RWANDA imeamua ‘kucheza rafu’ kwa kuanza kuhujumu Bandari ya Dar es
Salaam, kwa kupandisha ushuru wa barabara kwa magari ya mizigo
yanayotoka Tanzania pekee kuanzia Rusumo hadi Kigali, kutoka dola za
Marekani 152 za awali, hadi 500.
Kwa mujibu wa taarifa za uhakika kutoka ndani ya kikao cha Baraza la
Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichomalizika hivi karib
uni
Arusha, ushuru huo ulianza kutozwa rasmi kwa magari hayo juzi.
Hali hiyo imesababisha mtafaruku katika eneo la Rusumo, mpakani mwa
Tanzania na Rwanda, ambako zaidi ya malori 200 yenye mizigo kutoka
Bandari ya Dar es Salaam, yamekwama kwa kushindwa kulipa kiwango hicho
kipya cha ushuru wa barabara.
Awali nchi hiyo ilikuwa ikitoza ushuru wa dola za Marekani 16 kwa
kila kilometa 100, ushuru ambao ndio uliokuwa ukitozwa na Tanzania kwa
malori yaliyokuwa yakipitisha mizigo kwenda nchi za nje.
Hata hivyo, katika kilichoonekana kuwa mazingira yasiyo sawa ya
kupata faida kutokana na udogo wa eneo wa nchi hiyo, Rwanda iliamua
kupandisha ushuru huo, kutoka dola 16 kwa kilometa 100, hadi dola 152
bila kuzingatia kilometa.
Kabla ya kupandishwa kwa ushuru huo, Tanzania ilionekana kupata
faida, kwa kuwa kutoka Dar es Salaam hadi Rusumo, ni kilometa 1,350 na
hivyo kwa ushuru wa dola 16 kwa kilometa 100, Serikali ilipata dola 216
kwa gari.
Kwa Rwanda taarifa zinaeleza kuwa hali ilikuwa tofauti kutokana na
udogo wa nchi, ambapo kutoka Rusumo hadi Kigali ni kilometa 139, ambao
kwa ushuru huo wa dola 16 kwa kilometa 100, Serikali ya Rwanda ilijikuta
ikiambulia dola 22.24 tu kwa gari.
Kutokana na mazingira yaliyoonekana ya kutopata sawa na Tanzania,
yaliyotokana na udogo wa nchi husika, Rwanda ilipandisha ushuru huo na
kuwa dola 152 bila kujali umbali, kwa kuwa kijiografia haukuwa na msaada
kwao.
Hata hivyo, taarifa zimeeleza kuwa Tanzania haikulalamika kwa
ongezeko hilo la ushuru na iliendelea kufanya biashara na Rwanda kama
inavyofanya na nchi zingine zinazopitisha mizigo yao katika Bandari ya
Dar es Salaam.
Hujuma kwa Tanzania.
Katika mazingira yanayotafsiriwa kuhujumu Bandari ya Dar es Salaam,
nchi hiyo mwanachama mwenza wa Afrika Mashariki, imepandisha ushuru tena
hadi dola 500, mara hii ushuru huo ukiwa kwa magari yanayopita Bandari
ya Dar es Salaam tu.
Ushuru huo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ulitangazwa ghafla muda mfupi
baada ya Kenya kutangaza kuondoa vikwazo vya barabara kwa magari ya
mizigo inayopita katika Bandari ya Mombasa kwenda Kigali.
Mfanyabiashara aliyeathirika na ushuru huo, alisema sasa ni wazi kuna
jaribio la Rwanda kuonesha kuwa usafirishaji wa mizigo kutoka Dar es
Salaam kwenda Kigali, umbali wa kilometa 1,350, ni aghali kuliko
kusafirisha mizigo kutoka Bandari ya Mombasa hadi Kigali, umbali wa
zaidi ya kilometa 2,700.
Taarifa rasmi.
Akizungumza na gazeti hili jana, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles
Tizeba, alikiri Wizara yake kupata taarifa za kupanda kwa ushuru huo
kupitia wafanyabiashara, lakini hadi sasa wizara hiyo haijapewa taarifa
rasmi na Rwanda.
