WABUNGE SASA KUWAJADILI HOTUBA ZA KIKWETE NA WALIOBA KATIKAM BUNGE MAALUM LA KATIBA DODOMA.
HOTUBA iliyotolewa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba zitajadiliwa bungeni baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kuridhia ombi hilo lililotolewa na baadhi ya wajumbe.
Sitta alikubali hoja hiyo iliyotolewa na Mjumbe wa Bunge hilo Maalum, Julius Mtatiro kupitia mwongozo alioomba jana.
Sitta alisema kiini cha kukubali hoja hiyo ni kufanya wajumbe kupata nafasi ya kujadili na kupata ufafanuzi wa hotuba hiyo kwa lengo la kuwa na Bunge moja na lenye maridhiano.
Rais Kikwete alilihutubia Bunge hilo Ijumaa iliyopita, wakati akifanya uzinduzi rasmi, wakati Jaji Warioba aliwasilisha rasimu ya Katiba Jumanne iliyopita katiba Bunge hilo. Hotuba hizo zimeibua hisia tofauti miongoni mwa wajumbe.
Kutokana na ombi hilo la mwongozo la Mtatiro na baadaye maombi yaliyowasilishwa kwa Mwenyekiti kwa njia ya maandishi, likiwemo la Mjumbe James Mbatia, Sitta alisema mjadala wa hotuba hizo utafanyika kesho.
“Waheshimiwa wabunge kimsingi nimekubaliana na ombi la hotuba hizi zote mbili kujadiliwa hapa bungeni kwa lengo la kupata ufafanuzi na kupeana uelewa mpana wa kile kilichosemwa na watoa hotuba wote wawili ili kutufanya kuwa na Bunge moja.
“Najua wapo wanaotaka kuulizwa maswali na pia wapo wanaotaka kupata ufafanuzi wa hapa na pale kwa hiyo tutatumia muda kidogo tutakaoupata Jumatano (kesho) ili tuzijadili hotuba zote mbili,” alisema Sitta.
Alisema mjadala huo, utafanyika baada ya Kitengo Maalumu cha Rekodi za Hotuba za Bunge (Hansard), kumaliza kuchapisha hotuba hizo, kazi aliyosema ingekamilika leo.
“Kukamilika kwa uchapaji wa hotuba hizi kutatufanya kujadili vizuri zaidi yale yote yaliyosemwa bungeni, maana Hansard inarekodi mambo yote yaliyosemwa. Tukisema tujikite katika kujadili zile hotuba zao zilizochapishwa kabla, hatutajadili vizuri maana baadhi ya mambo waliyaongeza wakati wakihutubia hapa ndani,” alisema Sitta.
Hatua ya Bunge kupanga kujadili hotuba hizo, inakuja baada ya baadhi ya wabunge wa Bunge hilo Maalumu la Katiba kugawanyika.
Lipo kundi la Wabunge linalojulikana kama Tanzania Kwanza, linaloundwa na zaidi ya wajumbe 400 chini ya Uenyekiti wa Mjumbe Said Nkumba, likiunga mkono hotuba ya Rais Kikwete.
Hata hivyo, tayari Umoja wa Wajumbe wanaounda kundi la Umoja wa Katiba ya Watanzania (Uwaka), umeeleza kutounga mkono hotuba ya Rais Kikwete na kusema utasimamia katika kuhakikisha kuwa rasimu ya Katiba mpya, iliyowasilishwa na Jaji Warioba ndiyo inayojadiliwa katika Bunge hilo Maalum la Katiba na si vinginevyo.
Wajumbe wafundwa.
Watu wa kada mbalimbali wameendelea kunyooshea vidole Bunge Maalumu la Katiba, wakitaka wajumbe wake kuzingatia viapo vyao kwa kuhakikisha, wanafuata kanuni na taratibu walizojiwekea, Katiba ipatikane.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Benson Bana alitaka wajumbe wajirudi kwa kutekeleza kiapo chao kuhakikisha wanajadili na kutumia fursa walizonazo vizuri, kushawishi ipatikane Katiba bora kwa Watanzania wote.
Alitaka wajumbe kuzingatia jambo lililowapeleka kwenye Bunge hilo. Dk Bana alisema wajumbe hao kwa sasa wanatakiwa kutambua hawakwenda kwenye Bunge hilo maalumu kufanya siasa za vyama au kuanzisha makundi.
Alisema kazi kubwa ambayo Watanzania wanategemea wajumbe hao kuitekeleza, si malumbano na makundi yanayoendelea kwa sasa, bali ni kupitia vifungu kwa mujibu wa kanuni na taratibu walizojiwekea na kisha kutengeneza Katiba mpya yenye msimamo wa Watanzania.
“Tunaomba wasikiuke kiapo chao, kwa sasa wameacha kabisa lililowapeleka kule na kujadili suala la mfumo wa Serikali kimakundi, hata kama hotuba ya Rais Jakaya Kikwete imewagusa na hawakuitarajia, basi watumie fursa waliyonayo kuijadili hotuba hiyo kwa hoja,” alisisitiza Dk Bana.
“Hoja za Rais Kikwete zinajadilika na ni wazi kuwa hakutoa msimamo kwamba yale aliyosema ndiyo dira ya wajumbe hao, bali alitoa fursa kwao na kuwasisitizia kuwa uamuzi wa mwisho ni wa wajumbe wa Bunge hilo, lakini cha ajabu watu wanajadili eti Rais aungwe mkono au la, huku ni kutaka kujipatia umaarufu,” alisema Dk Bana.
Alisema katika hotuba ya Rais pamoja na kusema mambo mengi ambayo Watanzania wengi wameyapongeza, hakuna sehemu aliyowaelekeza wajumbe wa Bunge hilo Maalum, kuwa maelezo na maoni aliyoyatoa ndiyo msimamo wa mwisho wa kutengeneza Katiba hiyo.
Wakati zikiwepo taarifa kwamba baadhi ya makundi yana mpango wa kufanya ziara kwa wananchi kuzungumzia namna mchakato unavyovurugwa, Dk Bana alisema wajumbe hao hawakuchaguliwa kuunda makundi. Alitaka wafahamu hawakuchaguliwa kuacha vikao vya Bunge ili kuwazungukia wananchi.
“Ndiyo, Sheria inawaruhusu kwenda kueleza maelezo yao kwa wananchi, wafanye hivyo wakitambua kuwa Watanzania wa sasa si mbumbumbu na hawadanganyiki na ukweli ni kwamba kwa sasa hakuna cha kuwafanya waache vikao vya Bunge na kwenda kwa wananchi, kwanza hizo ziara wanafanya kwa gharama ya nani?” Alihoji.
Wanasheria
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Hellen Kijo- Bisimba, alisema kwa hali ilivyo sasa wajumbe hao wanasikitisha, kwa kuwa inaonekana wamesahau kilichowapeleka bungeni.
Alisema iwapo malumbano na makundi yaliyozuka chanzo chake ni hotuba ya Rais Kikwete, walichotakiwa ni kuijadili hotuba hiyo kwa hoja ndani ya vikao vya Bunge hilo na si kujigawa huku kila mmoja akianika msimamo wake.
“Wafuate mfano wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikuwa na wajumbe takribani 34 wenye misimamo tofauti lakini baada ya kupewa kazi ya kutafuta maoni ya wananchi, walijiunga na kuwa wamoja na kufanya kazi hiyo kwa kuzingatia matakwa ya Watanzania na si matakwa yao,” alisema Bisimba.HABARILEO
0 comments:
Post a Comment