BannerFans.com

MBUNGE SUZAN KIWANGA AKWAMISHA KESI MAHAKAMANI MOROGORO

WAKUTUBI WA MAKTABA WANOLEWA KUPITIA PROGRAMU YA "TANZANIA YA KESHO" MORO NA DODOMA

Mkufunzi wa mafunzo ya matumizi ya maktaba kwa wakutubi na wanafunzi shule za msingi kutoka shirika la maendeleo la Korea (KOICA), Ja Young Lee (katikati) akiendesha mafunzo hayo mbele ya wanafunzi wa shule za msingi, kulia ni Mkutubi mkuu maktaba ya mkoa Morogoro, Edward Fungo na kushoto ni Mkutubi msaidizi wa maktaba hiyo, Mashaka Nyama/JUMA MTANDA.



Juma Mtanda, Morogoro.
Samaki mkunje angali mbichi, hii ni methali inayoweza kutumiwa ama kuwahimiza wazazi kupenda kupeleka watoto wenye umri wa kuanza masomo shule za awali na msingi ambako ndiko kuna chimboko la kutengeza maarifa kwa mtoto akiwa darasani ili kuanza kupanua uwezo wa akili wa kuelewa hapa duniani.

Methali hiyo haiwezi kuishia na tafsiri hiyo pekee isipokuwa imepiga hatua na kumtaka mzazi ama mwalimu kuwa na tabia ya kumshawishi mtoto kupenda kusoma vitabu katika maktaba mbalimbali kwa lengo la kupanua wigo wa kuelewa historia mbalimbali zilizowahi kufanyika siku za nyuma.

Usomaji wa vitabu imekuwa ni njia ya kupanua akili ya binadamu ambaye inahitaji matunzo na kurutubisha hasa kwa kusoma vitabu ili kurutubisha na kuipalilia kwa kusoma historia za siasa, saikolojia, sayansi, maisha, falsafa, na uchumi.

Ja Young Lee (33) ni raia wa Korea ambaye ni Mkufunzi wa Wakutubi wa Maktaba na anayefanya kazi Maktaba aliyezaliwa katika mkoa wa Suncheon na kupata elimu hiyo katika chuo kikuu cha Chonnam nchini humo.

“Mimi ni Mkutubi na nafanya kazi katika maktaba pia nafundisha wakutubi wa maktaba nyumbani Korea na hapa Tanzania tangu Augost mwaka 2015 nikiwa na programu ya “Tanzania ya Kesho” inayolenga kuhamasisha wanafunzi kupenda kusoma vitabu katika maktaba.”alisema Ja Young.

Ja Young anaeleza kuwa lengo la Tanzania ya Kesho ni kumfumbua macho na kumwamsha kutoka usingizini lakini kumhamasisha mwanafunzi wa shule ya msingi kutambua matumizi ya maktaba na kupenda kusoma vitabu.

“Katika maktaba nyingi za Tanzania kumejaa vitabu vya lugha ya kiingereza na kuwa vigumu kwa wanafunzi wasiojua kiingereza hasa wanaoingia maktaba kusoma vitabu hivyo na badala yake wamekuwa wakiangalia picha tu.”alieleza Ja Young.

Aliongeza kwa kueleza kuwa baada ya yeye kugundua hilo aliingia kwenye mpango wa kutafsiri vitabu 50 yenye masomo mbalimbali pamoja na hadithi kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili fasaha.”Alieleza Ja Young.

Aliongeza kwa kueleza kuwa aliandika ripoti kwa Shirika la kimataifa la Korea International Cooperation Agency (Koica) juu ya kuomba fedha za kutafsiri vitabu na kutoa fedha kwa ajili ya kutafsiri vitabu 50 kwa lugha ya Kiswahili fasaha ili wanafunzi waweze kuelewa kilichoandikwa ndani ya vitabu.