Alisema juzi akiwa katika kikao hicho cha mawaziri wa Afrika
Mashariki, Wanyarwanda walikuwa wakilalamikia kiasi cha ushuru
kinachotozwa nchini katika barabara kuwa ni mkubwa ikilinganishwa na
nchi za Afrika Mashariki.
Alisema kutokana na malalamiko hayo, alilazimika kuwajibu kuwa ushuru
huo ni lazima utozwe kutokana na vigezo vilivyowekwa na lengo lake
kubwa ni kulinda barabara.
“Kama Wizara hatujapata taarifa rasmi, lakini tumepokea malalamiko
kutoka kwa wafanyabiashara kuhusu kutozwa ushuru huo mpya, tunachofanya
sasa ni kuangalia namna suala hili litakavyoathiri usafirishaji na baada
ya hapa, tutashauri wizara za fedha na ujenzi hatua za kuchukua,”
alisisitiza.
Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dk Stergomena Tax ambaye sasa ni Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo
ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), alisema hatua hiyo ya Rwanda
kupandisha ushuru ni ya kutengeneza ushindani usio sawa.
Kwa mujibu wa Dk Tax, kwa sasa Bandari ya Dar es Salaam inafanya
vizuri ikilinganishwa na ya Mombasa na ndiyo maana anaona ushuru huo ni
wa kuweka mazingira yasiyo sawa ya ushindani kati ya Bandari ya Dar es
Salaam na ya Mombasa.
“Tangu Rwanda ilipojiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilikuwa
ikilalamikia vikwazo vya Tanzania vya barabara, lakini ukweli ni kwamba
Tanzania na Kenya zimekuwa zikijenga barabara zake zenyewe, ndiyo maana
ni vema zitengeneze mkakati wa kudhibiti matumizi ya barabara hizo ili
zikiharibika kuwe na fedha za kuzikarabati,” alisema.
Suluhisho
Hata hivyo, Dk Tax alisisitiza kuwa kabla ya kuondoka wizara hiyo ya
Afrika Mashariki, tayari nchi za Jumuiya hiyo zilikuwa na mkakati wa
kuanza kutumia kiwango kimoja cha uzito wa magari kisichozidi tani 55,
ili kuhakikisha miundombinu ya nchi hizo hususani barabara haiharibiwi
na uzito wa magari hayo.
“Hili ndilo suluhisho la pekee iwapo nchi zote za Afrika Mashariki
zitakuwa na kiwango kimoja cha uzito, hata tozo za ushuru zitakuwa sawa
na ushindani inaowaumiza wafanyabiashara hautakuwapo,” alisisitiza.
Msemaji wa Chama cha Umoja wa Wasafirishaji wa Malori nchini (TATOA),
Zacharia Hans-Pope, alikiri kuwa na taarifa za kupandishwa kwa ushuru
huo na hadi jana jioni magari ya mizigo zaidi ya 200 yalikuwa yamekwama
Rusumo kutokana na kushindwa kulipa tozo hiyo.
“Magari zaidi ya 200 yamekwama pale Rusumo kwa kuwa hayana uwezo wa
kulipa tozo hiyo… ni kubwa mno, sisi chama tunasubiri tamko la Serikali
ya Tanzania, kwanza hatukuwa na taarifa kabisa juu ya suala hili,”
alisisitiza.
Alisema ushuru huo utakuwa ‘mwiba’ kwa Bandari ya Dar es Salaam kwa
kuwa utaifanya ionekane kuwa ya gharama kusafirisha mizigo kwenda Kigali
jambo ambalo si la kweli.
Ni nchi za SADC pekee ndizo zenye ushuru mmoja wa barabara ambao ni
dola 16 kwa kilometa 100 za barabara, lakini bado Jumuiya ya Afrika
Mashariki haijaweka kiwango kimoja cha tozo hiyo. HABARILEO
MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO
Home / Uncategories / RWANDA YAIHUJUMU TANZANIA, YAPANDISHA USHURU WA BARABARA KUTOKA DOLA ZA MAREKANI 152 HADI KUFIKIA 500 KWA MAGARI YA TANZANIA PEKEE.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment