WANAOITANA MAJINA YA KEJELI YA MNYAMA TUMBILI NA MWIZI KATIKA UKUMBI WA BUNGE DODOMA WANATUFUNDISHA NINI WATANZANIA ?.
Mwenyekiti wa Bunge, Mussa Azzan Zungu (kushoto) akijaribu kuwasuluhisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema (kulia) na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila katika Viwanja vya Bunge Dodoma jana. Picha na Edwin Mjwahuzi.
INAWEZEKANA sio wengi walioshtushwa sana na kitendo cha Mwanasheria Mkuu wa Serikali kumuita mbunge tumbili.
Kwa Bunge hili lililo chini ya Anne Makinda, tumeshuhudia mengi sana. Tulishahuhudia mbunge akimwambia mwenzake haongei na mbwa bali mwenye mbwa.
Na baada ya kauli hiyo akazawadiwa uwaziri mdogo. Tumeshashuhudia lugha ambazo hazifai kutolewa hata kwa mtu mnayegombana naye zikizungumzwa kama lugha ya kawaida kabisa. Wakati watu wakijadili nani zaidi kati ya mwizi na tumbili, mimi nadhani tujadili tumefika vipi hapa?
JAJI WEREMA.
Lugha hizi zilizokosa staha ni matunda ya tulichopanda. Hata kama zenyewe ni makosa, lakini ni matokeo ya makosa mengine. Haijawa bahati mbaya mtu anayepaswa kuheshimika kutumia lugha ambayo ni ya kudhalilisha utu wa mtu na kumkufuru Mwenyezi Mungu ambaye baadhi ya vitabu vya dini vinatufundisha kwamba alimuumba mtu kwa mfano na sura yake.
Hivyo kushusha utu wa mtu kwa kiwango cha kumuita tumbili sio tu tusi, lakini ni dharau iliyokithiri, ubabe uliopitiliza na jeuri isiyokubalika.
Nilibahatika kutokusikia maneno hayo waliyorushiana watu wawili hao ambao huitwa waheshimiwa. Nimesoma kwenye magazeti kwamba bwana mbunge alianza kumuita ndugu mwanasheria mkuu kuwa ni mwizi. Ndipo ikawa jino kwa jino.
Mwanasheria Mkuu naye akamuita mbunge tumbili. Ni fedhea na aibu kwa taifa. Lakini nini kimetufikisha hapa?
Tumefika hapa kwa sababu hakuna maadili ya uongozi. Tumeona watu wasivyostahili kuwa viongozi wakipewa nafasi zilizowazidi kimo. Imekuwa jambo la kawaida kabisa sasa watu kutokuwajibika kwa makosa yao ambayo kimsingi yanawanyima sifa za uongozi. Hili ni tatizo la msingi.
Kama kuna kanuni yoyote ya maadili ya viongozi wa umma, basi kanuni hizo zitakuwa kwenye makaratasi na kuhifadhiwa kwenye makabati bila utekelezaji wake.
Na Bunge hili la wakati huu tumelishuhudia likikosa nidhamu kwa viwango vya watu kusema sasa hivi kutazama Bunge kwenye luninga iwe kwa wakubwa tu maana hatujui ni nani atafyatuka na kutoa kioja gani.
Mhe Kafulila.
Ikiwa mwanasheria mkuu anaweza kuhamaki na kudhalilisha watu kwa kumuita mwenzake tumbili, tutarajie nini kwa wale ambao hawajui kanuni na taratibu za Bunge?
Mwanasheria huyu atakuwa na mamlaka gani ya kimaadili kukemea wale wanaochukua sheria mkononi? Anakuwa na tofauti gani na wananchi wanaoitwa wenye hasira ambao wakisikia mtu kaitwa mwizi nao wanaanza kumshughulikia mara moja?
Kiumri na kimamlaka, mwanasheria mkuu wa serikali alipaswa kuchukua hatua za kistaarabu za kumkanya mbunge aliyemwita mwizi kama anadhani jina hilo la mwizi si haki yake.
Sio kumuita tumbili. Ikumbukwe kwamba mwizi ni jina analopewa mtu aliyeiba. Hivyo mtu anaweza kuwa mwizi kweli, lakini kamwe mtu hawezi kuwa tumbili isipokuwa kwenye hadithi za watoto.
Jambo jingine linalotufikisha hapa tulipofika ni watu wazima wanaopaswa kuwa na akili zao kwa makusudi au kwa bahati mbaya kutokujua wajibu wao kwa taifa.
Kama ndani ya Bunge wabunge na wanaoingia ndani ya Bunge wangejua kwamba wao wana wajibu kwa raia wa taifa hili tusingefika mahali pa watu kutukanana hadharani, tena katika vikao rasmi.
Kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali angeutambua wajibu wa mbunge kwa wapiga kura wanaolipa kodi ili mwanasheria mkuu alipwe mshahara na marupurupu mengine, kamwe asingethubu hata kufikiria kumuita mbunge tumbili.
Tusi hili linawafikia wapiga kura wote. Kwamba katika wingi wao wamemchagua tumbili awawakilishe bungeni. Tusi hili linawafikia wabunge wote; kwamba miongoni mwao kuna tumbili wanayeshirikiana naye na hata kumuunga mkono au kupambana nae.
Tusi hili, mbaya zaidi linamvua nguo yule aliyelitoa. Linaonyesha kiwango chake cha hekima. Limekuwa mizani ya haki ya kumjua mtu huyu anavyoyachukulia madaraka yake.
Limetupa sura halisi ya mtu huyu anavyowaona wawakilishi wa watu. Heshima yake imedidimia hata kama bado anaonekana mtanashati akiwa amezaa suti ya gharama. Kwa hakika matusi yanayotolewa na wakubwa tena hadharani na katika vikao rasmi ni majanga ya kitaifa!
Jumapili iliyopita niliandika makala kwamba kuna kila sababu ya kupunguza ukubwa wa Bunge. Hatuhitaji wabunge wengi wanaotukanana ndani ya Bunge.
Tunahitaji wabunge wachache makini wanaojua namna ya kuibana serikali itimize wajibu wake. Tunahitaji wabunge wanaojua wajibu wao kwa jamii na wanaojibu hoja kwa hoja.
Kilichotokea siku ya kuitana mwizi na tumbili ni ushahidi zaidi kwamba wingi wa wabunge hausaidii chochote katika kutuletea maendeleo.
Hata hivyo, hebu tuangalie jambo jingine ambalo tunajifunza katika tusi lililorushwa. Kumuita mwakilishi wa watu tumbili. Hapa tunajifunza kwamba watu wenye vyeo katika utawala huu sasa hivi hawajui wala hawatambui kwamba vyeo vyao ni dhamana.
Kwamba kwa niaba ya wananchi wamekabidhiwa madaraka ya kutekeleza mambo kadha wa kadha. Watu hawa wenye madaraka wanajiona wameinuliwa juu ya watu na wanatarajia sasa wasujudiwe kama miungu.
Hawataki waondolewe pale mmoja anapotia shaka kuhusu uadilifu wa mwingine. Hawataki waguswe na ukiwagusa basi wewe ni tumbili. Mnyama dhaifu wa porini asiye na hadhi wala staha ya kuhoji yanayodaiwa kutendwa na kiongozi anayedhani ana utukufu wa miungu.
Na pengine mawazo yao yamefanywa kweli na tabia zetu. Kwamba sisi kama wapiga kura tumekosa uwezo wa kuwaadabisha wale tuliowapigia kura au waliokabidhiwa madaraka ili kututumikia.
Badala ya kuwa na uwezo wa kuwaadabisha wanapoharibu tumekuwa tukikaa kando na kuchukulia kama mambo ya mzaha mzaha tu. Hakuna uwajibikaji kwa kauli au matendo ya viongozi. Na hili lilianza zamani. Wapo waliojiona wako juu yetu kwa viwango vya kutuambia hata ikibidi kula nyasi tutakula bali ndege ya rais itanunuliwa.
Wapo waliosema wasioweza kulipa nauli ya kivuko kutoka ng’ambo moja ya taifa letu kwenda nyingine wapige mbizi. Wapo waliowahi kusema wasiotii amri za polisi wapigwe tu.
Wapo waliosema liwalo na liwe. Wapo waliosema hawataki kura za wafanyakazi. Wapo waliosema Watanzania uwezo wao ni wa kutengeneza juisi tu.
Wapo waliosema Watanzania ni washamba na wavivu wa kusoma. Haya ni machache sana kati ya mengi yaliyosemwa isivyostahili, lakini Watanzania hawakumuwajibisha yeyote.
Lakini ukweli ni kwamba wote wanaotoa au waliotoa maneno haya ya kufedhehesha Watanzania wana ukomo wa madaraka yao.
Kauli hizi za kibabe na nyingine zisizo na staha ni ushahidi kwamba sasa kwa wengi wa viongozi wetu, vyeo sio dhamana tena, ni uthibitisho kwamba maadili ya uongozi yamekufa kifo kibaya na ni kielelezo cha kutosha kuthibitisha kwamba wananchi hawana mamlaka ya kuwaadabisha viongozi wanaochepuka.
Wamechepuka mara nyingi, lakini hatukuweza hata kuwanyooshea kidole na kuwaonya, walau kuna vikundi viliibuka na kumburuza kortini waziri mkuu aliyesema watu wakifanya makosa wapigwe tu. Vinginevyo Tanzania viongozi wanabakia watu wasiokosa hata wakikosa.TANZANIA DAIMA
0 comments:
Post a Comment