Mkufunzi wa mafunzo ya matumizi ya maktaba kwa wakutubi na wanafunzi shule za msingi kutoka shirika la maendeleo la Korea (KOICA), Ja Young Lee akiendesha mafunzo hayo kwa wakutubi wa maktaba ya mkoa wa Morogoro, wa kwanza kushoto ni mkutubi Ha Young/JUMA MTANDA.

Program ya “Tanzania ya Kesho” ina lengo la kuwajengea wanafunzi kupenda kujua historia kwa kusoma vitabu mbalimbali lakini maktaba ndio sehemu rafiki ya kusoma vitabu kwa njia nzuri kwani vitabu vimekuwa vikuzwa bei ghali lakini maktaba kuu za mikoa ni rahisi kufika.alieleza Ja Young.

Ja Young alisema kuwa mpaka sasa tayari wakutubi 18 wamepata mafunzo ya kuwahudumia wanafunzi kutumia maktaba na kujisomea vitabu ambapo wakutumia 11 wakitoka maktaba wa mkoa wa Dodoma na saba maktaba ya mkoa wa Morogoro ili waweze kuhudumia jamii katika maktaba.

Wakutubi hao 18 kutoka maktaba za mkoa wa Morogoro na Dodoma wamefunza masomo yakiwemo ya Sheria ya mpango wa maktaba, Mpango wa Maktaba, Kuhusu mpango wa maktaba, Hadithi na namba ya Kitabu.

Katika somo la Sheria ya mpango wa maktaba ipo namna ya mkutubi ya kujua Kitabu kipo maktaba kwa njia ya kutafuta kitabu kizuri na bora na mpango wa mkutubi kumsindikiza msomaji mpaka kwenye kitabu (shelve) kujua ni njia ipi nzuri kwa maktaba, wakutubi, na wasomaji.

Somo la Mpango wa Maktaba inamfundisha mkutubi kujua jinsi gani ataweza kumuonesha msomoji juu ya vitabu vizuri, kutengeneza mpango wa kuwavutia wasomaji vitabu au masomo, katika maktaba kuwe na idara ikiwemo maktaba yenyewe, wakutubi, vitabu, wasomaji lakini wakutubi kujua ni jinsi gani wamefahamu kuwa umefanikiwa.

Kwa upande wa mmoja wa wakutubi wa maktaba ya Dodoma, Judith Lugongo anaeleza katika mpango wa maktaba amejifunza namna ya kuandaa mpango wa maktaba kuhusu kuwafundisha watoto namna kuchagua vitabu vya kusoma na kupata maarifa mbalimbali.

Judith anaeleza kuwa licha ya kupata maarifa ya kuwafundisha watoto pia sasa ana ufahamu wa kutosha wa kufundisha jamii namna ya kutumia maktaba kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali kwa kutumia machapisho na kujua vitabu gani vipo maktaba ili kutumia maktaba kwa kujiendeleza na kuendeleza utamaduni wa mtanzania kwa manufaa ya nchi.

“Nimefurahi kupata haya mafunzo lakini huyu mkufunzi Ja Young Lee ni mbunifu licha ya kutupatia mbinu mbalimbali za kufundisha watoto na kuhudumia jamii tayari ameweka kivutio cha watu wanaotembelea na kupata huduma maktaba wana fursa za kupima urefu wa mwili wake na uzito bure.”alieleza Judith.

Mkutubi Mkuu wa Maktaba ya Mkoa wa Morogoro, Edward Fungo anaeleza kuwa mafunzo hayo yameongeza ufanisi kwa upande wa uongozi wa maktaba kwa kutengeneza vivutio kwa wanafunzi kuvutiwa kusoma vitabu.

Fungo alieleza kuwa baada ya mafunzo hayo wametenegeza pragramu maalumu kwa wanafunzi wote wa shule za msingi kuingia maktaba na kusoma vitabu bure kwa siku za jumamosi lakini kutoa fursa nyingine ya kulipia ada ya uwanachama kwa kulipia sh5,000 kwa mwaka.

