazi zetu, maana baadhi yao walikuwa watendaji wa Serikali na wakawa wamedhulumiwa haki zao na wakaelekezwa kituoni kwetu.
“Na pia hata sasa kuna wanaoamini hivyo, lakini kuna muda watapata fursa ya kuujua ukweli, nao utawaweka huru.”
Alisema jambo ambalo huwa hasahau katika harakati zake, ni pale walivyoweza kufungua shauri mahakamani dhidi ya kauli ya aliyekuwa Waziri Mkuu, wakati huo, Mizengo Pinda, aliyepata kusema bungeni kuwa watu wapigwe tu.
“Sitasahau pia tulivyowezesha wananchi vijijini, ambao sasa wamesimama wakiwa wasaidizi wa kisheria katika maeneo yao huko Tarime, Kiteto, Babati, Loliondo, Singida, Simanjiro, Tandahimba, Ludewa, Nanyumbu, Maswa na kwingineko.
0 comments:
Post a Comment