“Unaweza kuona namna tunavyounga mkono juhudi za pragramu ya “Tanzania ya Kesho” katika kutoa fursa na kuwavutia wanafunzi kupenda kusoma vitabu katika maktaba yetu ya mkoa wa Morogoro”anaeleza Fungo.

Fungo anaeleza kuwa baada ya wakutubi nane kutoka maktaba ya mkoa wa Morogoro kupata mafunzo hayo kutoka kwa mkufunzi wao, Ja Young Lee walianza juhudi za kusaka wanafunzi 40 kwa ajili ya kuanza kuwahudumia ndani ya maktaba.

“Wakutubi wetu nane wamefaidika na mafunzo haya lakini yalienda vizuri kwa sababu tayari walengwa wakuu “wanafunzi” wamehudumiwa kulingana na muongozo wa mafunzo unavyolenga namna ya kuwahudumia na kutengeneza ushawishi usomaji wa vitabu maktaba”alieleza Fungo.

Mwanafunzi wa darasa la nne shule ya msingi Mwere A Manispaa ya Morogoro, Ally Hassan anaeleza kuwa mpango wa kutafsiri hadithi kutoka kingereza kwenda Kiswahili fasaha ni jambo zuri lakini waendelee zaidi kutafsiri vitabu vingi.

Hassan alieleza kuwa kitendo cha vitabu vya kingereza kutafsiliwa kwa lugha ya kiswahili itasaidia sana kwa wanafunzi kuingia maktaba na kusoma vitabu vingi lugha ya kiingereza imekuwa sio rafiki kwa wanafunzi wengi.

“Lugha ya kiingereza sio rafiki kwa wanafunzi wengi kwani vitabu vya Kiswahili maktaba vipo vichache tofauti na kiingereza hivyo wazo la kutafsiri vitabu kutoka kiingereza kwenda Kiswahili hilo ni jambo la kupongeza.”alieleza Hassan.

Kazi ya kukusanya wanafunzi kutengeneza ushawishi wa kupenda kusoma haikuwa rahisi kwani ilibidi kuwe na michezo kama njia ya kuwavutia na kuwajengea uelewa wa mambo mbalimbali kupitia michezo.

Mwalimu wa Taekondo, Min Ju Kim na Andrew George walikuwa sehemu ya kitengo cha michezo baada ya wanafunzi hao kumaliza kufundishwa na wakutubi.

Kupitia mchezo huo, Walimu hao walifundisha somo la nidhamu, kujihami na adui na kulinda kupitia mchezo wa Taekwondo.

Mwalimu Min Ju Kim anayetoka chuo cha polisi Dar es Salaam anasema kuwa mchezo wa Taekwondo ni sehemu ya kuwahamasisha wanafunzi wa kitanzania kupenda kusoma vitabu katika maktaba ili kujua historia mbalimbali lakini watoto wameonyesha kushika mafunzo yote.

“Mchezo wa Taekwondo ni miongoni mwa utamaduni wa watu wa Korea tumekuwa tukijifunza tangu utoto wetu kama sehemu ya kutujenga kinidhamu, kujilinda pele adui anapotushambulia lakini kutujenga kiafya, kiakili na kujenga mwili wenye ukakamavu.”alieleza Min Ju.

Mwandishi wa vitabu nchini, Evodius Katare amewahi kueleza kuwa ili raia wa Tanzania wawe na utamaduni wa kupenda kusoma vitabu ni lazima kuwe na mfumo bora wa kujenga maktaba katika shule zote za msingi na sekondari.

Katare anaeleza kuwa uwepo wa maktaba nyingi katika shule za msingi na sekondari, kazi itayobakia itakuwa kwa walimu kuhamasisha wanafunzi kusoma vitabu ili kuwa na jamii bora zaidi.
Share on Google Plus

About mtanda blog

Blogger maarufu nchini Tanzania na mwanahabari mkongwe kwenye Tasnia ya habari
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments: